ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 1, 2012

Sitta: Polisi wana ushahidi Mwakyembe kupewa sumu

Raymond  Kaminyoge
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta amemjibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nohodha kuwa hatapeleka ushahidi wa madai aliyotoa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe alilishwa sumu kwa kuwa polisi tayari wanao ushahidi.


Amesema wanachotakiwa kufanya Polisi ni kufanya uchunguzi kuhusu madai hayo ya Dk Mwakyembe kulishwa sumu kwa kuwa ushahidi wanao na wasianze kurushiana mpira.Waziri Sitta alisema hayo jana alipozungumza na mwandishi wa habari hizi kwa simu.

“ Waziri Nahodha anataka ushahidi gani ikiwa taarifa za madaktari zinazomhusu Dk Mwakyembe kuhusu sumu aliyopewa  zilishapelekwa polisi, anataka mimi nitoe ushahidi gani,” alisema Waziri Sitta.

Alisema suala hilo la kulishwa sumu ambalo limempata Waziri si la kawaida hivyo Polisi wanatakiwa kufanya uchunguzi ili kupata ukweli.Alisema kuendelea kukaa kimya kwa kisingizio cha ushahidi, kitawatisha Watanzania wengine kuwa wanaweza kufanyiwa chochote na sheria isifuate mkondo wake.

Juzi Waziri Nahodha alimtaka Sitta kuwasilisha ushahidi wa madai aliyoyatoa kuwa Dk Mwakyembe alilishwa sumu.
Alisema ushahidi wa suala hilo ukiwasilishwa ndipo uchunguzi unaweza kufanyika.

Kauli hiyo ya Nahodha ilikuja baada ya Jumapili iliyopita, Waziri Sitta akiwa na kundi la makada wenzake wanaojipambanua kuwa wapambanaji wa ufisadi alirejea kauli yake ya awali kuwa Dk Mwakyembe ambaye pia ni  Mbunge wa Kyela alilishwa sumu.

Sitta alisema hayo katika uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, Jijini Dar es Salaam.

“ Nasema Dk Mwakyembe kapewa sumu, kama vyombo vya uchunguzi vinasema siyo, basi watueleze ukweli, tena haraka,” alisema Sitta na kushangiliwa na waumini wa kanisa hilo.

“ Ni vipi uone binadamu ambaye ukimshika katika ngozi unga unamwagika chini, mhudumu anakuja kuufagia lakini baada ya saa moja unarudia tena, kitu hicho si cha kawaida,” alisema.Sitta alisema wamejaribu wameshindwa kwa kuwa Dk Mwakyembe analindwa kwa jina la Yesu ambalo ni kubwa kuliko yote.

Tangu Dk Mwakyembe arejee nchini Desemba 2011 kutoka katika Hospitali ya Apollo, India alikokuwa akitibiwa maradhi yaliyosababisha ngozi yake iharibike, Jumapili iliyopita ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuonekana katika hadhara ya watu.

Wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kahama, James Lembeli, Mbunge wa Viti Maalum Mbeya, Hilda Ngoye, aliyekuwa Mbunge wa Vunjo, Alloyce Kimaro na Mjumbe wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Makonda.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Mwakyembe aliapa kuendeleza mapambano dhidi ya ufisadi.Alisema, “ Nilifika Hospitali Oktoba 10 (mwaka jana) na tangu wakati huo sikuweza kuvaa viatu lakini leo hii naweza kuvaa viatu, kwa hiyo shetani ameshindwa.

Mwananchi

No comments: