
Mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu akimtoka kipa wa Miembeni, Abass Nassor Ali na kufunga bao kwa kichwa wakati wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayondelea kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Picha na Jackson Odoyo
USHINDI wa Simba umezua mpya kwenye Kombe la Mapinduzi baada ya kocha wa Miembeni United, Salum Bausi kujiuzulu nafasi yake kwa kile anachodai viongozi wake kupanga matokeo.
Uamuzi wa kocha huyo ulikuja muda mfupi baada ya timu yake kukubali kichapo cha mabao 4-3 kutoka Simba katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea Kisiwani Zanzibar.
Akizungumza na Mwananchi, kocha huyo alisema haoni sababu ya kuendelea kuifundisha timu hiyo katika mashindano hayo ambayo yanaendeshwa kimaslahi ya watu wachache.
“Mimi ni kocha mwenye kiwango na naheshimu kazi yangu siwezi kufurahishwa na matokeo haya kwa sababu kuna watu walishapanga matokeo yao kabla ya timu kuingia uwanjani,” alisema Bausi
Bausi alisema hawakuwa na sababu ya kufungwa na Simba kwani walicheza vizuri na kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo licha ya kutokuwa na wachezaji wenye majina makubwa kama wapinzani wao.
“Siwezi kusema nani aliyehusika kupanga matokeo haya, lakini mambo yamefanyika kwa uwazi na kila shabiki aliyekuwa uwanjani aliona kilichoendelea. Nimeamua kujiuzulu na tayari nimetoa taarifa kwa uongozi wa timu hata mazoezi ya leo (jana) sikwenda," alisema
"Nimeamua kujiuzulu ili kulinda heshima yangu, familia yangu pamoja na talaamu yangu, lakini pia kwa lengo la kuinusuru soka la Zanzibar na Tanzania nzima.”
Hata hivyo, kauli ya kocha huyo iliungwa mkono na baadhi ya mashabiki waliokuwa uwanjani hapo huku wengine wakidai kuwa mmiliki wa timu hiyo Amani Makungu ndiye aliyehusika katika kupanga matokeo.
Mashabiki walisema muda mfupi baada ya mmiliki huyo kwenda katika bechi la ufundi ghafla wachezaji wote wakainamisha vichwa vyao na baada ya hapo wakaanza kucheza chini ya kiwango ndani ya dakika tano kabla ya Simba kupata bao na kufanya matokeo kuwa 4-3.
“Bwana hapa kila kitu kimefanyika kwa uwazi mkubwa, wote tumeona kilichotokea, baada ya Simba kuzidiwa katika matokeo ya 3-3 mmiliki wa wa Miembeni United, Makungu alishuka na kwenda kuongea na benchi la ufundi na baada ya hapo Simba wakapata bao la 4-3 katika dakika ya 47” alisema Salum Mbarouk.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo mmiliki wa Miembeni, Makungu kabla ya kujibu alicheka na kusema hayo ni maneno ya mashabiki na kwamba hakuna kitu kama hicho na anaamani Simba imeshinda kihalali.
“Mimi ni mmiliki wa timu hii, nina haki ya kwenda kwenye benchi la ufundi na kuzungumza nao na nilichokwenda kuzungumza ni kuwaongeza wachezaji wangu hamasa ili washinde,”alisema Makungu.
Kwa upande wake kocha wa Simba, Milovan Cikovic alisema amefurahishwa na matokeo hayo, lakini hakufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake.
"Kuna kazi kubwa ya kuitengeneza upya timu ili kufikia kiwango ninachokitaka si uchezaji wa aina hii," alisema Milovan.
Alipoulizwa juu ya madai kwamba matokeo yalipangwa ili timu yake ishinde kwa lengo la waandaaji wa michuano hiyo kupata mapato alijibu: “Mimi sifahamu lolote kuhusu hilo, pili sifahamu mazingira soka la Tanzania bali ninachofahamu ni kwamba vijana wangu wamejituma na kupata ushindi.”
Wakati huohuo, timu ya Mafunzo imetinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea mjini hapa baada ya kuifunga Kikwajuni bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kwa matokeo hayo, Mafunzo sasa itasubiri mshindi kati ya Yanga na Azam waliokuwa wakicheza baadaye jana usiku kwenye Uwanja wa Aman.
Shujaa wa mechi hiyo alikuwa Sadik Habibu aliyefunga bao pekee la ushindi katika dakika ya 59 akimaliza mpira wa krosi iliyochongwa na Jako Joma.
Kabla ya kufunga bao hilo, Habibu nusura afunge bao katika dakika ya 26 kama shuti lake lisingekwenda nje kidogo ya lango.
Kwa jumla, Mafunzo ndio waliotawala mchezo kwa kiasi kikubwa na kustahili ushindi huo wa taabu.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment