Mwanadada Mtanzania Hazala 'The Ball Juggler' Mohammed, ambaye ni maarufu kwa kupiga danadana anatarajiwa kuondoka nchini leo kwenda Equatorial Guinea ambako mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka huu yanaendelea kwa ajili ya kuonyesha kipaji chake.
Akizungumza jana
jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Hazala atakuwa Equatorial Guinea kuanzia leo hadi Februari 7 na atapata nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa kuchezea mpira kwenye viwanja mbalimbali nchini humo.Wambura alisema kuwa binti huyo ambaye hakuweza kujumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), amepata mwaliko wa kwenda huko kupitia Taasisi ya State of the Union ambayo ilikuwa ikiwasiliana na uongozi wa Chama cha Soka cha Wanawake cha Mkoa wa Dar es Salaam (TWFA).
"Hazala alipata nafasi ya kuitwa katika timu ya Twiga Stars lakini hakuweza kufaulu kubaki kwenye timu hiyo lakini ana uwezo wa kuuchezea mpira kwa aina tofauti akiwa peke yake, tunamtakia safari njema huko anakokwenda," alisema Wambura.
Hazala 'The Ball Juggler' mara kadhaa amekuwa akionyesha uwezo wake mkubwa wa kupiga danadana za kila aina wakati wa mapumziko ya mechi za ligi au za kimataifa na kuwapa furaha mashabiki wanaofika uwanjani kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita chini ya mwaliko wa mlezi wake ambaye ni Katibu Mkuu wa TWFA, Stephania Kabumba.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment