ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 20, 2012

Sindano 11 zitakazotibu tabia yako ya wivu - 6

WIVU hushamiri kwenye kipengele cha hisia. Hii ndiyo sababu ya wiki iliyopita kukutaka ubadili hisia kwa mawazo chanya.
Jifunze kutafsiri matendo yake kwa upendo. Vuta picha na ujipe hamasa chanya badala ya kuumia kwa kila atendalo. Katika hili, ni vizuri ukaongozwa na subira, kwani asili ya watu wenye wivu wa kupindukia, hukimbilia kupandwa na jazba, badala ya kuuliza kwa utaratibu na kupokea jibu linalojitosheleza.
Hata siku moja usije ukadanganywa kwamba ukiwa mkali ndiyo kutamfanya mpenzi wako asikusaliti. La hasha! Wekeza upendo kisha muishi kwa maelewano, hapo utaweza kumpa sababu ya kuishi kwa uaminifu. Utafiti unaonesha kuwa kundi la wasaliti wa uhusiano wao, huundwa na idadi kubwa ya watu waliochoshwa na migogoro ya kimapenzi.
Mantiki hapa ni kuwa mtu yupo kwenye uhusiano wake lakini anaamua kutoka nje baada ya kuona hana maelewano na mwenzi wake. Hivyo basi, ni vizuri ukawa unafuata hatua zinazofaa katika kupata ufumbuzi wa kila jambo unaloona halipo sawa kwa mwenzi wako, badala ya kugombezana. Itakugharimu.
Kama wivu wako unakufanya ujione wewe ni dhaifu, huna jambo la kufanya zaidi ya kuhakikisha unaishinda hali hiyo. Ukiwa na tabia ya kujiamini, itakusaidia kuufunika wivu, japo bado utaendelea kuwepo ndani yako lakini jinsi utakavyokuwa unashughulikia mambo yako na mwenzi wako, itakupa heshima zaidi.
Wivu ukizidi ni hatari kwa sababu unaweza kukuweka roho juu muda wote, ukaonekana mapepe na jamii ikakucheka kutokana na jinsi kichwa chako kilivyo rahisi kushika moto. Hii ina maana kuwa kudhibiti wivu ni kujiongezea heshima. Tafakari mwenyewe, unataka uheshimiwe au udharauliwe?
Unajidharau? Unakosea sana, muonekano wa juu hubadilika kutokana na wewe mwenyewe unavyoamua na kujipanga. Tatizo ni nguo? Mbona hivyo ni vitu vya kununuliwa? Unayo nafasi ya kutafuta na kupata, kwa hiyo punguza kuchachawa, wekeza upendo kwa sababu ndiyo dawa ya kila kitu.
Jambo lingine ni kuwa hutakiwi kumlazimisha mwenzi wako kuwa kama unavyotaka wewe lakini si vibaya kumshauri akawa na muonekano ambao unakuvutia. Labda anavaa akiwa anaacha wazi maungo yake, haitakiwi upandwe na jazba kisha kumtolea maneno makali, kaa naye mjadili mavazi sahihi.
Mapenzi ni diplomasia, hivyo wewe zungumza halafu muachie nafasi na yeye aseme linalompendeza. Hakikisha hutumii maneno ya kuudhi katika mazungumzo yenu. Vilevile na yeye anapaswa kudhibiti hasira zake. Mwisho mnakubaliana kwa upendo. Vuta picha inavyokuwa, mapenzi yanataka hivyo.
3. UNARUHUSIWA KUULIZA
Kuna jambo linakutatiza au umeona mwenzi wako anawasiliana na watu ambao huwaelewi, inawezekana pia akawa karibu na mtu wa jinsi yako, kwa hiyo unahisi kwamba unaweza kuibiwa. Suluhu hapo siyo kukaa na msongamano wa vitu kichwani, keti naye ukiwa na hali ya utulivu kisha muombe akupe ufafanuzi.
Kama una hasira usizungumze naye kwa sababu inaweza kuharibu maana. Siku zote, mazungumzo ya uhusiano wa kimapenzi, huendeshwa kwa njia ya upendo. Kama unahisi mbele utapandwa na jazba endapo hutapokea majibu mazuri, vema ungoje siku utakayokuwa na utulivu wa kutosha.
Usiyafanye mazungumzo yenu kuwa mahojiano. Jiweke kwenye kipengele cha mapenzi, kwa hiyo wewe siyo polisi. Pengine majibu yake yakawa siyo ya kunyooka, unachotakiwa kufanya ni kumuelewa au pale anapokuwa anasitasita, jaribu kumuongoza kuelekea kwenye jibu ambalo litasaidia ujenzi wa uhusiano wenu.
Hasira, jazba, ukali na mikunjo ya sura yako, vinaweza kumfanya ashindwe kukupa majibu sahihi.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

1 comment:

Anonymous said...

Mzee wa Vijimambo kama kuna dawa ya wivu ya vidonge (sio miti shamba)naomba tu unitafutie maana hizi makala nishoma weeeee ila najiona nimerudi pale pale. nampenda sana mpenzi wangu