ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 15, 2012

Kiza kinene kujiuzulu kwa Waziri Mponda

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk. Hadji Mponda
Hatma ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, ambaye anashinikizwa ajiuzulu kutokana na kuboronga mambo katika kushughulikia mgomo wa madaktari, bado ni kitendawili.
Katibu Mkuu wa Ikulu, Peter Alanambula Ilomo, alisema suala la kuchukuliwa hatua za kuwajibishwa Dk. Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya, kutokana na mgomo wa madaktari, lipo juu ya uwezo wake hivyo hawezi kulitolea maelezo kama Rais Jakaya Kikwete amechukua uamuzi gani hadi sasa dhidi ya viongozi hao.
Ilomo alitoa kauli hiyo jana alipotakiwa na NIPASHE kueleza kama kuna hatua zozote zimechukuliwa za kumwajibisha Dk. Mponda kuhusiana na mgomo huo ambao ulisababisha athari kubwa kwa wagonjwa na huduma ya afya nchini kwa ujumla.

Dk. Mponda na Dk. Nkya wamekuwa wakishinikizwa na madaktari, wanaharakati, wanasiasa na wananchi kuwajibika kwa kujiuzulu au Rais Kikwete awafute kazi kutokana na mgomo wa madaktari uliodumu kwa takribani mwezi mmoja katika baadhi ya hospitali za umma nchini.
Aidha, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,wakati akizungumza na madaktari katika harakati za kuzima mgomo huo, wiki iliyopita alisema baada ya kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa, Waziri na Naibu wake anamuachia Rais Kikwete ambaye atajua cha kufanya dhidi yao.
“Mimi ni Katibu Mkuu Ikulu, lakini katika suala la Waziri wa Afya na Naibu wake, angeulizwa Katibu Mkuu Kiongozi, yeye ndiye anaweza kujua kama Mheshimiwa Rais amechukua hatua gani, kila kazi ina mipaka,” alisema Ilomo wakati akizungumza na NIPASHE jana.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, NIPASHE ilipomtafuta ili atoe ufafanuzi wa suala hilo, Katibu Muhtasi wake alijibu kuwa yupo nje ya nchi kikazi.
Jana NIPASHE ilipomtafuta Dk. Mponda ili aeleze kama yuko tayari kuwajibika kwa kujiuzulu, alisema alikuwa katika vikao na kumtaka mwandishi kumtafuta baadaye.
Pamoja na ahadi hiyo, hakupatikana kutokana na simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.
Hata hivyo, juzi NIPASHE lilipomuuliza Waziri Mponda kama baada ya kufungua mkutano wa jumuiya za nchi kumi za Afrika Mashariki na Kati juu ya mikakati ya kupunguza vifo vya akinamama na watoto jijini Dar es Salaam, alijibu kwa ufupi: “Sikuja kwa kazi hiyo, nimekuja kufungua mkutano, ningependa kusikia maswali yanayohusu mkutano.”
Wiki iliyopita, Dk. Mponda alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa hawezi kukimbilia kujiuzulu kabla ya kutathmini jambo husika kwani siyo suluhu ya kutatua tatizo.
“Kukimbilia kujiuzulu siyo suluhu sana ya tatizo, watu wanaweza kuharibu mambo kwa makusudi wakitegemea watajiuzulu na kukaa pembeni.
Unajua mtu anaweza kufikiria zaidi kujiuzulu kama atakuwa amefanya au amesababisha kitu na yeye mwenyewe nafsi yake ikathibitisha hilo,” alinukuliwa akisema. Dk. Mponda alisema wakati wa mgomo huo alikuwa akifanya jitihada zote kuhakikisha anakutana na madaktari hao ili kufikia mwafaka na kumaliza mgomo huo, lakini bahati mbaya juhudi hizo hazikufanikiwa haraka.
CHANZO: NIPASHE

No comments: