ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 25, 2012

Siri 20 usizozijua za kufurahia mapenzi


NI Jumatano nyingine tena imewadia marafiki zangu ambapo tunakutana katika uwanja wetu ule ule wa kupeana darasa hili maridhawa. Ninaamini mtakuwa wazima wa siha njema na mpo tayari kupokea kile nilichowaandalia kwa wiki hii. Karibuni. 
Ndugu zangu, kuna mambo mengi sana yanazunguka, ambayo yanatakiwa kufanywa ili mtu aweze kufurahia mapenzi na mwenzake. Wakati mwingine kuna vitu ambavyo tunavikosea bila kufahamu, matokeo yake vinaleta matatizo kwenye ndoa hapo baadaye.
Leo nataka kukupa siri muhimu ishirini ambazo kwa hakika kama ukizizingatia, kwako mapenzi yatakuwa burudani ya aina yake. Huwezi kulia asilani katika maisha yako kwa sababu utakuwa umeshajua cha kufanya.
Ukweli ni kwamba, baadhi ya matatizo ambayo yanakuwepo kwenye ndoa, husababishwa na mwanzo mbaya wa wahusika, wakati walipokutana na kuamua kuanzisha uhusiano.


Wengi hawafikirii kuhusu hili, lakini ndiyo ukweli wenyewe. Hata kama upo kwenye ndoa, usiwe na shaka, mada hii ni kwa ajili yako, kwani zipo siri ambazo unaweza kuzitumia hata ukiwa tayari upo kwenye ndoa yako.
Hapa katika All About Love, kinachofanyika ni kukupa siri kuanzia mwanzo wa uhusiano ambao inatambulika kama urafiki, uchumba na baadaye ndoa. Kwa maneno mengine, kila aliye kwenye uhusiano, mada hii inamhusu.
Ikiwa upo ndani ya ndoa na mwanandoa mwenzako anaonekana hashibi chakula cha usiku au anavimbiwa, ndani ya siri hizi ishirini utapata tiba. Mathalani mwenzako hakuridhishi mnapokuwa faragha, mada hii ni kwa ajili yako. Yapo mengi ya kujifunza, wapo ambao wanatoa harufu mbaya sehemu za siri, wana maumbile madogo au wanashindwa kufanya kazi inavyotakiwa na hivyo kudharauliwa, nao nitazungumza nao.

Niseme tu, ni siri ishirini ambazo zipo sirini, lakini hapa tutazungumza kwa lugha ya kirafiki zaidi bila kuchafua hali ya hewa na mambo yataenda sawasawa. Haya sasa marafiki, twende tukaanze kuhesabu siri moja baada ya nyingine. Kama nilivyosema awali, kwamba nitaanza mwanzoni kabisa mwa uhusiano (urafiki), uchumba na baadaye ndani ya ndoa, ambapo huko ndipo kwenye kasheshe zaidi, maana hakuna ‘option’ zaidi ya kukabiliana na tatizo.
Wengi tunafahamu kwamba, walio kwenye urafiki hata uchumba, wanaweza kuamua lolote kama wataona wenzi wao wana matatizo fulani. Ni rahisi kubadilisha uamuzi hata kama watakuwa wamefikia katika hatua ya mwisho kabisa.
All About Love haitarajii uingie kwenye matatizo hayo; lengo lake ni kukuandalia ndoa imara, bora itakayokuwa faraja ya maisha yako na siyo kilio. Anza kutiririka na siri hizo...  

1. FANYA UCHAGUZI SAHIHI
Hapa ndipo watu wanapotakiwa kutumia akili zao mpaka zile za akiba, ukikosea hapa ni rahisi sana kuvurunda hapo baadaye. Uhusiano wenye nguvu, hujengwa na penzi la kweli. Acha kukurupuka, lazima ujihakikishie kwamba uliyenaye ni chaguo kutoka ndani ya moyo wako.
Najua una maswali; kwamba utawezaje kumjua mwenye mapenzi ya kweli, hiyo ni mada ambayo nimeshaandika mara kadhaa katika ukurasa huu na gazeti damu na hili, Ijumaa. Kimsingi, kwa kufuata maelekezo hayo, mwenzi ambaye unatarajia kuwa naye katika maisha ya ndoa hapo baadaye, lazima msingi uwe ni uchaguzi sahihi.
Sikia, watu wengi waliokuwa na fedha, wamefilisika baada ya kuoa/kuoleawa na wenzi ambao si sahihi. Aidha, wapo wenye mafanikio makubwa sana, ambayo wameyapata baada ya kuoa/kuolewa na wenzi sahihi. Rafiki zangu, si jambo rahisi kumpata yule aliye sahihi. Inahitaji utulivu.
Yapo mengi sana ambayo unapaswa kuyaangalia, ambayo nimekwishaeleza sana katika makala zangu zilizopita. Wakati nahitimisha kipengele hiki, shika neno moja tu; unapomchagua mwenzi wa maisha yako, hakikisha ni yule aliye sahihi! Tuendelee na kipengele kingine. 

2.  JIELEZE
Migogoro mingi baina ya walio kwenye uhusiano husababishwa na wenzi kutowafahamu vyema wenzao. Usiingie katika mkumbo huu, ni suala la kujieleza tu. Kumweleza mpenzi wako ulivyo, kutamfanya ajue vitu unavyopenda na usivyopenda. Aidha, kama unao udhaifu wowote wa kiafya na kadhalika, mweleze mwenzako.
Kumweleza kutamfanya ajiamini kuwa anapendwa. Kunaonesha unavyojiamini na unayetaka mwenzako ashirikiane na wewe katika hali uliyonayo. Si vibaya mwenzio kukufahamu kwamba una hasira sana. Yes! Maana akishajua hilo, ataacha utani unaokaribia kukuudhi maana anajua vizuri kuwa una hasira za karibu.
Ipo mifano mingi sana, lakini kikubwa cha kushika katika kipengele hiki ni kuwa mkweli kwa mwenzako kuhusu maisha yako. Acha kumdanganya kwamba familia yenu ina uwezo mkubwa, wakati ni wa kawaida. Kuwa mkweli, mapenzi si utajiri, ni hazina iliyojificha ndani ya moyo.
Kama anakupenda, anakupenda tu! Siku akigundua kwamba unamdanganya, pendo lake litapungua kwa kiasi kikubwa sana. Jieleze kwa uwazi na ukweli kutoka ndani ya moyo wako. Naye atakuheshimu na utakuwa umetengeneza mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye ndoa isiyo na migogoro.
Rafiki zangu, nilisema zipo siri ishirini, tumeshaona mbili, wiki ijayo tutaendelea na siri nyingine. Ni mada ndefu kidogo, lakini yenye elimu pana, itakayobadilisha kabisa mtazamo wako katika mapenzi. Tafadhali usikose!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.

No comments: