ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 21, 2012

Naibu Waziri chupuchupu kuvuliwa uanachama MAT


CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT) kimezima jaribio la madaktari waliopendekeza 
kuvuliwa uanachama wa chama hicho Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya. 

Madaktari wanaoendelea na vikao vya kudai ongezeko la posho na mishahara katika ukumbi wa Don Bosco, Dar es Salaam jana, walipendekeza kuvuliwa uanachama kwa Dk. Nkya kwa madai ya kusaliti fani ya udaktari na kuvunja miiko na maadili ya udaktari. 

“Walipendekeza Dk. Nkya naye avuliwe uanachama kwa kipindi cha mwaka mmoja kama 
mwenzake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa, kwa kosa lile lile la kusaliti fani ya udaktari na lile la kuvunja miiko na maadili ya udaktari kama yanavyosomeka kwenye kiapo cha udaktari.
 

“Kiapo hicho kinasema kila daktari atatambua na kuthamini madaktari wenzake kama ndugu zako na kuwatendea wema, kuwapenda na kuwaheshimu. Chama cha Madaktari Tanzania kitawafikiria kwenye mkutano ujao wa kawaida. Hii maana yake nini? Wamepoteza sifa ya kuwa weledi wa utabibu! Wamebaki kuwa wataalamu wa udaktari tu,” alisema mmoja wa madaktari ambaye hakutaka kutajwa jina. 

Hata hivyo, akizungumzia jaribio hilo, Makamu wa Rais wa MAT, Dk. Primus Saidia alisema pamoja na baadhi ya madaktari kupendekeza hilo, lakini katika majumuisho yaliyofikiwa na MAT suala hilo halijaafikiwa. 

“Ni kweli lilikuwa moja ya mapendekezo yaliyotolewa na baadhi ya madaktari, kama unavyojua kila mwanachama ana uhuru wa kutoa maoni yake, lakini katika maazimio, suala 
hilo halijakubaliwa. 

“Dk. Nkya anaendelea kuwa mwanachama halali. Unajua sisi kazi yetu ni kusimamia taaluma na kuona misingi ya udaktari inafuatwa bila kuegemea upande wowote. Kazi yetu ni kusaidia madaktari wanaponyimwa haki yao na pia kuipongeza Serikali inapofanya jambo jema kwa madaktari,” alisema Dk. Saidia. 

Kuhusu nini Ofisi ya Waziri Mkuu imeamua baada ya kufikisha suala hilo huko, Dk. Saidia alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliagiza suala hilo lirejeshwe kwenye meza ya majadiliano ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili lipatiwe muafaka.


Habari Leo

No comments: