Asema wanaopanga sasa kuingia Ikulu 2015 ni walafi
Hakuna anayesumbuliwa na shida za kweli za wananchi
Hakuna anayesumbuliwa na shida za kweli za wananchi
Sitta alisema watu hao hawana nia ya dhati ya kutaka kuingia Ikulu ili kutatua matatizo yaliyopo katika jamii na kwamba wananchi wanalijua hilo; jambo linalowafanya wawe na wakati mgumu katika kufanikisha mipango yao.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufungua semina kuhusu masuala ya matumizi ya mimea kwa ajili ya kuzalisha mafuta (bio-energy) na usalama wa chakula kwa nchi za Afrika Mashariki.
Baada ya kufungua semina hiyo, Sitta alijibu maswali mbalimbali ya waandishi waliotaka kupata maoni yake juu ya malumbano ambayo yamekuwa yakiendelea nchini kuhusu mtu wa kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Kada huyo mashuhuri wa CCM ambaye pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Tisa alilolibatiza la kasi na viwango, alisema watu wanaotajwa kutaka nafasi ya urais pengine hawajui uzito wa kazi hiyo na umuhimu wake kwa mustakabali wa nchi.
Mwanasiasa huyo ambaye naye amekuwa akitajwa mara kadhaa kuwa anakitamani kiti hicho, alisema wenye ndoto ya kuwania urais wanatazama urais utampa nini baada ya kuupata na sio ataifanyia nini nchi yake na Watanzania.
Alithibitisha kuwa wananchi katika maeneo mbali hawaridhiki na wanasiasa na kwamba suala la kupata mtu wanayemuamini na kumpa urais linahitaji umakini na mtu aliye safi mbele ya macho yao.
"Siamini kama agenda ya watu hao wanaotajwa kuwania urais mwaka 2015 wana nia ya kushughulikia matatizo ya wananchi badala ya kuangalia maslahi yao binafsi baada ya kupata nafasi hiyo," alisema Sitta.
Hata hivyo, alisema sio kosa mtu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutangaza nia ya kugombea urais kwa kuwa Rais Kikwete hagombei tena nafasi hiyo.
Alisema suala la rushwa litawapa wakati mgumu wagombea wa urais mwaka 2015 kwa kuwa utaratibu huo umetawala mpaka watoto wa miaka minane wanaujua.
Baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, majina ya vigogo kadhaa ndani ya CCM yamekuwa yakitajwa kutaka kuwania urais kumrithi Rais Kikwete.
Vigogo hao ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Sitta mwenyewe.
Hata hivyo, makada hao wa CCM hawajatangaza nia yao ya kutaka kiti hicho, kutokana na kwamba muda wa kufanya hivyo haujafika, lakini kumekuwa na makundi yanayowaunga mkono.
NYALANDU NA URAIS
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu, alisema kuendelea kushamiri kwa siasa za makundi ndani ya CCM kunaliweka taifa katika hatari kutokana na kuzorotesha shughuli za maendeleo za kila siku.
Alisema hali hiyo inaliweka taifa katika wakati mgumu na hasa kipindi hiki ambacho linakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi, kijamii na kukuza demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Nyalandu alitajwa kuunga mkono kundi mojawapo la watu wanaotajwa kuwania urais, ingawa alikanusha na kusema hana mpango huo wala hamuungi mkono mtu yoyote.
“Hali ya kisiasa iliyopo sasa na hasa kwa baadhi ya viongozi kujikita katika kutafuta urais wa 2015, huku wafuasi wao wakiendeleza mapambano dhidi ya wale wasiokubali kuwa ndani ya makundi husika inasikitisha na ina lengo la kukatisha tamaa viongozi wenye nia ya kufanya kazi walizopewa kwa bidii,” alisema.
SITTA NA UGAWAJI ARDHI
Wakati huo huo, Sitta ameitahadharisha serikali na kuitaka kuacha kutoa maeneo makubwa kwa wawekezaji kwa ajili ya kupanda mimea itakayotumika kuzalisha mafuta ya magari na mitambo.
Alisema kwa kufanya hivyo kutawafanya wananchi wawe vibarua wa kudumu katika mashamba makubwa ya wawekezaji huku hatua hiyo ikiathiri upatikanaji wa chakula nchini.
Badala yake alitaka jua litumike kama nishati ya kuendeshea mitambo mbalimbali na kuongeza kwamba Watanzania wanahitaji chakula zaidi kuliko mafuta yatokanayo na mimea.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment