ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 15, 2012

Wazee Chadema waponda CCM kuwaondoa wastaafu


Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limeponda uamuzi uliochukuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuwaondoa wazee wakiwemo marais wastaafu waliowahi kuwa wenyeviti wa CCM kwenye ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho.
Mwishomi mwa wiki, NEC iliwaondoa viongozi wastaafu wa Taifa kwenye vikao vyake na Kamati Kuu (CC) badala yake wameundiwa Baraza la Ushauri.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema, Nyangaki Shilungushela, alisema uamuzi huo wa CCM haukufanyika kwa makini kwa kuwa umewaengua kabisa marais hao wastaafu katika nafasi ya maamuzi ndani ya chama.
“Uamuzi huu wa kuwaundia baraza la ushauri wazee mbali ya kuonekana kuwa umeiga namna Chadema inavyowatumia wazee, lakini uigaji huo bila shaka haukufanyika kwa makini kwa kuwa umewaengua kabisa katika nafasi ya maamuzi ya chama hicho wazee hao wamekitumikia chama hicho kwa muda mrefu,” alisema Shilungushela.
Alisema wakati CCM inapita katika hali ngumu ya kisiasa, ilikuwa busara kuendelea kupata mawazo ya wazee katika vikao halali, badala ya kusubiri kuwaita na kuomba ushauri, wakati ambapo mambo yanakuwa yameshakwenda mrama.
Alisema CCM wasiwadanganye wananchi kuwa kwa namna ambavyo wamefikia tamati ya kuendelea kuaminiwa na Watanzania, kuwa eti wao wanaweza kusikiliza, kuamini na kufanyia kazi ushauri wa wazee hao, tena baada ya kuwaondoa katika vikao halali vya vyama.
Alisema ndani ya Chadema, utaratibu wa kuwawezesha wazee kuunda Baraza la Ushauri, kwa nia ya kukishauri chama umeanza kutumika tangu mwaka 2006, pale baraza hilo lilipoundwa rasmi wakati wa mabadiliko ya katiba ya chama hicho.
CHANZO: NIPASHE


No comments: