Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amesema mpango wa Tanzania kuuomba Umoja wa Mataifa (UN) kuiongezea maili 150 sawa na kilometa 241.5, kutoka usawa wa mwambao wa Tanzania, haukufanywa na wizara yake peke yake bali una baraka zote za Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.
Profesa Tibaijuka alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa ameshangazwa na taarifa zilizotolewa katika vyombo mbalimbali vya habari vilivyoripoti kwamba Serikali ya Tanzania imefanya makosa kuandaa, kupeleka maombi ya kutaka kuongezewa mipaka ya eneo tengefu la bahari kuu (EEZ) bila kuishirikisha Zanzibar.
“Hili suala sijaliamua mimi wala wizara yangu peke yake, lakini nashangaa taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kwamba nimefanya makosa, nisingeweza kwenda mimi bila Mkuu wa nchi kujua na kukubali. Pia tulikuwa na ujumbe kutoka Zanzibar tuliokwenda nao kwa hiyo nashangaa wanaosema hatujashirikisha Zanzibar,” alisema.
Tibaijuka alisema sheria ya Umoja wa Mataifa juu ya mikataba ya sheria ya baharini, ilianzishwa mwaka 1982 ambapo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliridhia mwaka 1985 na sheria hiyo kuanza kutumika rasmi mwaka 1994.
Baada ya kuridhiwa kwa sheria hiyo, baraza la mawaziri kwa waraka namba 38 wa 2008 liliagiza Wizara kutekeleza mambo mawili ikiwa ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa juu ya Sheria ya Bahari ya mwaka 1985, makubaliano hayo ni pamoja na kuainisha mipaka baharini na nchi jirani.
Vile vile, iendelee na mchakato wa kudai eneo la nyongeza nje ya ukanda wa kiuchuni baharini. Mchakato huo ikiwa ni pamoja na kukusanya takwimu za jiolojiana taarifa nyingine ili kuthibitisha iwapo jamhuri ya muungano wa Tanzania inastahili kudai eneo la nyongeza nje ya ukanda wa kiuchumi baharini.
Alifafanua kuwa katika kutekeleza majukumu hayo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo alipewa jukumu la kuunda kamati mbalimbali ambazo zitatekeleza mradi huo.
Alizitaja kamati hizo ni kamati ya makatibu wakuu, kamati ya ufundi na kamati ya utekelezaji.
Profesa Tibaijuka alisema Tanzania iliingia mkataba na Serikali ya Norway katika kufadhili mradi huo ambapo kulikuwa na wawakilishi kutoka Zanzibar.
Aliwataja wawakilishi hao kuwa ni Ayoub Mohamed Mahmoud, ambaye alisema alishiriki kikamilifu katika ziara ya Norway na alipewa nafasi ya kuongea kwa niaba ya SMZ na Zakia Meghji.
“Kwa hiyo madai ya Chama cha Wananchi (CUF) kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushiriki au kushirikishwa hayaendani na yaliyojiri na hayana ukweli wowote,” alisema Profesa Tibaijuka.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Hapa kunaonekana kuna hali mbili, kama profesa anapindisha ukweli au kiswahili halifahamu vizuri, anaelezea kuwa zanzibar ilikuwa na wawakilishi wake katika mchakato mzima, ukisema wawakilishi ni zaidi ya mmoja, hapo inaonekana ni muwakilishi mmoja tu aliewakilisha zanzibar, nanukuu "Aliwataja wawakilishi hao kuwa ni Ayoub Mohammed Mahmoud, ambae alishiriki kikamilifu katika ziara ya norway na alipewa nafasi ya kuongea kwa niaba ya SMZ na Zakia Meghji".
Watunga sheria wa zanzibar yaani wajumbe wa baraza la wawakilishi wamepatwa na mshituko baada ya kusikia taarifa hizi, ni wazanzibar wepi walioshirikishwa bila chombo kikuu cha kutunga sheria hakina taarifa na huo mpango mzima, na wemepiga kura ya kutokukubaliana na mpango huo, kama wazanzibari walishirikishwa kwanini wapige hura ya kupinga. inaonekana hakukuwa na ushirikiano katika suala hili.
Post a Comment