ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 20, 2012

Jengo la kisasa kujengwa uwanja wa ndege wa Dar

 
Serikali ipo katika mchakato wa kutafuta mwekezaji atakayejenga jengo jipya na la kisasa kwenye uwanja wa ndege wa Kikataifa wa Mwalimu Julius Nyerere litakalojulikana kama (Terminal three) na tayari makampuni 19 yameshajitokeza kuwania nafasi hiyo.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa  Uchukuzi, Omari Nundu, wakati akizungumzia kongamano  la Taifa la Usafiri wa Anga litakalofanyika katika Dar es Salaam kesho hadi Jumatano.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuuwezesha uwanja huo kuhudumia mashirika ya ndege zaidi, na kupokea na kusafirisha abiria milioni sita kwa mwaka ambapo kwa sasa uwanja huo una uwezo wa kusafirisha abiria milioni 1.5.
“Tupo kwenye mchakato wa kuruhusu mashirika zaidi ya ndege kuja kuwekeza nchini ili kusaidia nchi yetu kuongeza mapato kwa kuongeza idadi kubwa ya watalii,” alisema Nundu.
Alisema litawakutanisha wadau wa sekta ndogo ya usafiri wa anga, utalii, uchumi na fedha ambao watakuwa ni wataalamu 150 kutoka ndani na nje ya nchi.
Alisema lengo kongamano hilo ni kujadili na kupata mawazo ambayo yatasaidia kuimarisha usafiri wa anga kwenye maeneo ya uwekezaji katika miundombinu ya viwanja, uendeshaji na uendelezaji viwanda vya ndege na mashirika ya ndege.
CHANZO: NIPASHE

No comments: