Wapo wengine 58 wakiwemo Sugu na Waziri Samia
Pia za Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba
Pia za Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba
Kadhalika, Tume hiyo imesema kuwa inafanya utafiti kabla ya kutoa mapendekezo ya kubadili sheria inayotenganisha biashara na uongozi ili kuweka nidhamu kwa viongozi wa umma.
Kamishina wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alitangaza uamuzi huo jana Jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Jaji Kaganda alisema Tume yake itaanza kutekeleza kazi hiyo kwa kufanya uhakiki wa mali za viongozi 60 wa umma. Miongoni mwa viongozi hao wa kwanza mali zao kuhakikiwa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, Samia Suluhu; Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika na Ludovick Mwananzila, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Wengine ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi; Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya; Mbunge wa Liwale (CCM), Faith Mitambo na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo.
Viongozi wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kasim Nyangarika; Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Deusdedit Lutafubirwa; Mbunge wa Lulindi (CCM), Jerome Bwanaus; Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), Patrick Kisaka; Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Allan Kijazi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Liberatus Materu.
Kaganda aliwataja viongozi wengine kuwa ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi; Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Charles Nyamrunda; Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu; Naibu Kamishina Mkuu wa TRA, Placidus Luoga na Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga.
Viongozi wengine katika kundi hilo ni Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Dani Makanga; Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Moshi Chang’a.
Jaji Kaganda alisema uhakiki huo unatarajia kuanza Februari 20, mwaka huu na kazi hiyo itajumisha nchi nzima kwa viongozi wanaohusika na sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995. Aliwataka wananchi kutoa taarifa ambazo zitasaidia kubaini mali zilizofichwa na viongozi ambao sio waaminifu.
Kuhusu uwezekano wa kubadilisha sheria ya kutenganisha uongozi wa biashara, Jaji Kaganda alisema muda utakapofika atatoa mapendekezo ya namna ya kuibadili ili kuwabana hususani viongozi wa kisiasa.
Alikiri kuwa uadilifu kwa viongozi wa umma umepungua kwa kiwango kikubwa na kwamba kuna haja ya kutunga sheria ambayo itasaidia kurudisha nidhamu.
Alisema tofauti ya watu wasiokuwanacho na walionacho inazidi kuwa kubwa huku akitoa hahadhari kwa viongozi kuacha kuwanyanyasa wananchi wao ambao wamewaweka madarakani.
“Enzi za Waziri Mkuu, Marehemu Edward Sokoine, kulikuwa na Sheria ya Uhujumu Uchumi ambayo iliogopwa na wengi na sasa tunahitaji sheria ambayo itasaidia kutenganisha siasa na biashara,” alisema.
Aliongeza kuwa mwaka jana Baraza la Maadili la Tume hiyo lilikutana na kuwahoji viongozi wengi wa umma ambao walijaza vibaya fomu za tamko la mali na madeni na kwamba mwitikio wa kuwasilisha tamko kwa tume umeongezeka.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza katika uhai wa Tume hiyo kutangaza hadharani kwamba inakwenda kuhakiki mali za viongozi ambazo zimewasilishwa katika ofisi hiyo.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Mmm! Sasa Mnyika na Sitta wanamali gani zakutisha kulinganisha na mafisadi fulani fulani. Kweli siasa mchezo mchafuuu! Hii double standard hii ata Mungu hapendi malipo ni hapa hapa duniani.
Post a Comment