ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 13, 2012

Mamia wakwama kushiriki uchaguzi mdogo Zanzibar

Mamia ya wananchi wamekosa haki ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi mdogo wa jimbo la Uzini mkoa wa Kusini Unguja kutokana na majina yao kutokuwa kwenye daftari la wapiga kura.
Kazi ya kuorodhesha majina kwenye daftari hilo inasimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili katika jimbo hilo ulibaini kuwa waathirika zaidi katika kadhia hiyo ni vijana waliofikisha umri wa miaka 18 hivyo kufuzu sharti la kisheria ili kupiga kura kwa mara ya kwanza.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Msimamizi wa Uchaguzi wa ZEC, wilaya ya Kati Zanzibar, Mussa Ali, alisema zoezi la kuandikisha wapiga kura lilikuwa lifanyike Oktoba mwaka jana lakini haikuwa hivyo.
Alisema ZEC iliamua kutumia daftari la lililotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hivyo watu ambao hawakundikishwa katika daftari hilo watakuwa hawana sifa za kushiriki.
Hata hivyo alisema kwa mujibu wa takwimu za wapiga kura katika jimbo hilo za mwaka 2010, jumla ya wananchi 8,743 wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi huo.
Alisema kwamba idadi hiyo ya wapiga kura pia inatarajiwa kupungua kutokana na watu wengine kufariki na wengine kuhamisha makazi yao.
Hata hivyo alisema zipo sababu mbalimbali zilizopelekea zoezi la uandikishaji wapiga kura waliofikisha umri wa miaka 18 kutofanyika Oktoba mwaka jana ikiwemo ukata wa fedha na msiba wa ajali ya kuzama kwa meli iliyotokea Septemba 10 mwaka jana.
Kimsingi alisema matayarisho yote ya uchaguzi mdogo yamekamilika na vifaa vilitarajiwa kuanza kusabazwa katika vituo 31 vya wapiga kura kuazia saa 1:0 usiku Jana.
Vituo hivyo vitafunguliwa leo kuanzia saa mnoja na kufugwa saa 10: jioni kabla ya kuanza kuhesabu na kutangaza matokeo.
Wagombea katika uchaguzi huo ni Ali Mbarouk Mashimba, (CHADEMA) Mohamed Raza Daramsi (CCM) Yussuf Rashid Mshenga,( AFP) Khamis Khatibu Vuai, (TADEA) na Salma Hussen Zarali (CUF) .
Viongozi wa kitaifa wa Vyama vilivyosimamisha wagombea jana walifunga mikutano ya kampeni katika viwanja tofauti katika jimbo hilio la Uzini.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mwakilishi jimbo hilo Marehemu Mussa Khamis Silima aliyekufa kwa ajali ya gali huko dodoma Oktioba 22 mwaka jana.

Uzini ni ya CCM, Chadema ya pili

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka kidedea katika uchaguzi mdogo wa uwakilishi Jimbo la Uzini, Mkoa wa Kusini Zanzibar baada ya mgombea wake kuibuka na ushindi wa asilimia 91.1 na kuwabwaga wagombea wa vyama vingine.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Kati Zanzibar, Mussa Ali, akitangaza matokeo hayo jana, alisema mgombea wa CCM, Mohamed Raza, ameshinda baada ya kupata kura 5,377 sawa na asilimia 91.1 ya kura 5,903 zilizopigwa.
Alisema mgombea wa Chama Cha Deomokrasia na Maendeleo (Chadema), Ally Mbarouk Mshimba, ameshika nafasi ya pili baada ya kupata kura 281 sawa na asilimia 4.8 akifuatiwa na mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Salima Hussein Lazaro aliyepata kura 223 sawa na asilimia 3.8.
Ali alisema mgombea wa Tadea, Khatib Vuai, amepata kura 14 sawa na asilimia 0.2 akifuatiwa na Rashid Yusuph Mchenga wa AFP aliyepata kura nane sawa na asilimia 0.1
WACHACHE WAJITOKEZA
Uchaguzi huo ulifanyika jana huku mahudhurio ya watu waliyojitokeza kupiga kura yakionekana madogo kutokana na sababu mbalimbali.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo, marehemu Mussa Khamis Silima, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari mkoani Dodoma Oktoba, mwaka jana.
Vituo 31 vya wapiga kura vilianza kufunguliwa saa 1:00 asubuhi, lakini hadi mchana baadhi ya vituo wapiga kura walikuwa wachache. Wanawake walionekana kuwa wengi huku baadhi yao wakiwa wamebeba watoto.
Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Kati Zanzibar, Mussa Ali, alisema pamoja na kujitokeza kwa wapigakura wachache, bado walikuwa na matumaini ya asilimia 50 ya watu walioandikishwa wangejitokeza kupiga kura.
Alisema hadi mchana hapakuwepo na malalamiko yoyote yaliyopokelewa katika ofisi yake na zoezi la upigaji kura lilikuwa linaendelea katika mazingira ya utulivu.
Mussa alisema jimbo hilo lina jumla ya wapiga kura 8,743 waliotarajiwa kujitokeza kwa mujibu wa Daftari la Kudumu la wapiga Kura la mwaka 2010.
Hata hivyo, alisema vijana waliofikisha umri wa miaka 18 katika jimbo hilo walikwama kupigakura kutokana na kutoandikishwa katika daftari.
Alisema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilitarajia kuandikisha wapiga kura wapya Oktoba, mwaka jana, lakini zoezi hilo halikufanyika kutokana na ukosefu wa fedha na msiba uliotokana na ajali ya meli ya MV Spice Islanders iliyotokea Septemba 10, mwaka jana.
Mbali na vijana waliofikisha umri wa miaka 18, pia wananchi kadhaa waolikosa nafasi ya kuandikishwa katika daftari hilo mwaka 2010 kutokana na sababu mbalimbali, pia jana walikwama kupigakura.
Katika vituo vya Uzini na Mtakarani, walionekana watu wachache waliojitokeza kupiga kura huku wananchi wengi wakionekana kuendelea na shughuli za kujitafutia mahitaji yao.
“Haiwezekani uende katika kituo cha kupiga kura wakati nyumbani hujui watoto watakula nini, hali ya maisha ni ngumu,” alisema Shabani Mtumwa, mkazi wa Gamba.
Aidha, wagombea watatu walishindwa kujipigia kura kutokana na kutokuwa wakazi wa jimbo hilo, akiwemo mgombea wa CCM, Mohammed Raza Daramsi, wakati mgombea wa Chadema, Ali Mbarouk Mshimba, alipiga kura katika Shehia ya Tunduni.
CHANZO: NIPASHE

No comments: