KWA kuendelea na mada yetu, nianze na swali: Una wasiwasi na mahali ambako mwenzi wako yupo? Huna amani na unahisi anakusaliti. Moyo wako umefunikwa na jakamoyo na kila hatua mapigo yanaongezeka kasi au yanashuka. Kimsingi huna sababu ya kuwa hivyo. Usiishi kwa dhana, ila simamia vitu vinavyoonekana.
Mawasiliano ni njia bora kabisa ya kudhibiti wivu. Mnapozungumza mara kwa mara au ‘kuchati’ kwa SMS, Facebook au mitandao mingine ya kijamii, huwaweka karibu. Kama una hali ya wasiwasi, itakwisha au kupungua kwa sababu muda wote utajiona kama mpo pamoja.
Je, mkiwa wawili chumbani au sehemu yoyote ya faragha, bila simu wala mtu wa tatu anayeweza kuingilia ukaribu wenu, mnaweza kuanza kulumbana kwa sababu ya kuoneana wivu? Jibu ni hapana. Hivyo basi, mawasiliano ya mara kwa mara huwaweka karibu na ni salama zaidi kuliko hata mngekuwa wawili chumbani.
Mawasiliano yasiwe yenye kuishia katika simu au mitandao, kama hamjafunga ndoa au tayari ni wanandoa lakini hamuishi pamoja, jitahidini kukutana mara kwa mara. Ikiwa mnaishi eneo moja, wekeni utaratibu wa kuonana kila inapobidi, hiyo itasaidia kukuza upendo na amani ambayo itayeyusha hulka za wivu.
Wakati ukitekeleza hili la kuonana mara kwa mara na mwenzi wako, si vibaya ukamwambia jinsi unavyoumizwa na tabia ya yeye kufanya mawasiliano ya karibu na watu wenye jinsia tofauti na yeye. Ukizungumza naye kwa upole, hali itakuwa nzuri kuliko kulaumu au kulalamika.
Hoja ya wivu iwekwe mezani halafu muijadili kwa upana. Kitendo cha kujadili na mwenzi wako jinsi wivu unavyokutesa, kitasaidia kuweka mwanga na kupata ufumbuzi wa tatizo husika. Kama atajua mambo ambayo akiyafanya utaumia halafu akatekeleza bila woga, maana yake atakuwa amedhamiria kukuumiza, hivyo hakufai kwa maisha yako.
Kama usipomwambia ukweli, itakuwa ngumu kwa mwenzi wako kujua jinsi ya kukusaidia kuyakabili hayo maumivu unayoyapata kwa sababu ya wivu. Waungwana wanasema kuwa dirisha la mazungumzo, hurahisisha yabisi kuwa laini. Anza leo kuamini katika kumshirikisha mwenzi wako uone matunda yake.
Shika kanuni hii “zungumza sana, ubishi hapana”, utakuwa kituko endapo utajibiidisha na ubishi badala ya kuzungumza kwa lengo la kumpa muongozo. Wivu ni chachandu lakini ukizidi mapenzi huonekana tamu yenye uchungu.
5. ACHA KUFANANISHA
Kuna tabia ambayo huwatesa watu. Ni kujifananisha na watu wengine. Mfano; Mwenzi wako ana ukaribu na mtu fulani, wewe badala ya kushughulikia tatizo ili amani ichukue mkondo wake, unaanza kumtazama huyo mtu halafu unajifananisha.
Pengine ukampima na kujifananisha kutokana na muonekano wako ukilinganisha na yeye. Unaweza pia kuweka kigezo cha fedha, ukajiuliza kama anakuzidi au unamzidi. Zaidi ya hapo, sura, mavazi na kadhalika, vinaweza kukutesa akili. Acha tabia hiyo, wekeza upendo na mambo yatakaa sawa.
Huwezi kujifananisha na mtu mwingine, vilevile kwa mwenzi wako, haipendezi pia haitakiwi kumlinganisha na yeyote yule. Kila mmoja yupo tofauti kwa sababu kadhaa. Pamoja na ukweli ni kwamba suala la kumtazama mtu na kumuona anakuzidi linaweza kukupa unyonge lakini ujinga wa kupindukia.
Watu wengi husumbuliwa na mawazo kuwa wenzi wao wanaweza kuwaacha na kwenda kuanzisha uhusiano na wengine wenye ubora kuliko wao. Kama mpenzi wako aliwahi kuvutiwa na mtu mwingine kabla yako, huwezi kujua, muhimu ni kuzingatia kile ambacho amevutika kwako.
Zingatia kuwa endapo mwenzi wako angekuwa amedata kwa mtu mwingine tofauti na wewe, huwezi kujua lakini ukweli ni kwamba msingekuwa na uhusiano wa kimapenzi mlionao leo. Achana na mawazo yasiyojenga, amini kuwa mwenzako amedata kwako ndiyo maana leo mpo pamoja.
Jenga utaratibu mzuri wa kuheshimu jinsi mwenzako alivyo. Kadhalika jiamini kwamba duniani hakuna mtu bora kama wewe, kwa hiyo usiishi kwa kumuogopa mtu kutokana na fedha zake au sifa nyingine yoyote. Dunia imeumbwa na vitu tofauti, hivyo na watu wametofautiana, ingekuwa wote tunafanana, hakika ingekuwa ni ulimwengu ‘unaoboa’ kuishi.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globapublishers.info
No comments:
Post a Comment