Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa (kulia) na mchumba wake, Josephine Mushumbuzi |
Peter Saramba, Arusha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha imemwagiza Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na mchumba wake, Josephine Mushumbuzi na mwanachama mwingine wa chama hichi, Aquilinne Chuwa kufika mahakamani hapo leo vinginevyo itatoa hati ya kukamatwa.
Agizo hilo la Mahakama limekuja baada ya Dk Slaa na Mushumbuzi kushindwa kufika mahakamani hapo jana kusikiliza kesi inayowakabili pia viongozi wengine waandamizi wa chama hicho, akiwamo Mwenyekiti, Freeman Mbowe.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha imemwagiza Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na mchumba wake, Josephine Mushumbuzi na mwanachama mwingine wa chama hichi, Aquilinne Chuwa kufika mahakamani hapo leo vinginevyo itatoa hati ya kukamatwa.
Agizo hilo la Mahakama limekuja baada ya Dk Slaa na Mushumbuzi kushindwa kufika mahakamani hapo jana kusikiliza kesi inayowakabili pia viongozi wengine waandamizi wa chama hicho, akiwamo Mwenyekiti, Freeman Mbowe.
Mbowe na viongozi wenzake hao wa Chadema jana walisomewa mashtaka mapya 13. Akisoma mashtaka hayo Wakili wa Serikali, Edwin Kakolaki alimwambia Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Charles Magessa kuwa ongezeko hilo limetokana na mashtaka mapya matano baada ya marekebisho ya hati ya awali iliyokuwa na mashtaka manane.
Washtakiwa wote walikuwepo mahakamani wakati hati hiyo mpya ikisomwa isipokuwa Dk Slaa, Mushumbusi na Chuwa.
Kukosekana kwa watuhumiwa hao kuliufanya upande wa mashtaka kuomba itolewe hati ya kuwakamata kwa kosa la kutofika mahakamani bila taarifa.
Hata hivyo, ombi hilo lilikataliwa na hakimu Magessa aliyeamua kutoa siku moja kwa washtakiwa hao kufika leo na iwapo hawataitikia wito huo hati hiyo itatolewa.
Uamuzi wa Hakimu Magessa ulitokana na taarifa na ombi la Wakili wa utetezi, Albert Msando aliyeitaarifu mahakama kuwa washtakiwa hao walijichanganya kuhusu tarehe ya shauri hilo wakidhani ni leo badala ya jana na kwamba muda huo walikuwa njiani wakitokea Dar es Salaam na kuomba mahakama isitoe hati ya kukamatwa, badala yake waamriwe kufika leo bila kukosa.
Akisoma hati hiyo mahakamani hapo mbele ya umati wa wasikilizaji, Wakili Kakolaki alisema washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa mawili ya kufanya fujo, mawili kutoa matamko yenye lengo la uchochezi na kushawishi kufanya kosa.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote 19 wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa la kufanya fujo kati ya Januari 3 na 5, mwaka jana wakiwa eneo na sehemu mbalimbali za Manispaa ya Arusha.
Shtaka la pili linalowakabili washtakiwa 18 la kula njama kutenda kosa na kukaidi amri halali pia linadaiwa kutendeka kati ya Januari 3 na 5, 2011 wakati katika shtaka la tatu wanadaiwa kula njama ya kufanya kusanyiko lisilo halali lililoishia kwa wote kutenda kosa la nne la kula njama za kufanya vurugu.
Dk Slaa na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo wanakabiliwa na shtaka la tano ambalo ni kula njama kutenda kosa la kutoa matamshi yenye lengo la kuleta uchochezi huku kwenye shtaka la sita linalomjumuisha Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba washtakiwa hao watatu wanadaiwa kushawishi watu kutenda kosa.
Ndesamburo peke yake anakabiliwa na shtaka la kutoa matamshi ya uchochezi ambayo anadaiwa kuwa mnamo Januari 5, mwaka jana alitamka maneno yenye nia ya kuamsha chuki dhidi ya Serikali na Rais Jakaya Kikwete akidaiwa kusema kuwa kitendo cha polisi kuwafyatulia mabomu ya machozi na risasi za moto viongozi na wafuasia wa Chadema waliokuwa wakiandamana kwa amani ni sawa na Rais kutia saini kuruhusu machafuko nchini.
Viongozi wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ambao walikuwepo mahakamani jana wakati hati mpya ikisomwa ni pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini.
Kuanzia leo hadi Machi 3, mwaka huu shauri hilo linatarajiwa kusikilizwa kwa siku 13 mfululizo na upande wa mashtaka unatarajiwa kuleta mahakamani jumla ya mashahidi 75 kuthibitisha madai yao.
Wakili Kakolaki aliieleza Mahakama kuwa katika ushahidi wao pia wanatarajia kuwasilisha mahakamani vielelezo kadhaa yakiwemo mawe, mapanga, sime na nondo vinavyodaiwa kuokotwa baada ya askari polisi kukabiliana na waandamanaji.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment