ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 6, 2012

Mukama aanika siri ya CCM kujivua gamba

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Wilson Mukama
ASEMA  UINGEREZA KUKIWA NA JAMBO LINALOSUMBUA WANAUNDA TUME ILI KUSAHULISHA WATU
Elias Msuya
KATIBU Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, amesema chama hicho hakitafukuza wanachama wake katika mpango wake  wa kujivua gamba.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema NCCR-Mageuzi na CUF vililaumiwa na jamii baada ya kuamua kuwavua uanachama wabunge wake.
 “Hata Waingereza wanatabia moja. Wakiona jambo linawasumbua, wanaunda Royal Commission, jambo hilo litachunguzwa kwa muda mrefu. Wakimaliza, watu wameshasahau,”  alisema.
Mukama alisema dhana ya kujivua gamba inahusu mageuzi ya kiuchumi na kimaadili na si kuwafukuza pacha watatu.


Alisema CCM haina mpango wa kuwafukuza makada wakiwamo wale walioelezwa kwamba wanapaswa kujivua gamba.

“Kufukuzana siyo dawa, si unaona jinsi jamii ilivyowageuka NCCR Mageuzi kwa kumfukuza David Kafulila au kufukuzwa kwa Hamad wa CUF. Sisi tumesema, kufukuzana siyo suluhisho.., utakuwa unashughulikia tu dalili wakati ugonjwa wenyewe haujaufikia,”alisisitiza Katibu Mkuu wa CCM.

Alisema kinachoendelea ndani ya CCM ni tofauti za kimawazo, jambo ambalo si baya.

“Kutofautiana ndani ya chama siyo vibaya. Hao wanaokwambia fukuza hawa,  ndiyo hao hao watakaukushambulia ukishawafukuza,” alisema.

Kuhusu majina ya makada wa CCM waliokuwa wakitajwa kuhusika na ufisadi, Mukama alisema hayakuwemo kwenye taarifa za vikao vya chama na kwa msingi huo si sahihi kuyajadili.

“Mimi mwenyewe kwenye ‘press conference’ (mkutano na waandishi wa habari) pale Dodoma mwaka jana, niliwauliza  waandishi wa habari, mbona sioni majina ya hao watu wanaotajwa kwenye minutes (agenda) za vikao? Maana kama yangekuwa kwenye vikao, basi tungeyatekeleza," alisema na kuongeza:

Alisema  chama hicho kinalenga katika kujitegemea kifedha kwa kutumia miradi yake na wanachama wake na kutaja  Mikoa ya Dar es Salaam Arusha na Mwanza kuwa  imeshapangwa katika mpango wa kujitegemea kifedha, hasa katika kuwalipa watendaji ndani ya chama.
“Vilevile tumezungumzia jinsi ya kuwapata wajumbe wa NEC. Badala ya kuwapata kwenye ngazi ya mkoa, sasa tumesema wajumbe hao watapatikana kuanzia ngazi ya wilaya ambako wananchi wanawajua. Hili ni la muhimu na la haraka,” alisema.

Alisema sekretarieti iliyopita iliyokuwa chini ya Yusuf Makamba ilikuwa imekifikisha chama mahali pabaya.

“Wakati ule tunaingia katika sekretarieti, chama chetu kilikuwa na udhaifu mkubwa. Hatukuwa na mvuto, ndiyo maana chama kilipoteza majimbo muhimu kama vile Ubungo hapa Dar es Salaam na majimbo mawili kule Mwanza,” alisema na kuongeza.

“Ndiyo maana Rais Kikwete alisema inabidi chama kijipime na kujilinganisha na kule kilipotoka kwenye TANU na ASP. Je, bado chama kinasimamia mambo yaleyale ya umoja, mshikamano na uadilifu,” alisisitiza.
Hata hivyo, jana mwenyekiti wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete alisisitiza ulazima wa utekelezaji wa mpango huo kwa watu wasiokuwa na maadili katika kilele cha maadhimisho ya miaka 35 ya chama hicho tawala.

Wanaotaka urais
Mukama alisema ni ruksa kwa wanaotaka urais kufanya hivyo lakini chama hakitambui kampenzi zao.

Hata hivyo, msimamo huo pia unapingana na wa  Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho, Philip Mangula,Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Mjumbe wa Halmashauri wa CCM, Abdulharam Kinana.
Mukama kwa upande wake, alisema  CCM haiwezi kuwazuia watu kunuia kuwania urais lakini, yenyewe haitambui kampeni zao zinazoendeshwa kwa njia mbalimbali.

 “Hili la watu kujitokeza kuwania urais lipo na wala siyo vibaya.  Hata Julius Caesar wa Roma aliwahi kusema ‘kuwa na ambition (nia) si vibaya’. Sisi tunajua kuwa tutapata mgombea mpya na mzuri,” alisema Mukama.

Alikuwa akizungumza katika  mahojiano maalumu na gazeti hili, yaliyofanyika jijini Dares Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Msimamo wa chama ni kutojiingiza kwenye mambo hayo haraka, lakini  hakikatazi mtu binafsi kuanza kujiandaa," alisema.

Mukama alisema CCM iko makini katika kutafuta mgombea wake lakini, hakiwezi kuacha mambo mengine na kukalia kujadili wagombea urais wa mwaka 2015.

“Hatuwezi kuacha mambo yetu yote tukakalia kujadili wagombea urais wa mwaka 2015. Kwani wewe unapokwenda kuchumbia, huwa unawaambia rafiki zako,"alihoji na kuongeza:

“Ukiwaambia hao hao watakwambia unayekwenda kumchumbia ni mbaya, halafu kesho yake hao hao watamchukua.”

Kauli ya Mangula
Tofauti na Mukama, Katibu mkuu mstaafu wa CCM Philip Mangula, amesema kitendo cha mwanachama kutangaza sasa nia ya kuwania urais mwaka 2015 kwa tiketi ya CCM ni makosa makubwa.
Mangula alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumzia mwenendo wa chama hicho kwa miaka 35 tangu kilipozaliwa, katika kipindi cha Asubuhi Njema kinachorushwa na Kituo cha Star TV cha jijini Mwanza.
Alisema kuwa kitendo hicho kinamchanganya rais aliyeko madarakani kwakuwa yeye ndiye anayesimamia ilani ya uchaguzi ya CCM.
“Kujitangaza sasa kuwa unatarajia kugombea urais ni makosa makubwa. Kwa sababu chama kimejiwekea ilani kisha kikampa rais aisimamie. Lakini yule anayejitangaza anakuwa na mambo yake mwenyewe,” alisema Mangula.

Kinana
Kauli hiyo ya Mukama pia inapingana na zile zilizotolewa na Nape na Kinana kwa nyakati tofauti wakielezea athari za  kampeni hizo miaka minne kabla.
Kinana ambaye ni Mlezi wa CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam, , alikemea makada alioanza mbio za urais wa 2015 akisema wanamdhoofisha Rais Jakaya Kikwete na serikali yake.

Kauli pia iliwahi kutolewa na Nape. 
Kwa upande wake Kinana alisema vigogo walioanza kampeni za urais sasa wanavuruga utendaji wa Serikali.
Aliwaelezea vigogo hao kuwa ni wabinafsi, wanaovuruga nchi na hawana lolote wanalolifanya kwa maslahi ya chama hicho tawala.
“Sasa hivi Rais Kikwete ana miaka mingine minne mbele kabla ya kumaliza uongozi wake na CCM ina kero nyingi za kushughulikia ili kutekeleza ilani yake, halafu wengine wanazungumzia urais sasa," alishangazwa  Kinana.

Alizitaja kero hizo kuwa ni pamoja na elimu, afya, maji, barabara, mazingira, maisha magumu yanayosababishwa na mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani shilingi.

Kauli ya Nape

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Januari 15, mwaka huu, Nape  alisema CCM haiko tayari kuendelea kuwavumilia wanachama wanaounda makundi ndani ya chama hicho kwa lengo la kutafuta urais 2015.
Nape alisema kitendo cha kuanza kampeni hizo sasa, kitazaa makundi ambayo yatasababisha kuvunjika wa umoja na mshikamano ndani ya CCM.
Alisema wanaojiingiza kwenye mbio hizo wanatumia fedha nyingi katika kujipanga ili kufikia malengo na  akawashauri wasipoteze muda kwa maelezo kuwa siku ikifika chama hakitawapa nafasi.

Mwananchi

No comments: