Muhimbili yasimamisha huduma
Mgomo waibuka upya Temeke
Walimu wataka mshahara zaidi Wakati madaktari bingwa wakiendelea kugoma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakishinikiza madai yao yapatiwe ufumbuzi na serikali, baadhi ya wabunge wa Kamati ya Huduma za Jamii wanaosaka suluhu hiyo, walijikuta wakibubujikwa machozi baada ya juhudi za kuwataka warejee kazini kugonga ukuta.
Wabunge wanawake wa Kamati ya Huduma ya Jamii walijikuta wakitokwa machozi baada madaktari hao kuwahakikishia kuwa hawapo tayari kuendelea na kazi kutokana na kufanya kazi katika mazingira magumu.
Kamati hiyo juzi ilifanya kazi ya kukutana na makundi mbalimbali hadi usiku wa manane.
Akizungumza na NIPASHE, mmoja wa madaktari bingwa alisema walikutana na kamati juzi hiyo majira ya saa 12:00 jioni hadi saa 1:45 usiku na kuelezea jinsi mgomo ulivyoanza hadi walipofikia maamuzi hayo.
Hata hivyo, alisema kutokana na msimamo wao wa kutokuwa tayari kurudi kazini, baadhi yao wabunge hao walitokwa na machozi.
“Sijajua kilichowafanya watokwe na machonzi ila ninahisi pale tulivyowaambia tumesitisha huduma katika hospitali hiyo ndipo tulipowaona wakiwa katika hali ya majonzi huku wakisikitika wakituomba tusifanye hivyo, lakini hatukubadilisha msimamo wetu na ndipo wengine wakaanza kutokwa na machozi,” alisema mmoja wa madaktari bingwa.
MUHIMBILI YASIMAMA
Hali ya huduma Muhimbili jana iliendelea kuwa kuwa tete baada ya mgomo wa madakatri bingwa kuanza kuonyesha makali yake.
NIPASHE ilitembelea wodi ya watoto jana mchana na kushuhudia wagonjwa wakiwa katika hali mbaya kutokana na kutopatiwa huduma na madaktari tangu asubuhi na wengine kutojua nini hatma ya maisha yao.
Letisha Edward, mama mzazi anayemuuguza mtoto wake Edison Enock, aliyelazwa katika wodi ya watoto, anayesumbuliwa na uvimbe shingoni alisema: “ Tangu nifike hapa kutokea Kigoma, ni wiki ya pili sasa mtoto wangu hajapata huduma yoyote inayostahili, madaktari wanapitapita tu, na mtoto wangu anatakiwa kufanyiwa upasuaji sijui nitafanyeje.”
Abela Kakopa aliyempeleka mwanaye, Gift Shomali, anayesumbuliwa na uvimbe tumboni na tumbo kujaa maji alisema: “Nimetokea Shinyanga, mwanangu anasumbuliwa na tatizo la tumbo kujaa maji, nimemleta Muhimbili kufanyiwa upasuaji na Februari 23, mwaka huu ndio siku ya upasuaji, lakini madaktari wamegoma, yote yatakayotokea namwachia Mungu.”
Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminieli Aligaesha, alidhibitisha jana kuwepo kwa mgomo wa madaktari bingwa katika hospitali hiyo alipokutana na waandishi wa habari.
Alisema: “Februari 6, mwaka huu, kamati ya madaktari bingwa iliandika barua kwa uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, MOI na MUHAS yenye kuazimia kwamba watasitisha rasmi huduma zote za tiba zitolewazo na Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI mpaka hapo Serikali itakapotoa tamko rasmi kuhusu mwafaka katika changamoto hii.”
Aligaesha alisema kutokana na hali hiyo, wagonjwa walioko wodini wataendelea kuonwa na madaktari wakuu wa idara na madaktari wachache wa kujitolea.
Aliongeza kuwa madaktari wa JWTZ wataendelea kuona wagonjwa wa dharura kwa jinsi wanavyowasili hospitalini hapo.
TEMEKE NAKO HUDUMA ZASITISHWA
Nayo Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam hali ni mbaya baada ya huduma ya matibabu kusitishwa na wagonjwa kutakiwa wapya kurudishwa, huku wakishauriwa kutafuta huduma kwenye hospitali binafsi au zahanati zilizo jirani na hospitali hiyo.
Usitishwaji wa huduma za matibabu hospitalini hapo zimefuatia kutangazwa kufungwa kwa huduma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
NIPASHE ilishuhudia wagonjwa wakiwa wamelala kwenye mabenchi yaliyokuwa mapokezi wakisubiri kupatiwa huduma, huku madaktari na manesi wakiwa wametoweka katika vyumba vya hospitali hiyo.
Wagonjwa waliofika kuandikishwa, walijibiwa na mfanyakazi wa mapokezi kuwa wamesitisha huduma ya kupokea wagonjwa baadaya madaktari wote kugoma.
“Kaka kama unaumwa sana nenda pale hospitali binafsi, kama unatokea Mbagala nenda Hospitali ya Rangitatu hapa hatuna huduma kuna mgomo wa madaktari,” alisikika akisema kisha akaondoka kwenye chumba hicho.
Vyumba vyote vya madaktari vilionekana kuwa vitupu baada ya madaktari na manesi kutoweka.
Mmoja wa wagonjwa aliyeonekana kukata tamaa, alisema madaktari na manesi walitoweka kwenye vyumba vyao majira ya saa 6:00 mchana na kuwaeleza wasubiri zamu ya madaktari wengine watakapoingia.
“Hatujui la kufanya hapa tulipo, unaona jinsi wagonjwa walivyolala na wengine tumekaa na kukata tamaa kabisa kama tutaweza kupata matibabu,” alisema mgonjwa huyo.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Amani Malima, alisema anachojua hospitali hiyo imekumbwa na kuzorota kwa utoaji huduma na sio kusitishwa.
KCMC NAKO MGOMO
HALI ya huduma za afya katika hospitali ya Rufaa ya KCMC bado ni tete kutokana na madaktari kuendelea na mgomo na kuwaacha madaktari walioko katika mafunzo kwa vitendo na wauguzi.
Wagonjwa waliokuwa wamelazwa walisema tangu jana asubuhi hakuna daktari hata mmoja aliyewatembelea.
Mama Anayasinta aliyelazwa hospitalini hapo kwa ugonjwa wa malaria na sukari, alisema jana hakuna daktari aliyepitia wodini.
Alisema kutokana na hali hiyo, baadhi ya ndugu wa wagonjwa wenye uwezo walikuwa wakiwahamisha wagonjwa wao kutoka hospitalini hapo na kuwapeleka sehemu zingine.
Ndugu wa mmoja wa mgonjwa aliyekutwa akimhamisha kutoka hospitali hapo, alisema ameamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuona dada yake anazidi kuteseka na kuomba kumpeleka katika hospitali teule ya wilaya ya Mtakatifu Joseph iliyopo Soweto mjini Moshi.
Pia, madaktari bingwa ambao walikuwa wakiendelea kutoa huduma, jana waliamua kugoma.
WAGONJWA MBEYA WAIKIMBIA HOSPITALI
Hali ya huduma kwa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya zimezorota kutokana na madaktari wengi kuendelea na mgomo.
Jana NIPASHE ilishuhudia baadhi ya vitanda vikiwa tupu kutokana na wagonjwa kuondoka hospitali hapo na kwenda katika hospitali binafsi.
Baadhi ya wauguzi waliozungumza kwa sharti la kutotaja majina yao, walisema huduma kwa wagonjwa hospitalini hapo bado ni mbaya kwa kuwa madaktari wengi hawajarejea kazini.
Wagonjwa waliofika hospitalini hapo, walisikika wakisema kuwa kutokana na huduma za hospitali hiyo kutoridhisha ni afadhari wawaondoe wagonjwa wao na kuwapeleka katika hospitali binafsi ili wapatiwe matibabu.
Mkurugenzi wan Hospitali hiyo, Dk. Eliuter Samky, hakupatikana kutoa ufafanuzi kwa maelezo kuwa yupo Dar es Salaam kikazi.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Humphrey Kiwelu alisema kuwa huduma hospitalini hapo bado sio nzuri kutokana na madaktari wachache kuripoti kazini.
WAGONJWA WAFURIKA MIKOCHENI
NIPASHE ilitembelea Hospitali ya Misheni Mikocheni na kushuhudia idadi kubwa ya wagonjwa waliohamia katika hospitali hiyo kutoka katika hospitali za umma.
Wingi wa wagonjwa hao umefanya uongozi wa hospitali hiyo kulazimika kubadilisha eneo lililokuwa likitumika awali kwa huduma za mapokezi kutokana na ufinyu.
Hivi sasa wagonjwa wapya wanahudumiwa katika eneo la uani ambalo awali lilikuwa limetengwa kwa ajili ya kuwahifadhi wagonjwa wanaosubiri kuitwa kwa ajili ya kuonana na daktari.
Mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, aliliambia NIPASHE kuwa ongezeko la wagonjwa limekuwapo tangu mgomo wa madaktari ushike kasi katika hospitali za umma.
Katika Hospitali za Aga Khan na TMJ, idadi ya wagonjwa ilishuhudiwa ikiwa ni ya wastani tofauti na hali ilivyo katika Hospitali ya Misheni Mikocheni.
SPIKA AZIMA MJADALA
Spika wa Bunge, Anne Makinda, jana alizuia mjadala kuhusu mgomo wa madaktari kufanyika bungeni.
Suala hilo liliibuka tena bungeni jana, baada ya Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, kuomba mwongozo wa Spika kwa mujibu wa kanuni ya 47 na 48 fasihi ya pili na tatu, akiomba suala hilo lipewe nafasi ya kujadiliwa na wabunge.
Alisema amepata habari kupitia vyombo vya habari kuwa madaktari bingwa katika Hospitaali ya Taifa ya Muhimbili nao wamegoma na kwamba hali katika hospitali ni mbaya zaidi kwani wagonjwa hawapati huduma.
“Mheshiwa Spika leo (jana) kuna habari katika vyombo vya habari kuwa madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili nao wamegoma na kwamba kwa sasa hali ni mbaya zaidi kwa wagonjwa, pamoja na maelezo ya Waziri wa Afya hali bado haijabadilika, jambo hili ni la dharura hatuwezi kuendelea na mijadala mingine wakati hali ikiwa hivi, natoa hoja tujadili,” alisema na kuhoji:
“Kama kuna hela madaktari wanadai kigugumizi ni cha nini kwa serikali kuwalipa?”
Baada ya Zambi kutoa hoja hiyo, Makinda alikataa kujadiliwa na wabunge, akisema kwa sasa linashughulikiwa na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, hivyo Bunge linatakiwa lisubiri hadi kamati hiyo imalize kazi zake.
Baada ya Spika kutoa maelezo hayo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mbunge wa Kigoma wa Kaskazini, Zitto Kabwe, walisimama wakiomba mwongozo wa Spika.
Hata hivyo, Spika aliwakatiza hakuna mwongozo kwa kiti, akisisitiza kuwa jambo hilo haliwezi kujadiliwa bungeni hadi hapo kamati ya bunge itakapomaliza kazi.
ASKOFU: SERIKALI IWALIPE
Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida, Desderius Rwoma, ameiasa Serikali itizame upya madai ya madaktari waliogoma ili warejee kazini kuokoa maisha ya Watanzania, wanaopoteza maisha kwa kukosa tiba.
Askofu Rwoma alisema hayo juzi kwenye hafla ya ufunguzi wa hosteli ya watumishi na wodi ya wazazi, hospitali ya Makiungu ambayo ni hospitali teule ya Wilaya Singida.
Alisema ni muhimu kusikilizwa kwa madai yao, kwa kuwa madaktari ni wafanyakazi rafiki wa Watanzania wote, sawa na watumishi wengine nchini ambao wameona maisha yamekuwa magumu.
Askofu Rwoma alisema lengo la madaktari hao siyo kusitisha huduma ili wagonjwa waathirike, bali ni kutokana na gharama za maisha kupanda na kuwa ngumu kwa Watanzania wote.
“Madaktari ni wafanyakazi rafiki wa Watanzania ni rafiki wa wagonjwa, sawa na wafanyakazi wengine… inaonekana mapato yao hayalingani na utumishi wao, serikali itafute namna ya kuongeza mapato yaongezeke, ili walipwe wafanye kazi vizuri,” alisema.
WANAHARAKATI: SERIKALI IWAJIBIKE
Wanaharakati wa mashirika zaidi ya 15 yasiyokuwa ya serikali, wameitaka serikali kumaliza mgogoro wa madaktari, vinginevyo yote iwajibike kwa kujiuzulu kwa kuwa imeshindwa kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu.
Tamko hilo lililosomwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen-Kijo Bisimba, kwa niaba ya asasi hizo lilisema kuwa serikali ina wajibu wa kuhakikisha inatoa dawa za kutosha katika hospitali ili kuwawezesha madaktari kufanya kazi zao za kutibu wananchi.
Hata hivyo, Bisimba aliwataka madaktari kuwa tayari kukutana na serikali ili kuzungumza na kutatua mgogoro unaoendelea ili kunusuru afya za wananchi ambao wanaendelea kuteseka kwa kukosa huduma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake, (Tamwa), Ananilea Nkya, alisema serikali inafanya makusudi kutomaliza mgogoro wa madaktari kwa kuwa wao na familia zao hawatibiwa nchini.
WALIMU NAO WADAI MSHAHARA MPYA
Baraza la Taifa la Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) limetoa tamko la kuitaka Serikali kuongeza mishahara ya waalimu kwa asilimia 100 kuanzia Julai 2012, na kuirudisha posho ya kufundishia, pamoja na kuanza kulipwa posho ya mazingira magumu.
Tamko hilo lilitolewa jana na Rais CWT, Gratian Mukoba, lililosomwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Hezekiah Oluoch, ambaye alisema kuwa tamko hilo limetolewa baada ya kikao kilichofanyika mwanzoni mwa mwezi huu.
Alisema kikao hicho baada ya kupokea taarifa ya hali ya mishahara na maisha magumu kwa walimu, kiliamua kudai mambo mbalimbali yanayohusu maslahi ya walimu, ikiwemo nyongeza ya mishahara, ambapo kiliamua kuwa walimu wa ngazi ya Daraja la III A, aanze na mshahara wa Sh. 500,000, ambayo ni ongezeko la asilimia 100.
Mwalimu mwenye Stashahada alipwe Sh. 750,000 na mwenye Shahada aanze na Sh. 938,000. Baraza la Taifa, limeagiza majadiliano kuhusu nyongeza hiyo ianze mara moja na yawe yamekamilika ifikapo mwisho wa Machi 2012, ili Serikali iingize makubaliano hayo kwenye bajeti ya mwaka 2012/13.
Mukoba alisema mwalimu ndiye mfanyakazi anayefanya kazi kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na wafanyakazi wengine wa umma, hivyo kwa kuzingatia hilo, Baraza limeona ni vizuri kuwa ifikapo mwaka ujao wa fedha walimu waanze kulipwa posho ya kufundishia, ambayo ni sawa na asilimia 55 kwa walimu wa sayansi, na asilimia 50 kwa walimu wa masomo ya sanaa, jambo ambalo alisema Rais Jakaya Kikwete aliahidi kulifanyia kazi wakati wa maadhimisho ya siku ya Walimu Duniani mwaka 2010.
Baraza hilo pia limeitaka Serikali kuanza kulipa posho ya mazingira magumu kwa walimu asilimia 25 ya mshahara kwa walimu wote wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Imeandikwa na Gwamaka Alipipi, Richard Makore, Moshi Luzonzo, Muhibu Said, Samson Fridolin na Beatrice Shayo, Dar; Abdallah Bawaziri, Dodoma; Elisante John, Singida; Charles Lyimo, Moshi na Emmanuel Lengwa, Mbeya.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment