ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 10, 2012

Madaktari waipuuza Mahakama, mgomo waendelea

HALI ya utoaji wa huduma ya matibabu katika hospitali za serikali imezidi kuwa tete licha ya mahakama kuwataka madaktari hao kusitisha mgomo kwa kuwa ni batili. 

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili jana katika hospitali kadhaa za serikali jijini Dar es Salaam imeonyesha hali kutorejea kama inavyotakiwa na baadhi kuwapo kwa huduma za kusuasua huku vyumba vingi vya madaktari vikibaki bila wahusika.
 

Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) zimeendelea kusimama kutokana na mgomo huo. 

Katika hospitali ya Wilaya ya Temeke, hali ilikuwa mbaya kwani hakuna huduma yoyote iliyotolewa kwa wagonjwa wa nje huku vyumba vya madaktari vikiwa vimefungwa na baadhi ya madaktari wakitoa huduma kinyemela kwa kupewa kitu kidogo. 

“Hali ni mbaya sana, nimemleta mke wangu na huduma imekuwa shida kuipata, lakini nimezungumza na dakatari ndio akaamua kunisaidia kunitibia mgonjwa wangu,” alisema Yahaya Mtunzi. 

Katika hospitali ya Amana hakuna huduma iliyokuwa ikiendelea zaidi ya kitengo cha huduma ya dharura, wodini huku uongozi wa hosptiali hiyo ukisitisha utoaji huduma ya kliniki. 

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshaki Shimwela alisema, wameamua kusitisha baadhi ya huduma kutokana na kuzidiwa na kazi. 

Kwa upande wa hospitali ya Mwananyamala, huduma zilionekana za kusuasua ingawa Katibu Mkuu wa Afya hospitalini hapo ,Edwin Bisakala kudai kuwa hakuna mgomo wa madaktari katika hospitali hiyo. 

Gazeti hili lilishuhudia vyumba viwili tu vikiwa na madaktari, kati ya zaidi ya 10 hospitalini hapo. 

Kutoka Dodoma, Sifa Lubasi anaripoti kuwa, utoaji wa huduma za Afya atika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma umeanza kuzorota baada ya madaktari walio katika mafunzo kuendelea na mgomo na kusababisha upungufu mkubwa wa madaktari hospitalini hapo. 

Madaktari zaidi ya 37 ambao wako katika mafunzo ya vitendo wamegoma kwa lengo la kuishinikiza Serikali kuwaondoa madarakani Waziri wa Afya na naibu wake. 

Upungufu huo umesababisha huduma zinazotolewa hospitalini hapo kupitia kwa madaktari walio kazini zimeanza kuzorota kutokana na madaktari hao kulemewa na wagonjwa. 

Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani, Dk. Zainab Chaula alisema, hali katika hospitali hiyo ni mbaya kutokana na ukweli kuwa madaktari waliogoma kuwa wengi kuliko madaktari waliopo. 

Alisema kuwa licha ya upungufu huo wamejipanga kutoa huduma kwa wagonjwa wote ili kuweza kunusuru maisha ya wananchi. 

Wagonjwa waliokuwa katika foleni ya kuingia kwa daktari wamekilalamikia kitendo cha mgomo na kusema kuwa, haipendezi kwa nchi kama tanzania kuwa na watu wasio na huruma kwa binadamu wenzao bila kujali hata watoto wanaofika hospitalini hapo kwa matibabu. 

CHAMA cha madaktari Kanda ya Kaskazini, baada ya kukutana katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi, kimebariki kuungana na wenzao kufanya mgomo uliotangazwa na chama hicho kitaifa kwa lengo la kushinikiza serikali kuwawajibisha Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Hajji Mponda na naibu wake Dk Lucy Nkya, anaripoti Nakajumo James kutoka Moshi. 

Akitangaza msimamo huo, katibu wa chama hicho katika kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro, Dk Lairumbe Kivuyo alisema wamefikia uamuzi huo kuunga mkono madai yao waliyotangaza mwezi mmoja uliopita. 

Alisema maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao chao cha pamoja kilichofanyika katika hospitali ya rufaa ya KCMC na kukubaliana kusitisha huduma kwa wagonjwa wa nje na waliopo wodini hadi hapo madai yao yatakapotekelezwa. 

Dk Kivuyo alisema pamoja na kuanza kwa mgomo huo lakini bado wataendelea kukutana madaktari wa idara tofauti ili kufanya majadiliano ya jinsi ya kushiriki mgomo huo hadi hapo serikali itakapowasiliza. 

Mmoja wa wagonjwa hospitalini hapo, Mussa Bushir anayesumbuliwa na uvimbe tumboni amedai kutopata huduma licha ya kufika hospitalini hapo tangu saa nne asubuhi akitokea kijiji cha Mikocheni wilayani Moshi vijijini. 

Pamoja na hali hiyo, Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk Moshi Ntabaye akizungumza na gazeti hili alielezea msimamo wake wa kutozungumzia suala hilo kwa madai kuwa msemaji ni mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Leonidas Gama.

Habari Leo

No comments: