ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 27, 2012

Senegal yafungwa tena, yatolewa Afcon

KIKOSI cha Equatorial Guinea kilicheza vizuri juzi na kuifunga Senegal, ‘Simba wa milima ya Teranga’ mabao 2-1 na kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Afcon inayoendelea mjini hapa. 

Senegal kwa kichapo hicho, imefungasha virago, kwani katika mechi mbili ilizocheza imeambulia mabao mawili na kuondoka bila pointi yoyote. 


Bao la David Alvarez la dakika za nyongeza ya 94, ndilo lililowapeleka wenyeji hao hatua ya robo fainali, baada ya kuanza kufunga na Senegal kusawazisha. 

Senegal ambayo iliingia kwenye michuano hiyo ikiwa moja ya timu inayopewa nafasi kubwa kulitwaa kombe hilo, ilianza michuano hiyo kwa kuchapwa mabao 2-1 na Zambia katika mchezo wa kwanza wa kundi A. 

Kocha wa Senegal, Amara Traore amesema kwamba timu yake haikuwa na bahati wakati ilipofungwa na mmoja wa waandaji wa michuano hiyo, Equatorial Guinea. 

Kufungwa huko kwa mabao 2-1, kunamaanisha kwamba Simba hao wa Teranga, wanakuwa timu ya kwanza kuondolewa kwenye michuano hiyo, kama ilivyokuwa mwaka 2008. 

“Tulijiandaa kwa kila hali na kwenye mchezo ule tulipata nafasi nyingi za kufunga. 

“Lakini hatukuwa na bahati. Nina furaha kubwa na wachezaji wangu, kwani walicheza kwa kujituma na bidii zote,” alisema Kocha Traore. 

Senegal sasa itacheza mchezo wake wa mwisho dhidi ya Libya, na hata kama watashinda haitawasaidia lolote. 

“Kwa uhakika kabisa nimekatishwa mno tamaa na matokeo haya kwenye michuano ya Afcon. 

“Na hii itawapa shida zaidi wachezaji wale ambao wanacheza michuano hii kwa mara ya kwanza. Lakini nawapongeza wachezaji wangu walicheza kwa kujituma mno, lakini bahati haikuwa upande wetu,” alisema Traore. 

Katika mchezo mwingine usiku huo wa juzi, Zambia ilitoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Libya, mechi ambayo ilichezwa kwenye uwanja uliojaa maji. 

Mchezo huo wa Zambia na Libya ulichelewa kuanza baada ya mvua kubwa iliyonyesha mapema kusababisha uwanja kujaa maji. 

Hata hivyo, Zambia ililazimika kusawazisha mara mbili baada ya kutanguliwa kufungwa katika kila kipindi. 

Ahmed Osman alianza kuifungia Libya katika dakika ya tano, kabla ya Emmanuel Mayuka kusawazisha dakika ya 29. 

Ahmed tena akaifungia Libya bao la pili na nahodha wa Zambia, Christopher Katongo kusawazisha kwa kichwa dakika ya 54. 

Mechi za mwisho za kundi hili zitacheza Jumapili, wakati Equatorial Guinea itakapovaana na Zambia, huku Libya ikicheza na Senegal. 

Iwapo Equatorial Guinea itatoka sare ya aina yoyote, itapanda kileleni kwa kundi na Zambia itaweza kushika nafasi ya pili. Lakini kama Libya itaifunga Senegal na Equatorial Guinea ikaishinda Zambia, itakuwa imefuzu hatua ya robo fainali.


Habari Leo

No comments: