ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, January 8, 2012

Ripoti Maalumu:Saratani inavyowatesa albino, watelekezwa na waume zao

Agnita
Florence Majani
UPANDE wa kulia wa uso wa Agnita Malolela ambaye amelazwa katika Hosipitali ya Saratani Ocean Road, Dar es Salaam hauna sikio na ngozi yake imevurugika na kuharibika kwa namna isiyoelezeka.

Upande wa kushoto wa uso wa mama huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Matondo, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, una kidonda kingine kikubwa ambacho kinachuruzika damu. 

Ni picha ambayo hakuna mmoja kati yetu ambaye angependa kuiona, lakini huu ni uhalisia katika mwilini wa binadamu mwenzetu.Licha ya Agnita ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino) kuwa na maumivu makali kutokana na hali hii ya ugonjwa, hana jinsi kwani analazimika kumnyonyesha mtoto wake wa kiume, Ezra au Baraka mwenye umri wa miezi miwili sasa.

Mbali na Agnita, mgonjwa mwingine ni Tereza Nzinza (34) ambaye alifika Dar es Salaam Septemba 20, mwaka jana akitokea kijiji cha Punze, Wilaya ya Kahama, Shinyanga.

Upande mmoja wa uso wa Tereza umevimba huku jicho lake likiwa limeharibika kabisa na ni takriban miaka mitano sasa tangu saratani ianze kumtafuna mwanamama huyu mlemavu wa ngozi.
 
“Hivi sasa nahesabu sina jicho (analigusa), hata meno manne ya chini nayo yamelegea kwani uvimbe umepita hadi kwenye fizi zangu,” anasema Tereza.

Machozi haya hayakomei kwa Tereza na Agnita pekee, bali yanamtoka pia mwanamke mwingine ambaye pia ni mlemavu wa ngozi, Martha Mabula.

Martha ambaye ni mkazi wa Geita, mkoani Mwanza anasema ana maumivu makali sana kutokana na ugonjwa wa saratani.

“Maumivu ni makali mno, usiku silali kabisa, ninageukageuka tu,” anasema Martha ambaye ni mama wa watoto wanne.

Martha anasema, alifika katika hospitali ya Ocean Road kwa msaada wa majirani na marafiki ambao walimchangia fedha za nauli. 

Ugonjwa wao
Agnita alifika Dar es Salaam mwezi Agosti mwaka jana akitokea Dodoma na wakati huo alikuwa mjamzito wa miezi sita, ujio ambao ulitokana na rufaa aliyopewa katika Hosipitali ya Mkoa wa Dodoma.

Alikwenda hospitalini Dodoma kutokana na uvimbe uliojitokeza kwenye sikio la kulia na kumsababishia maumivu makali.

“Niliona uvimbe mdogo nyuma ya sikio langu  na kadri siku zilivyopita maumivu yalizidi na uvimbe huo kukua,” anasimulia Agnita.

Anasema, alitibiwa katika Hospitali ya Dodoma kabla ya kupewa rufaa kwenda hospitali ya Muhimbili ambako alifanyiwa vipimo na madaktari kuamua afanyiwe upasuaji.

Alisema madaktari walisita kumpa tiba ya mionzi kutokana na ujauzito na kwamba upasuaji aliofanyiwa kuondoa uvimbe uliacha shimo kubwa nyuma ya sikio lake.

Agnita anafafanua kuwa madaktari walilazimika kukata nyama kutoka kwenye ziwa lake lake la kulia ili kuziba shimo hilo na wakati huohuo iliwabidi kumfanyia upandikizi wa ngozi unaojulikana kitaalam kuwa skin grafting kwa kukata ngozi yake paja.

“Unaona hapa..” anaonyesha jeraha kubwa la nyuzi kumi na sita lililopita kuzunguka ziwa lake la kulia, kisha  anaonyesha paja lenye alama ya umbo la pembe mraba, alipochunwa ngozi.

Anasema aligundulika kuwa na saratani inayotafuna mifupa ya kichwa chake mwaka jana mwishoni na kwamba amekuwa akipata maumivu makali yasiyoelezeka.

“Usiku huwa naumwa zaidi, kichwa kinauma mno, hapa nilipo sisikii vizuri upande wa kulia, ukitaka uzungumze nikusikie inabidi ukae upande wa kushoto,” anasema Agnita huku akimnyonyesha mtoto wake.

Kwa upande wake, Tereza pia anatibiwa vidonda vilivyotokana na saratani ambavyo vinamsababishia maumivu makali.

“Ukija usiku wote hapa wodini utatukuta tunalia kutokana na maumivu ambayo kweli hayasimuliki, moto si moto, sindano si sindano,” anasema Tereza huku akigusagusa uvimbe mkubwa katka shavu lake.

Tereza anasema matibabu ya mionzi anayopatiwa yanampa nafuu ingawa nayo yanasababisha apate kichefuchefu na nywele kunyonyoka.

“Wakati mwingine naharisha damu na vidonda vinanisababishia maumivu na maji hunika sehemu za siri,”anasimulia.

Martha kwa upande wake anasema kutokana na kuwa mlemavu wa ngozi alinyanyaswa sana na mama yake wa kambo.

“Mama yangu alifariki nikiwa na miaka minne, nikabaki na baba, baada ya baba kuoa mwanamke mwingine ndipo matusi na vipigo vilipoanza,” anasema Martha na kuongeza: “Mama alikuwa ananitukana na kunidhalilisha kuwa nafanana na nguruwe”.

Wote wametekelezwa
Agnita, Thereza na Martha baada ya kupatwa na maradhi kwa nyakati tofauti wote wametelekezwa na wanaume waliozaa nao.

Agnita mbali na mwanaye Baraka, kijijini ameacha watoto wawili, ambao wanalelewa na mama yake (bibi yao) na kwamba hawana msaada kutokana na mume wake kumkimbia mara tu alipoanza kuumwa.

“Nimezaa naye watoto wote watatu, lakini baada ya kuniona nimepatwa na matatizo amenikimbia,” anasema Agnita.

Agnita ambaye baba yake alifariki  miaka mingi iliyopita, anasema hata kama mumewe atajitokeza leo, hawezi kumsamehe kutokana na kumtelekeza akiwa mgonjwa na watoto wote.

Kilio cha kutelekezwa pia kinasikika kutoka kwa Tereza ambaye anasema mume wake, Marko Kalolo alimkimbia mara tu baada ya yeye kuanza kuugua kila mara.

“Sina hamu na wanaume, sikujua kama ni wakatili kiasi hiki. Hivi kweli mimi na hali hii Marko ananikimbia? Nilidhani angenivumilia hadi nitakapopona?” anasema huku akitokwa na machozi.

“Wakati mwingine nawaza mengi, nawaza maumivu na ninawaza kama nikifa leo kwa maradhi haya ya kansa (saratani) watoto wangu wawili watalelewa na nani,” anahoji Tereza.
 
Anasema pamoja na matatizo mengine, mtoto wake mwenye umri wa miaka 12 ni bubu, hivyo anawaza sana juu ya hilo kwani anahisi mtoto huyo atateseka zaidi.
 
Kwa upande wake Martha anasema baada ya mateso yake mama wa kambo kuzidi, aliona bora apate mtu wa kuishi naye.

“Nikaolewa na mume ambaye ni ki umri ni sawa na babu yangu, nimezaa naye mtoto mmoja, lakini huyu pia hakunifaa,” anasema Martha.

Anasema mwanaume huyo, hakumsaidia kwani ni mlevi na kwamba alikuwa akimtukana matusi na baadaye alimtelekeza.

“Akirudi kwenye pombe alikuwa akinitukana kwa kuniambia amechoka kukaa na mimi kama sina pa kwenda niende serikalini,” anasema Martha na kuongeza:

“Maradhi ni mtihani unaoweza kumkuta yeyote … wakati wowote. Hakuna haja ya kutunyanyasa kutokana na ulemavu watu, tunaomba tusaidiwe.”

Anasema alibahatika kupata mwanamume mwingine ambaye alizaa naye watoto watatu na kwamba bahati mbaya alifariki na kumwachia mzigo wa watoto hao.
“Alipofariki ilimbidi nirudi nyumbani ambako nililakiwa na sura ya mama yangu wa kambo iliyonuna”, alisema.


Kauli ya daktari
Daktari  bingwa wa uchunguzi wa maradhi mbalimbali katika Kitengo cha Patholojia cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Innocent Mosha anasema, walemavu wa ngozi  hawana tabaka la ngozi linaloitwa melanin na kwamba ndicho chanzo cha kupata maradhi ya saratani.

Anasema melanin ndizo zinazosaidia  kupambana na mionzi ya jua ambayo mara nyingi husababisha saratani ya ngozi.

Dk Mosha alibainsha kuwa, aghalabu  albino hupata saratani maeneo ya kichwani, mikononi au sehemu za miili yao ambazo hupigwa na jua kutokana na kuwa wazi.

Kuhusu tiba Dk Mosha anasema: “Albino wanaweza kupona saratani ya aina hii kwa kuanza tiba mapema, hasa tiba ya upasuaji na mionzi.”
Anasema pia albino wanaweza kukingwa dhidi ya athari za jua ikiwa Serikali na/au taasisi za kijamii zitawapa vifaa vya kuzuia jua vikiwamo kofia za pama na miamvuli.


Chanzo:Mwananchi

No comments: