Kampeni Arumeru zapamba moto
CCM, CHADEMA vyashutmiana.jpg)
Mvutano kati ya Nyerere na Mkapa ulizuka, baada ya Mkapa kudai kuwa mbunge huyo sio mtoto wa baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere kwa kuwa anaifahamu vizuri familia hiyo.
Madai ya Mkapa aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) za ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, yalijibiwa na Nyerere, ambaye alisema Hayati Nyerere ni baba yake mkubwa.
Pia, mmoja wa watoto wa Hayati Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere, ambaye pia ni msemaji wa familia hiyo, aliingilia kati na kusema kuwa Vincent ni mdogo wao.
Vincent Nyerere, ambaye ni Meneja wa kampeni za mgombea ubunge wa Chadema Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, jana alisema kuwa Mkapa amemfuata Joseph
Butiku kuomba amuombea msamaha kwake (Vincent).
Akimnadi Nassari katika mkutano wa hadhara wa kampeni, Nyerere, alisema kuwa Mkapa alimweleza Butiku kuwa alikuwa anamtania ingawa mbunge huyo aliichukulia kauli ya Rais huyo mstaafu kama ya kweli.
“Huyu Butiku jana (juzi) alinipigia simu akiniomba tuachane na haya mambo ya malumbano kwa sababu Mkapa alikuwa ananitania na hakujua kama itakuwa hivyo, na mimi nimeendelea kulisema hadharani, sasa anaomba basi yaishe,” alisema Nyerere katika mkutano uliofanyika katika kijiji cha Msitu wa Mbogo, Kata ya Mbuguni.
Alisema kuwa amekataa kuombwa radhi kupitia njia ya simu au kukutana wawili na kuongeza kuwa anachotaka ni Mkapa kwenda Arumeru kuomba radhi katika mkutano wa hadhara ambao aliuhutubia na kumchafua kuwa hana undugu na Hayati Mwalimu Nyerere.
Aidha, alisema Mkapa anapaswa kuwenda kumuomba radhi kwenye ukoo wao. “Mimi ni wa ukoo wa Nyerere atake asitake, Nyerere ni baba yangu na sitaacha kumtaja kamwe,” alisema Vincent.
Alisema kuwa Mkapa alikuwa anamheshimu sana kama Rais mstaafu na alifahamu anahitaji kupumzika, ila kwa kumgusa kwa hilo na kumchafua hadharani kuwa anajifanya mtoto wa Nyerere, wakati hamfahamu, kwa hilo aende katika ukoo kumsafisha.
NIPASHE jana ilipomtafuta Butiku kuthibitisha kama amechukua jukumu la kuwapatanisha Nyerere na Mkapa, alisema kwa kifupi: “Kijana nisamehe.”
AMLIPUA TENDWA
Vicent Nyerere pia amemlipua Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, kwa kimzuia kumzungumzia Hayati Mwalimu Nyerere.
Amemshauri kuwa kama anahitji kuwa mmoja wa familia yao, anaruhusiwa kuandika barua kuomba kujiunga na ukoo wao kama alivyofanya Mkapa.
Alisema anamshangaa Tendwa kumpiga marufuku kuongelea mambo ya baba yake na kulidanganya Taifa kuwa watahatarisha amani na kujenga chuki kwa Taifa kwa kumzungumzia Nyerere.
“Mimi huyu ni baba yangu na kila siku lazima nimtaje na sisi wakatoliki tuna sala maalum ya kumwombea Nyerere na leo (jana) pia nimesali mara baada ya kuamka, sasa yeye ni nani anayenizuia kutaja jina la baba yangu, kama anataka ajiunge na ukoo wetu aombe kwa barua, kama alivyofanya mwenzake Mkapa, aliandika barua akaingizwa katika ukoo,”alisema Nyerere.
WAHUSIKA WA RADA WAKAMATWE
Aidha, aliitaka serikali kuwakamata waliohusika na kashfa ya ununuzi wa rada na sio kuwaacha majukwaani wakiendelea kuhutubia watu uwongo.
“Mimi nasema hawa watu mafisadi sio kujigamba fedha zimerudi Watanzania tunataka wahusika wakamatwe na wawekwe ndani kwani wamesababisha taifa kuingia katika shida na baadhi ya watu kulala njaa,” alisema Nyerere.
Natse: CCM WAOGOPWE
Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse aliwataka wakazi wa Arumeru Mashariki, kuiogopa CCM kama ukoma, akidai wanaendesha siasa za matusi jukwaani bila kujali watoto wadogo wanaohudhuria mikutano hiyo na wamesahau kuwa wanatumia rasilimali za nchi kwa watu wachache.
Alisema kuwa siku zote mti wenye matunda mazuri hutupiwa mawe na ndio maana CCM wanatupia matusi ya kila aina Chadema. “Sisi kwa sababu ni tunda zuri hatujibu matusi, tunajibu sera tu, cha muhimu mtunze kadi zenu za kupigia kura kwa sababu CCM ni mafisadi, wananunua shahada zenu,” alisema Natse.
Alisema anawashangaa Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, kusimama hadharani katika kampeni hizo na kutoa matusi.
Aliongeza kuwa Mkapa pia ni mwongo kwa sababu aliwarubuni watu wa Meru kuwa, atamshauri Rais Jakaya Kikwete kurudisha ardhi ya Meru kwa kufuta hati za wawekezaji walioshindwa kuendeleza maeneo yao endapo Sioi Sumari atakuwa Mbunge, wakati alipoingia madarakani alikuta ardhi ya Meru ipo mikononi mwa walowezi na alishindwa kufanya hivyo.
Alisema Mkapa alishindwa kuleta ukombozi wa ardhi hiyo kurudisha mikononi mwa Wameru.
Naye Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Babati kijijini na Mratibu wa Baraza la Wanawake Mkoa wa Manyara, Paulina Warsis, alimtaka Sendeka kwenda Simanjiro kushughulikia matatizo ya wananchi wake ambayo ni lukuki na kuacha kukimbilia jimboni humo kumnadi mgombea.
Mgombea wa Chadema, Joshua Nassari, alisema anaishangaa serikali ya CCM kwa kushindwa kujenga shule bora miaka hamsini ya Uhuru na katika kipindi cha miaka mitatu hawawezi kufanya maajabu yoyote.
“Shule ya Msingi Msitu wa Mbogo Mbuguni, hazina milango wala madirisha, hivyo inaoyesha hawa watu wameshindwa kuongoza hii nchi, hawa watu wamesababisha sida kwa watu sababu ya ufisadi na kulindana tusiwape kura,” alisema Nassari.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Rwakatare, alidai kuwa kuna kikosi cha Jamaica Mocas kutoka Musoma Mjini kwa lengo la vurugu kampeni na kuongeza kuwa chama chake kimejipanga kama polisi wakishindwa kuchukua hatua za kuwadhibiti watu hao.
CCM YAISHUTUMU CHADEMA
Katika hatua nyingine, CCM imekishutumu Chadema kwa madai kuwa kinakodisha vijana wa kufanya fujo katika mikutano yao pamoja na kupora shahada za kupiga kura za wazee na wanawake.
Shutuma hizo zilitolewa jana na Meneja wa kampeni za CCM katika Jimbo la Arumeru Mashariki, Mwigulu Nchemba katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ngome kuu ya chama hicho.
Chama hicho kimesema kuwa makada wa chama hicho wameanza kupita nyumba kwa nyumba kufanya hivyo, jambo ambalo sio la kistaarabu katika siasa za sasa.
Aidha Mwigulu aliongeza kuwa Chadema kinaendesha kampeni za uchonganishi na uchochezi wakidai kuwa mgombe wa CCM sio raia wa Tanzania wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) tayari imeshathibitisha kuwa mgombea ni raia wa Tanzani na ana haki ya kugombea.
Alisema kuwa kuwa Chadema kinaelekea kukosa mwelekeo na kuanza kutafuta mbinu chafu za kutafuta huruma ambapo pia kinaeneza uvumi kuwa zimetolewa Shilingi bilioni tatu kwa wananchi na mwananachi atakayezikosa atakuwa amepuuzwa.
“Hizi sio siasa za kistaarabu, tushindane kwa hoja na sera na sio kutumia njia za msituni kuwarubuni wapiga kura,” alisema Nchemba.
Akizungumzia suala la fujo, Nchemba, alisema kuwa CCM ni chama kikubwa chenye wanachama wengi na ikiwa chama hicho hakitaaacha vitendo hivyo kinaweza kujilinda.
“Fujo hizo kwa kweli zinawakosesha sifa wapinzani mbele ya wapiga kura, sisi tunaweka wazi kuwa hatutegemei polisi, wanatuma watu wawili watatu kutusumbua, tunao uwezo wa kuwashughulikia,” alisema.
Pia aliwataka wana CCM kama hawafurahishwi na sera za vyama vingine ni vyema wakakaa majumbani na kusubiri mikutano ya chama chao ili kuepusha vurugu.
Kadhalika, aliwataka wanachama wa Chadema kama wanakerwa na mikutano ya CCM wakae nyumbani na kusubiri mikutano yao ili kuondoa vurugu katika kampeni.
Wakati CCM wakitoa malalamiko hayo, Chadema nao wamewatuhumu wana CCM kuwazuia wananchi kuhudhuria katika mikutano ya hadhara sambamba na kusambaza waraka wa kuwachafua viongozi wa Chadema.
Katika waraka huo, ambao Chadema inasema unasambazwa na CCM, unadai kuwa Chadema ni cha kifalme kutokana na kujaza ndugu katika nafasi za ubunge na uongozi wa chama hicho.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Ccm kwa ujumla inaeleweka kwamba waongo ni wengi kuliko watekelezaji, na safari hii kazi wanayo nzito.
Post a Comment