ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 22, 2012

Waziri Chami: Mimi ni mzima wa afya

Waziri wa Viwanda na Biashara,
Dk. Cyril Chami



Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, amesisitiza kuwa yeye si moja kati ya mawaziri wanaonekana kuwa mzigo katika uongozi wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete.
Badala yake amewaasa Watanzania wasiwe watu wa mstari wa mbele kuhukumu watu.
Kadhalika, amewataka Watanzania kuacha tabia ya kuombeana mabaya, ikiwa ni pamoja na kuombeana vifo na kuzushiana magonjwa.
Dk. Chami aliyasema hayo kwenye kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV, kila siku ya Jumatatu usiku baada ya kutakiwa kueleza kuhusu uvumi uliotapakaa nchini kuwa ni mmoja kati ya mawaziri ambao ni mzigo kwa Rais Kikwete, kwa kuwa hawamsaidii kutokana na afya yake kutokuwa ya kuridhisha.

Hata hivyo, Waziri Chami aliwataka Watanzania kujemga utamaduni wa kuombea mazuri badala ya mabaya.
Aidha, aliwataka wananchi wa Moshi Vijijini kutokuwa na wasiwasi na maneno ya mitaani yanayovumishwa kuwa afya yake ina mgogoro kwani yu mzima wa afya.
“Rais ana vigezo vyake vya kuangalia ni nani anamsaidia na ni nani hamsaidii katika utendaji kazi, na ana uwezo wa kumteua mtu yeyote kuwa waziri au kumwacha, bila kujali hali yake kwani kuwa mgonjwa au kuwa mzima siyo kigezo cha kuteuliwa au kuachwa,” alisisitiza.
Dk. Chami alisema anashangazwa na habari zilizoandikwa na baadhi ya magazeti kwa kuwa yeye yu salama na haumwi ingawa ni kweli kuwa aliugua mwaka jana na kupelekwa nchini India kwa matibabu na kwamba hali kama hio inaweza kumtokea mtu yeyote.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, alilalazwa nchini India akitibiwa kwa siku 70.
"Na tangu nimerudi kutoka huko Desemba, mwaka jana, nimekuwa nikifanya shughuli zangu za kiutendaji wizarani," alisisitiza.
“Nimekuwepo ofisini toka mwishoni mwa mwaka jana na nafanya kazi kama kawaida hata siku za Jumapili nakwenda ofisini, nimeshiriki kwenye vikao vyote vya Kamati za Bunge na baadaye kwenye kikao cha Bunge. Sasa hawa wanaovumisha hayo, wao siyo madaktari na wala hawajaniona, sasa haya yanatoka wapi? Jamani tuache kuombeana mabaya, siyo vizuri,” alisema Waziri Chami.
Aidha, alisema watu wanaosambaza maneno hayo ni wale walioshindwa kwenye medani za kisiasa na hivyo kutumia njia hiyo kumharibia na kutaka kuwatia hofu wapiga kura wa Moshi Vijijini.
CHANZO: NIPASHE

No comments: