ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 3, 2012

Bunge lawaomba madaktari wasitishe mgomo


Wauguzi wa Hospitali ya Amana iliyopo katika Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, wakimshusha mgonjwa aliyekuwa amezidiwa kutoka kwenye gari la wagonjwa hospitalini hapo Alhamisi. Baadhi ya wananchi waliofika kupata matibabu wamedai kuwa huduma zimerudi kama kawaida. (Picha na Mohamed Mambo).


BUNGE limewaomba madaktari waliogoma warudi kazini. 

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema bungeni kuwa, wabunge wanawapenda sana madaktari hivyo warudi kazini. 

“…tunawapenda sana, warudi kazini, wazingatie viapo vyao” amesema Ndugai leo mchana kabla ya kuahirisha kikao cha Bunge mjini Dodoma. 

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, naye ametoa mwito kwa madaktari na wataalamu wengine wa afya wasitishe mgomo na kurudi kazini. 

“Serikali inasisitiza kuwa mgomo wa madaktari si halali kwa sababu kisheria hawapaswi kugoma” amesema Waziri Mponda. 

Dk. Mponda amewaeleza wabunge kuwa, Serikali inasikitika kwa athari zilizotokea kwa wananchi kutokana na mgogoro huo. 

“Ni vyema madaktari wakatambua juhudi zinazofanywa na Serikali za kuboresha maslahi ya watumishi wa sekta ya afya” amesema. 

Amewaeleza wabunge kuwa, huduma zimeanza kutengamaa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, lakini huduma za dharura na wodini katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) zimedorora kwa kuwa madaktari 21 hawajarudi kazini. 

“Mipango ya kupeleka madaktari kutoka jeshini inakamilishwa ili huduma za wagonjwa wa nje (OPD) zirejeshwe” amesema Mponda wakati anawasilisha bungeni kauli ya Serikali kuhusu namna Serikali ilivyoshughulikia mgomo wa madaktari. 

Amesema, madaktari walio kwenye mafunzo kwa vitendo kwenye maeneo mengi wengi bado hawajarudi kazini Muhimbili. 

Dk. Mponda amesema, huduma zinaendelea kama kawaida katika hospitali za manispaa za Dar es Salaam kwa kuwa madaktari 75 walio kwenye mafunzo kwa vitendo wamerudi kazini. 

Amelieleza Bunge kuwa, huduma zinatolewa kama kawaida katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, na pia hali ni kama hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza. 

Amesema, madaktari 81 walio kwenye mafunzo kwa vitendo kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi wamerudi kazini hivyo huduma zinaendelea kama kawaida. 

“Serikali inatoa shukurani kwa madaktari na wauguzi wote ambao walikuwa kazini wakiendelea kutoa huduma kwa wagonjwa na kwa kutambua hali hiyo, walikutana na kuwasihi madaktari wenzao waache mgomo na kurejea kazini” amesema Dk. Mponda. 

Dk. Mponda amewaeleza wabunge kuwa, madaktari wote 65 walio kwenye mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Rufaa Mbeya wamerudi kazini hivyo huduma zinaendelea kama kawaida. 

Amesema, huduma zinaendelea kama kawaida katika hospitali za rufaa za mikoa ya Dodoma, Morogoro na Tanga kwa kuwa madaktari wote walio kwenye mafunzo kwa vitendo wamerudi kazini. 

“Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu utoaji wa huduma katika hospitali zilizokumbwa na migomo ili kuchukua ili kuchukua hatua za haraka matatizo yatakapojitokeza” amesema. 

Januari 29 mwaka huu, Waziri Mkuu aliwataka madaktari waliogoma warudi kazini ifikapo Januari 30, 2012 na ambao hawakutekeleza agizo hilo wangepoteza ajira zao. 

Bunge leo limeiagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii izungumze na Serikali na madaktari ili kumaliza mgomo huo. 

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, ameitaka kamati hiyo hiyo ifanye kazi hiyo haraka na itoe taarifa kuhusu yaliyojiri kwenye mazungumzo hayo na ushauri wa Bunge kwa pande husika. 

Ndugai amesema, ushauri wa Bunge kwa pande hizo si lazima yawe maagizo, na kwamba, wabunge wanaruhusiwa kuhudhuria vikao vya kamati na pande husika, kusikiliza na kuchangia. 

Ndugai amewaeleza wabunge kuwa, baada ya kamati ya Bunge kuwasilisha taarifa kuhusu mazungumzo na pande husika, Mbunge yeyote ambaye atahitaji mjadala ataruhusiwa kuwasilisha hoja mahsusi. 

Kiongozi huyo wa Bunge ameiomba Serikali na madaktari watoe ushirikiano kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii.

No comments: