ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 14, 2012

Chadema wamkaanga Mzee Mkapa Arumeru

WADAI ALIUZA NCHI AKIWA IKULU, CCM WAHAHA KUVUNJA MAKUNDI, NASSARI AAHIDI KUREJESHA ARDHI ILIYOPORWA. Waandishi Wetu, Arumeru, JOTO la kuwania ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha linazidi kupanda.

Jana Chadema kilimgeukia Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye aliongoza uzinduzi wa kampeni za CCM juzi kikidai kwamba kiongozi huyo hana uadilifu wa kushiriki kampeni za uchaguzi huo mdogo.

Madai hayo ya Chadema kwa Mkapa yalitolewa katika mikutano iliyofanyika katika Kata za Legaruki, Poli, Selunani na Sing’isi, siku moja baada ya Mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM kusema chama hicho cha upinzani hakina sera zinazoweza kuwakomboa wana Arumeru na kuwataka wasimchague mgombea wake, Joshua Nassari.
Kadhalika, Mkapa katika mkutano huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Ngaresero, Usa River, alimshambulia Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere akisema katika kuishi na kufanya kazi na Hayati Mwalimu Julius Nyerere hakuwahi kusikia jina la Vicent likitajwa katika ukoo huo wa Baba wa Taifa.


Jana, mbunge huyo ambaye ni Meneja Mwenza wa kampeni za Chadema katika uchaguzi huo alimjia juu Mkapa akisema kiongozi huyo si mwadilifu akidai kwamba ndiye chanzo cha matatizo mengi yanayolikabili taifa kwa sasa.
 “Tuliwahi kusema kuhusu Mzee Mkapa na tukapata wito kwamba tumwache apumzike baada ya kustaafu lakini inavyoonekana hapendi kupumzika na badala yake amekuja hapa (Arumeru) na kuanza kutuchokonoa.
Mimi nasema huyu mzee siyo mwadilifu kwani alifanya madudu mengi alipokuwa Ikulu,” alisema Nyerere na kuongeza::
“Eti jana (juzi) aliwaahidi kwamba atashughulikia matatizo ya ardhi, kwani aliyesababisha matatizo haya yote ni nani?…. ni yeye. Halafu yeye sasa siyo Rais, siyo diwani wala mbunge, kwa hiyo hana uwezo wowote wa kutatua matatizo yenu, wala msidanganyike.”
Nyerere alidai kwamba utawala wa Mkapa ni mbaya kuliko mwingine uliowahi kutokea nchini kwani ulisababisha mauaji Kisiwani Pemba kiasi cha Watanzania wengine kugeuka wakimbizi baada ya kukimbilia eneo la Shimoni, Mombasa, Kenya.
Mbunge huyo wa Musoma Mjini alisema matatizo ya ajira nchini ni matokeo ya ubinafsishwaji wa viwanda vyote uliofanywa na Serikali ya Mkapa... “leo hii ukiwa mijini huwezi kujua nani ni kichaa na nani mzima, vijana wengi wanaokota makopo. Ni bingwa wa kuuza kila kitu, aliuza benki zote na aliuza viwanda vyote na sasa hivi tunavyozungumza viwanda vingi vimegeuzwa magodauni (maghala) ya kuhifadhia bidhaa za Wachina badala ya kuwa vitovu vya ajira kwa vijana wetu.”
Nyerere alidai pia kwamba Mkapa ni kiongozi pekee ambaye baada ya kukaa madarakani miaka 10, kisha kupata fursa ya kulipwa pensheni ambazo ataendelea kuzipata maisha yake yote, aliingiwa na tamaa ya mali, hivyo kujiuzia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira.
“Kama tusingetumia nguvu ya umma kuudai mgodi huo asingeurudisha, sasa mtu wa aina hiyo ana kitu gani cha kutuambia hapa Arumeru?... Kama kweli ana uadilifu, basi aje hapa kesho atujibu ili tumwambie madudu yake mengine aliyofanya akiwa Rais,” alidai Nyerere.
Kuhusu uhusiano wake na Baba wa Taifa, Nyerere alisema kimsingi yeye ni mwanafamilia kwani Baba yake, Mzee Kiboko Nyerere alikuwa ndugu wa damu wa Julius Nyerere na kwamba Mkapa si mwanafamilia hiyo hivyo hawezi kufahamu masuala ya familia yao.
Nassari na Ardhi
Kwa upande wake, Nassari katika mikutano ya jana alisema anatambua matatizo ya ardhi ambayo yanawakabili wakazi wa Arumeru na kusema: “Niko tayari kuyabeba hadi bungeni Dodoma ili kuyapatia utatuzi.”
“Baba zangu na mama zangu, mimi ni mtoto wenu niliyezaliwa hapa na kukulia hapa, tuachane na wageni wanaojifanya kwamba wao ni wenyeji kwa lengo la kupata ubunge, nipeni kura zenu maana matatizo haya yamekuwa ni sehemu ya maisha yangu,” alisema Nassari.
Alisema migogoro mingi ya ardhi ni matokeo ya udhaifu wa uongozi ambao haujali maslahi ya umma, hivyo kugawa ardhi kwa wageni ambao wengi wamekuwa wakikiuka matumizi yake na sheria za nchi... “Ninachoweza kuwaahidi ni kushughulikia suala hili, kama leo hii CCM wanasema watatatua tatizo hili, wakija waulizeni kwamba miaka yote walikuwa wapi, maana matatizo haya yamekuwapo kwa muda mrefu.”
Katika mikutano ya juzi iliyofanyika katika mji mdogo wa Tengeru, Nassari alisema: “Ndugu zangu siombi ubunge ili niendeshe magari ya kifahari na kuishi kwenye nyumba za anasa, nimezaliwa hapa hivyo nitahangaikia matatizo yetu ambayo yamekuwa kama donda ndugu kwa miaka mingi.”
Katika Kijiji cha Shambarai, Kata ya Mbuguni, aliwaomba wananchi wamchague ili akabiliane na matatizo ya elimu na afya, pia kutafuta ufumbuzi wa tatizo la maslahi duni wanayolipwa wafanyakazi katika mashamba ya maua... “Ninafahamu vizuri shida mnazopata kina mama, kwa sababu mama yangu amenisomesha kwa kuamka saa 11:00 alfajiri kwenda soko kuu kununua mboga akifukuzwa na mgambo wa halmashauri ili apate fedha za kunisomesha, leo hii ni mgonjwa wa kifua kutokana na baridi, mvua na jua kali.”
Mbunge wa Arusha mjini (Chadema), Godbless Lema alisema Nassari ni mgombea shujaa anayeweza kuwawakilisha ipasavyo bungeni wananchi wa Arumeru badala ya kuchagua wabunge wa CCM ambao kazi yao kubwa bungeni ni kuzomea jambo ambalo alisema haliwezi kubadilisha maisha ya wananchi.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema kuendelea kuichagua CCM ni kuamua mwenyewe kuchagua ugumu wa maisha kwani wabunge wa CCM wamekuwa wakiunga mkono bajeti zinazowatesa wananchi.

Mgombea TLP na Mkapa
Mgombea wa ubunge wa TLP, Abraham Chipaka jana aliwataka wakazi wa Meru kupuuza maneno ya Mkapa aliyotoa katika uzinduzi wa kampeni za CCM kuwa wananyang’anya ardhi inayomilikiwa na walowezi na kupawe wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni, Chipaka alisema wakazi wa Meru wanapaswa kujiuliza alikuwa wapi kwani tangu wakati wa utawala wake ardhi ya Wameru ilikuwa inamilikiwa na walowezi... “Msikubali kudanganyika ndugu zangu, chagueni mbunge wa upinzani ndiye atarejesha mashamba yenu.”
Alisema miaka 50 ya Uhuru Serikali ya CCM imeshindwa kutatua matatizo ya Wameru ambao wengi sasa ni masikini, hawana huduma muhimu, hawana ardhi , hawana barabara wala maji akisema ni aibu Meru ikiwa na utajiri mkubwa maisha ya watu wake bado ni duni huku jimbo hilo likigeuzwa ni la kifalme kutokana na mgombea wa CCM, Sioi Sumari kutaka kumrithi baba yake marehemu Jeremiah Sumari.

CCM na makundi
Wakati Chadema wakiendelea na kampeni, Chama cha Mapinduzi (CCM), jana viongozi wake waliripotiwa kushinda kwenye vikao katika mji wa Kikatiti, hoteli ya Gateway iliyopo eneo la Leganga na Ofisi ya CCM mkoa wa Arusha kusaka suluhu ya makundi yanayodaiwa kudhoofisha nguvu ya chama hicho kwenye kampeni.
Habari zinasema CCM kiliwakutanisha viongozi na makada mbalimbali wa chama hicho wakiongozwa na Katibu Mkuu wake, Willison Mukama pia kupanga mikakati mbalimbali ya ushindi katika jimbo la Arumeru Mashariki.
Vyanzo vya habari vya gazeti hili vimedai ya kwamba kikao katika ofisi za mkoa kilianza saa 4.00 asubuhi na kumalizika majira ya saa 9.30 mchana ambapo kwa pamoja walikubaliana kuungana kuwa kitu kimoja kunyakua ushindi.
Vyanzo hivyo vimeliambia gazeti hili kwamba mkutano huo uliweka mkakati wa viongozi wa CCM ngazi ya kitaifa kwa kushirikiana na wale wa mkoani Arusha kushambulia kila kata katika mikutano ya chama hicho kama njia mojawapo ya kunyakua ushindi... “Tumeambiwa tushikamane na tuungane kuwa kitu kimoja,” alisema mmoja wa wajumbe wa mkutano huo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alikataa kuzungumzia mikutano hiyo akisema ni ya ndani na haiwahusu wanahabari.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martine Shigella alikutana na wanachama wa umoja huo wilayani hapa kuweka mikakati ya ushindi pamoja na kuwasihi kuvunja makundi. Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Meru, Esther Maleko.

CCM, Chadema vita
Vyama vya CCM na Chadema vimeanza kushutumiana kila kimoja kikidai kingine kuandaa kundi la vijana wake na kuwavalisha sare za chama kingine ili wafanye vurugu za katika mikutano ya kampeni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, Mukama na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba walisema  makundi hayo yameandaliwa kufanya vurugu ili ionekane chama kimoja kuwa ndicho chanzo cha vurugu.
Akitoa tuhuma hizo, Mwigamba alidai kwamba wamepata taarifa kuwa CCM kuandaa vijana wafanya fujo huku wakiwa na sare za Chadema.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa Chadema kimejipanga kufanya kampeni za kistaarabu na kiustadi kwa kuwa kina uhakika wa ushindi lakini akadai kuwa kuna njama za kuwepo vurugu zitakazoanzishwa na vijana wa CCM.
“Tumejiandaa kuwadhibiti tunaomba wasithubutu kufanya vurugu hizo wakiwa na sare zetu kwani tumejipanga kuhakikisha hatuhusiki na vurugu zozote ili ushindi upatikane kihalali,” alisema Mwigamba.
Juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM, Mukama alisema wamepata taarifa za chama kimoja bila kukitaja kununua sare za CCM ili zitumiwe na vijana wake kufanya vurugu... “Tuna taarifa wamenunua watu wavae sare zetu ili waje kufanya vurugu na ionekane CCM ndiyo wamezifanya.”
Alisema CCM ina uzoefu mkubwa  katika chaguzi hivyo, hakitarajii kufanya vurugu na itahakikisha kinafanya kampeni zenye weledi wa hali ya juu... “Tutawashinda kwa sera nzuri na siyo kwa vurugu kama wao wanavyojipanga,” alisema Mukama.

TLP wazindua kampeni
Mwenyekiti wa (TLP) Augustine Mrema amewaomba wakazi wa Arumeru Mashariki kumpa zawadi kwa kumchagua kuwa mbunge wa jimbo hilo, Abraham Chipaka kwani bila yeye Wameru wote wangekuwa hawana dini kutokana na makanisa yao kuteketea moto kutokana na vurugu za kidini zilizotokea mwaka 1993.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Imbaseni, Kata ya Maji ya Chai jana, Mrema huku akitumia gazeti la Kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Umoja, lililochapishwa mwaka 1993, lililoelezea jitihada zake katika kusuluhisha vita hiyo, alisema hakuna zawadi ambayo wakazi wa jimbo hilo wanaweza kumpa zaidi ya ubunge.
“Mimi ndiye nilikuja kuwaokoa huku Meru, vita vilikuwa vimepamba moto, makanisa yanachomwa moto, watoto wenu wanashindwa kwenda shule vijana wanapigana… mimi nikaja huku bila vitisho wala helikopta tutakaa na maaskofu na nikamaliza vita vyenu” alisema Mrema na kuongeza:
“Ndugu zangu muogopeni Mungu, tafuteni historia yenu, mimi ni ndugu yenu za damu, waulizeni hawa wanaokuja sasa wakati wa vita vyenu walikuwa wapi?”
Habari hii imeandaliwa na Neville Meena, Filbert Rweyemamu na Moses Mashalla, Arumeru.

Mwananchi

No comments: