ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 1, 2012

Sh18.4 bilioni za rada kununua madawati

Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa
SERIKALI imetangaza kuwa Sh18.4 bilioni kutoka katika fedha zilizorudishwa za rada zitatumika kwa ajili ya kununua madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Martha Mlata Viti Maalumu (CCM).

Mlata alitaka ufafanuzi ni kiasi gani cha fedha kilichotengwa kutokana na fedha za rada ambacho kitatumika kwa ajili kupunguza tatizo la madawati  kwa shule nyingi nchini.

Awali, katika swali la msingi Vicent Nyerere mbunge wa Musoma Mjini (Chadema) alitaka kujua Serikali imejipanga vipi katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa madawati kwa shule zote nchini.

Naibu Waziri alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2009/10, Serikali ilitoa  Sh1 bilioni kwenda katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya ununuzi wa madawati kwa shule za sekondari na mwaka 2010/11 ikatoa kiasi cha Sh3 bilioni kwa ajili ya kununua madawati kwa shule za msingi.

Hata hivyo alisema walimu wakuu wa shule nchini wamepewa mamlaka ya kutumia fedha zinazotengwa kwa ajili ya ukarabati kwa ajili ya kufanya ukarabati wa madawati yanayoharibika mashuleni mwao.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tmisemi), George Mkuchika alisema Serikali iko mbioni katika kukamilisha waraka ambao utasambazwa na Waziri Mkuu nchi nzima utakaoelezea kuwa huu ni mwaka wa kumaliza tatizo la madawati kwa shule zote.


Mwananchi

No comments: