ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 30, 2012

Mgomo wa madaktari:Serikali yakunjua makucha

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akizungumza jambo kwa mkazo hivi karibuni, Jana alitoa msimamo wa Serikali kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea kushika kasi
PINDA ASEMA WASIORIPOTI LEO HAWANA KAZI, MADAKTARI WA JWTZ KUTOA HUDUMA DAR, WENYEWE WATISHIA KWENDA MAHAKAMANI
Waandishi Wetu
BAADA ya madaktari kugomea ombi la Waziri wa Mkuu, Mizengo Pinda kukutana nao jana ili kusikiliza madai yao na kuwasihi wasitishe mgomo, Serikali imetishia kuwafukuza kazi wote watakaoshindwa kuripoti kazini leo huku ikiiagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kupeleka madaktari wake katika hospitali za mikoa.
Mbali ya hatua hiyo, Serikali pia imepiga marufuku mikusanyiko yote ya madaktari hao na kuliagiza Jeshi la Polisi kuwasambaratisha popote watakapoonekana hatua ambayo imepingwa na madaktari hao ambao nao jana wametoa tamko wakisema watakwenda mahakamani kupinga agizo hilo.
Pinda alisema: “Katika hatua iliyofikiwa, Serikali imetambua kuwa madaktariwanaoongozwa na kamati ya mpito hawataki suluhu licha ya juhudi zote ambazo zimekuwa zikifanywa kuwaita ili kushughulikia madai yao. Kuanzia sasa Serikali inahimiza madaktari wote walio kwenye mgomo kuacha mara moja na kuripoti kazini ifikapo kesho asubuhi (leo), Januari 30, mwaka huu, ”alisema Waziri Mkuu na kuongeza:

“Watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo watakuwa wamepoteza ajira zao. Serikali imeshachukua tahadhari za kukabiliana na hali hiyo kwa kuagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa  kupeleka madaktari wake katika Hospitali za mkoa wa Dar es Salaam ili kusaidia wagonjwa walioko hospitalini.”
Madaktari nchini walianza mgomo wao Januari 16, mwaka huu wakitoa madai mbalimbali, ikiwemo kutaka kuongezewa mishahara, posho na kupatiwa nyumba za kuishi.

Januari 25, Pinda akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari  ofisini kwake aliwaangukia wanataaluma hao akisema alikuwa tayari kukutana nao wakati wowote lakini, madaktari hao waligoma na kutaka kiongozi huyo awafuate Ukumbi wa Starlight.

Jana, Waziri Mkuu akiwa katika mchakato huo wa kutafuta suluhu ili kunusuru maisha ya wagonjwa katika hospitali zilizokumbwa na mgomo, aliwaalika kukutana nao katika Ukumbi wa Karimjee lakini licha ya kufika hapo akiwa na jopo la mawaziri pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali, madaktari hao hawakutokea.
Waliokuwa wameambatana na Pinda tayari kwa mkutano huo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, Naibu wake Dk Lucy Nkya, Waziri Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa, na maofisa wengine waandamizi wa Serikali.

Mgomo palepale
Hata hivyo, licha ya onyo hilo la waziri mkuu madaktari hao jana jioni waliitisha kikao na kutoa msimamo kwamba mgomo wao uko palepale.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka alisema leo hawatafanya mkusanyiko wowote kutii amri ya Waziri Mkuu lakini, akasema watakwenda mahakamani kutaka amri hiyo itenguliwe.

Dk Ulimboka alisema  kikatiba, Waziri Mkuu hana mamlaka ya kuzuia mikusanyiko halali ya wananchi hivyo, wataomba Mahakama itengue uamuzi huo huku akisisitiza kuwa mgomo wao uko palepale na kuwataka madaktari nchini kote kuendelea na msimamo huo wa pamoja.

Pinda ageuka mbogo
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kushindwa kukutana na madaktari hao jana, Pinda alisisitiza kwamba  mgomo huo siyo halali kwa sababu haukufuata taratibu. Alisema walipaswa kutangaza mgogoro na Serikali na kisha, kutoa notisi ya siku 60 kabla ya kuanza kugoma.

Katika kuhakikisha kuwa Serikali inawadhibiti madaktari hao, Pinda aliwaagiza watendaji wakuu wa Serikali, wakuu wa mikoa, wilaya na waganga wakuu wa mikoa na wilaya kutembelea hospitali zote kuona na kubaini madaktari wanaoendelea na kazi na wale waliogoma, ili hatua ya kusitisha ajira zao zichukuliwe.

Akizungumzia sababu za madaktari hao kugoma kukutane naye, Pinda alisema walitoa sababu tatu ambazo walielekeza kwake kwa barua waliyomkabidhi katibu wake, mnamo saa 3:00 usiku wa juzi.

Walimtaka awasubiri wenzao walioko mikoani wafike ili kushiriki mazungumzo,walitaka pia ofisi yake kujibu madai yao kwa maandishi ili waweze kuyajadili na kutaka Serikali itoe tamko la kutotoa adhabu ya aina yoyote kwao au mtumishi wa kada yoyote ya afya kutokana na mgogoro huo.

Achambua madai
Hata hivyo, pamoja na tamko hilo la kuwataka kurejea kazini mara moja, Serikali imebinisha hoja zao kadhaa isipokuwa mishahara ambazo zinaweza kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Pinda alisema mshahara unaopendekeza na madaktari hao wa Sh3.5 milioni kwa kila daktari anayeanza kazi ni mkubwa na hauwezi kulipwa kutokana na hali ya uchumi wa taifa kutoruhusu.

Alisema hoja ambazo Serikali iko tayari kuzifanyia kazi ni posho za kulala kazini, kufanya kazi katika mazingira magumu, nyumba, usafiri, mikopo ya gari na bima ya afya.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu alisema hayo yanaweza kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi huku akisisitiza kuwa viwango vya posho vilivyowekwa na madaktari hao ni vikubwa mno.

Alisema Serikali imekubaliana na madai ya madaktari hao ya kuwarejesha katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) madaktari bingwa, waliohamishwa na wizara katika kipindi cha mwaka juzi.
Wizara iliwahamisha madaktari bingwa 61 kutoka MNH na kuwapangia vituo vingine hali iliyosababisha baadhi yao kugoma kuripoti katika vituo hivyo vipya... “Niliona dai hili nikashauri wizara iwarejeshe kwani sisi tunawahitaji waje kuwahudumia Watanzania.”

Zitto: Posho zetu chanzo cha mgomo

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alisema kuwa mgomo huo wa madaktari ni ujumbe kwa Spika, Makamishna wa Bunge na wabunge wenzake kuwa hoja ya posho za walizojiongezea ndiyo inayoleta matatizo hayo.

Alisema kutokana na kujiongezea posho, hoja ya kwamba Serikali haina fedha inakosa nguvu kwa kuwa madaktari watahoji za kuwalipa wabunge zinatoka wapi?

Muhimbili bado hali tete

Mgomo huo wa madaktari unaoendelea nchi nzima umeendelea kuwatesa wagonjwa Muhimbili ambao wamekosa huduma kwa siku 10 sasa.

Katika Taasisi ya mifupa (Moi) ya hospitali hiyo, baadhi huduma zilikuwa bado zimesitishwa.

“Hapa nilipo ni siku ya 10 tangu nifike kwa matibabu. Nilitakiwa kufanyiwa upasuaji wa mguu lakini mpaka sasa sijamuona hata daktari mmoja,” alisema Zebedayo Mwanri aliyelazwa Moi na kuongeza: “Nimekuwa nikipewa dawa za kutuliza maumivu na wauguzi.”

Msemaji Msaidizi wa Moi, Frank Sebastian alisema: “Huduma ambazo zimesitishwa kutolewa ni kwa wagonjwa wa nje ambao wanafika kwa ajili ya matibabu.”

Alisema japo kuna mgomo wa madaktari lakini wao bado wanaendelea kutoa huduma nyingine za dharura.

Habari hii imeandaliwa na  Geofrey Nyang’oro, Boniface Meena Aidan Mhando, Keneth Goliama wa Gazeti la Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

madaktari hawana imprest za safari tofauti na viongozi ambao wanasafiri kila mara.Hivyo wanastahili mshahara mkubwa. Ni kweli kitendo cha kujiongezea posho (allowances)kubwa kwa wabunge kitaendelea kushawishi malalamiko makubwa nchini. Mheshimiwa Rais wawajibishe viongozi wazembe wasilindwe.