MSICHANA mwenye umri wa miaka 13 mkazi wa Majengo Tanesco, mjini Sumbawanga aliyetumikishwa ngono ya lazima kwa miezi saba akitafutiwa wanaume na mwenye danguro kwa ujira wa chakula, ametoboa siri ya kutisha kuhusu biashara ya binadamu inayoendelea
nchini.
Binti huyo ambaye alisema kwamba alirubuniwa kuondoka nyumbani kwao kisha kujikuta
akitumikishwa kwenye ngono kwa miezi saba jijini Mbeya, alifanikiwa kutoroka; na hivi karibuni alizungumza na gazeti hili, akielezea suluba za kuishi katika danguro akitumikishwa ngono kwa zaidi ya wanaume wawili kila usiku.
Binti huyo alisema kwamba hakuwa peke yake, bali zaidi ya 30 ambao waliofungiwa nyumbani
kwa tajiri wakilindwa na walinzi watatu usiku na mchana, lakini usiku husambazwa kwenye baa kwa ajili ya kuuza miili yao, chini ya ulinzi wa wapambe wa `tajiri’.
Alisema kwamba mabinti hao waliotumikishwa ngono walikuwa wakiandaliwa kwenda kufanya ukahaba nje ya nchi hasa Uarabuni na Ulaya.
Kutoroshwa kwake
Ilikuwaje binti huyo akafikia hatua hiyo? Akizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyefanyia uchunguzi wa matukio ya kupotea kwa watoto wa kike mjini hapa sambamba na taarifa za kuwapo biashara ya watoto hususani wa kike, alidai kurubuniwa na mwanamke aliyemtaja kwa jina la Angelina ili atoroke nyumbani kwa bibi na babu yake.
Wakati anatoroshwa Februari 21 mwaka 2011, binti huyo alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika moja ya shule za mjini hapa.
Babu wa msichana huyo, Edwin Ndasi (66) mganga mfawidhi katika zahanati ya Pito, Sumbawanga na bibi yake Lilian Ndasi (54), muuguzi wa zahanati ya Majengo walikiri kutoweka kwa mjukuu wao huyo kwa miezi saba.
Kwa mujibu wa bibi huyo aliyeishi na mjukuu wake huyo Majengo, siku moja alimwamsha aende shule, lakini akakataa akidai anaumwa kichwa na kwamba sare zake za shule zilikuwa zimechakaa.
Kuanzia siku hiyo hakuonekana nyumbani hadi Julai 3 aliporejea nyumbani na kudai kuwa alitoroka kutoka danguro lililopo Mbeya. Akisimulia mkasa uliompata, msichana huyo alisema asubuhi ya Februari 21 mwaka jana alikataa kwenda shule, licha ya kushurutishwa na bibi yake na kusingizia kuwa hakuwa anajisikia vizuri.
"Nilimdanganya bibi kuwa naumwa kichwa, hivyo nisingekwenda shuleni, niliondoka nyumbani baada ya bibi kwenda kazini, nikaenda kwa mama Angelina na kukaa kwake hadi jioni nilipomweleza kuwa nasikia njaa akanipa ugali na maharage.
“Nilipomaliza kula nililala usiku kucha na alfajiri nilijikuta ndani ya teksi na mama huyo na wasichana wawili wa rika langu, tukiambiwa tunakwenda Mbeya," alisimulia msichana huyo.
Alidai kuwa katika maisha yake yote hakuwahi kufika Mbeya, walifika katika nyumba kubwa na kukuta wasichana wengine kama 30 hivi.
Maisha kwenye danguro
Msichana huyo alidai kuwa wakiwa hapo hawakuruhusiwa kutoka, na kwamba nyumba hiyo ilikuwa ikilindwa na walinzi watatu usiku na mchana ambapo kila chumba walilala wasichana watatu.
Usiku teksi ilikuwa ikiwachukua kwa zamu huku wakifuatana na mwanamke wa makamo na mwanamume na kutawanywa kwenye baa chini ya ulinzi.
Msichana huyo ambaye anadai hakuwa akimjua mwanamume yeyote kabla, aliamriwa
kujiuza kwa wanaume katika baa hizo na walikuwa wakirudishwa 'nyumbani' usiku wa manane.
Kwa miezi hiyo mbali ya chakula pia walinunuliwa nguo na viatu vya kutokea usiku kwa ajili ya ‘kazi’ hiyo kwenye baa.
"Mimi nilikuwa nalala chapchap na wanaume wawili kwa usiku mmoja … baada ya maafikiano, matajiri wangu, walinipeleka kwenye nyumba ya kulala wageni kwa muda na kila mteja wangu nilimtoza Sh 10,000, hivyo nikirudi nilikuwa nakabidhi Sh 20,000 kwa tajiri.
“Niliishi maisha hayo ya kuchukiza na machafu ya ukahaba kwa miezi saba hivi," alisema huku akilengwa na machozi.
Kuhusu ratiba ya maisha katika nyumba hiyo, alisema walikuwa wakiamshwa alfajiri na kufanya mazoezi ya viungo ndani ya nyumba, mchana walikula ugali kwa maharage na jioni mazoezi ya viungo tena.
Alidai ilipokuwa inafika saa 12 jioni, walinyweshwa uji wa ulezi na kujipumzisha hadi saa tatu usiku, ambapo walikuwa wakitawanywa kwa zamu kwenye baa. Tajiri wao alikuwa akishirikiana
na Angelina (aliyemtorosha).
Waliwafahamisha kuwa watakaa katika nyumba hiyo kwa muda wakipewa mazoezi na kufanyishwa biashara ya ukahaba hadi hapo watakapohitimu na kupelekwa Urusi na nchi zingine za Uarabuni.
"Miye nilishuhudia wenzetu 10 wakituaga kuwa wanasafiri kwenda Urusi na hivyo tulibaki 20 kwenye ile nyumba; watatu tu ikuwa tukitoka Rukwa (majina tunayo) wengine sikumbuki walikuwa wametoka wapi, maana nadhani tulikuwa tukichanganyiwa dawa kwenye chakula,
kwani muda mwingi tulikuwa kama tumelewalewa hivi," alidai msichana huyo.
Alitoroka vipi?
Alisimulia kuwa alifanikiwa kutoroka nyumba hiyo baada ya kumwibia tajiri wake Sh 30,000 na kumrubuni mlinzi ambaye alimruhusu kuondoka Julai 3 alfajiri na akiwa barabarani bila kujua mwelekeo, alikutana na mama akamwomba amwelekeze iliko stendi kuu ya mabasi.
Msichana huyo alidai kuwa mama huyo bila kumwuliza maswali mengi alimtaka asubiri, kwani naye alikuwa ameagiza teksi impeleke stendi kuu kwa safari ya Sumbawanga, lakini kwa mujibu wa msichana huyo, mama huyo alishukia kijiji kimoja kabla ya Sumbawanga.
“Tukiwa stendi, nilimweleza kuwa naelekea Sumbawanga, naye akanieleza kuwa anauza tiketi moja, kwani mwenzake ameahirisha safari…nilimpa shilingi 17,000 akanipa tiketi yangu nikasafiri hadi Sumbawanga … niliposhuka tu huku nikisita kwenda nyumbani mmoja wa ndugu zetu alinitambua pale stendi na kunisindikiza hadi nyumbani," alisema.
Walezi wanasemaje?
Bibi wa msichana huyo alisema alipomwona mjukuu wake alishangaa, kwani alionekana kukomaa misuli na kama ana tatizo la akili.
Kwa mujibu wa bibi huyo alidai kuwa siku kadhaa baada ya kupotea kwake na kumtafuta sehemu mbalimbali mjini hapo wanafamilia walitoa taarifa Polisi na kufungua jalada la kutoroshwa kwa mwanafunzi yenye namba Sum/RB/1236/2011 kwenye kituo cha Polisi mjini humo, kisha wakatoa taarifa shuleni alikokuwa akisoma msichana huyo.
"Kwa kuwa mjukuu wangu alikuwa amesajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba, aliporejea nyumbani tulimpeleka shuleni akaruhusiwa kufanya mtihani wake wa darasa la saba, lakini matokeo yalipotoka alikuwa amefeli,” alisema bibi wa msichana huyo.
Kwa mujibu wa babu, sasa wana mpango wa kumpeleka kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ukiwamo wa kisaikolojia ndipo atakapokuwa ametulia waamue wafanye nini.
"Mjukuu wetu huyu alipokuja alionekana kubadilika tabia akifanya vitendo vya ajabu kwani alikuwa akilala kuanzia saa 12 jioni hadi kesho yake saa saba mchana, sasa naona ameanza kuwa kawaida,” alidai bibi huyo .
Chanzo:Habari Leo
3 comments:
Kweli mwisho wa dunia .pole mtoto ndio maisha uombe mungu uwe ujapata gonjwa la ukimwi.ukiona hivyo ndio mwisho wa dunia.dunia imebadilika sasa matukio ya hivyo yako mengi .
Mmmmhhh dunia inamambo,Mungu awaokoe hao watoto jamani.
pole binti...jitahidi kukumbuka ulipokuwa umefichwa uko mbeya ili ukomboe wenzio ambao umewaacha wakiteseka na hawajui watatokaje kwenye janga hilo. Dunia ina watu wabaya sana ...
Post a Comment