![]() |
| Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa |
Uongozi wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, klabu ya Yanga, umesema kuwa kipigo walichopata cha bao 1-0 kutoka kwa Zamalek na kuondolewa katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika ni halali na hivyo hawafikirii kuchukua hatua zozote za kukata rufaa.
Yanga walirejea nchini jana asubuhi wakitokea Cairo, Misri, ambako baada ya kufungwa, walitolewa kwa kip[igo cha jumla cha mabao 2-1 kufuatia sare ya awali ya bao 1-1 waliyopata wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, ambaye alikuwa Cairo na timu hiyo, alisema kwamba wanamshukuru Mungu kwa kurejea salama na kinachofuata ni kujipanga vyema ili kuhakikisha kuwa wanatetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Bara.
Mwesigwa aliiambia NIPASHE kwamba Yanga haina mpango wowote wa kukata rufaa dhidi ya Zamalek ambayo inadaiwa iliruhusu watu wengine zaidi ya maelekezo yaliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF); ya kutaka kila timu kuwa na watu uwanjani wasiozidi 40."Hakuna kitu kama hicho (rufaa)… hatujazungumzia rufaa tukiwa Cairo na hata leo (jana) baada ya kufika. Tutafanya tathmini na kuangalia wapi tulipokosea ili tusonge mbele siku zijazo," alisema Mwesigwa.
Kocha wa Yanga, Kostadin Papic, alisema kuwa mipango yao ya kusonga mbele kwenye mashindano hayo ya kimataifa iliingia doa tangu katika mechi yao ya kwanza nyumbani wakati walipokubali kutoka sare ya 1-1.
Akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya kurejea nchini, Papic alisema kwamba timu yake haikuwa na bahati kwa sababu ilicheza kwa kiwango cha juu katika mechi zote mbili ukilinganisha na wapinzani wao, lakini haikuibuka na ushindi.
Papic alisema kuwa licha ya kutolewa, lakini Zamalek hawakuwa na kazi rahisi ya kuwaondoa kwenye michuano hiyo kwa sababu wachezaji wake walipambana kwa muda wote wa mchezo.
"Timu imetolewa lakini mechi haikuwa rahisi, tunakubaliana na matokeo na tutakuwa tayari kupambana tena katika mashindano hayo mwakani, kila siku huwa kuna nafasi nyingine ya kujaribu," alisema Papic.
Papic aliongeza kuwa anawapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha kwamba walikuwa wanataka ushindi kwenye mechi zote mbili, lakini kwenye soka matokeo ya mwisho yanapaswa kuheshimiwa na hivyo Zamalek ndio iliyofanikiwa kusonga mbele.
Katika hatua nyingine, Papic alisema kwamba hakuna kulala na leo asubuhi kikosi chake kitaanza kujiandaa na mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam ambayo itachezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
"Timu iko vizuri na mechi hiyo itakuwa nzuri kwa sababu joto la wachezaji wangu bado liko juu, kwangu naona mechi hii imekuja katika wakati muafaka," Papic aliongeza.
Jana, baadhi ya vyombo vya habari vilidai kwamba uongozi wa Yanga una mpango wa kukata rufaa kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kupinga kipigo walichopata kutoka kwa Zamalek. Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, ambaye ndiye aliyedaiwa kusema kuwa watakata rufaa, hakupatikana jana kuzungumzia maelezo mapya ya katibu wake, Mwesigwa.
CHANZO: NIPASHE
.jpg)
No comments:
Post a Comment