ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 14, 2012

Madaktari wakosa kauli huhusu Dk. Mponda, Nkya

Rais wa MAT,
Dk Namala Mkopi
 
 


Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimesema hawana la kusema baada ya Rais Jakaya Kikwete kuweka wazi msimamo wake kwamba hata kama akiwafukuza kazi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya  hakuwezi kumaliza matatizo yao.
Rais Kikwete aliweka wazi msimamo wake juzi alipolihutubia Taifa kupitia kwa wazee wa mkoa wa Dar es Salaam na kuongeza kuwa matatizo ya madaktari hayawezi kulizwa kwa viongozi hao kufutwa kazi, badala yake kinachotakiwa ni kuweka mfumo mzuri ndani ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kina mtu atakayekuwa anaiongoza aweze kuufuata.
Rais wa MAT, Dk Namala Mkopi, alisema hawana cha kusema kufuatia kauli ya Rais na kuongeza kuwa madai yao yanashughulikiwa na Rais Kikwete kama wallivyokubaliana wiki iliyopita.

“Kwa hilo sina comment (maoni) ila msimamo wetu ni ule ule kwa kuwa tayari tulishazungumza na Rais na tukatoa tamko katika mkutano wetu hivyo kwa sasa siwezi kutengeneza opinion (maoni)  kwani tulishaafikiana,” alisema.
Dk. Mkopi alisema wao tayari walishaongea na Rais Kikwete, hivyo kwa sasa hawana maoni kwa kuwa juzi Rais alikuwa anazungumza na wazee na sio madaktari. Alisema pia kuwa hawakumsikia Rais Kikwete akizungumzia chochote kwamba Dk. Mponda na Nkya hawataondolewa.
Wakati huo huo, wanaharakati wamesema kuwa harakati walizokuwa wakizifanya zilikuwa zinalenga kuishinikiza serikali kutatua mgomo wa madaktari ili wananchi wasiendelee  kufa na sio vinginevyo na si kuchochea mgomo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba, alisema kauli zilikuwa hazilengi kushinikiza kuwepo kwa mgomo wa madaktari na kwamba nia yao ilikuwa ni kumaliza mgogoro ili wananchi wasikose huduma pindi wanapofikishwa hospitalini.
Kuhusu kauli ya Rais Kikwete ya kuwashangaa kwa kushindwa kukemea mgomo huo, Dk. Bisimba alisema walichukua hatua zikiwemo za kukutana na madaktari kwa ajili ya kusikiliza madai yao ya msingi kwa serikali.
CHANZO: NIPASHE

No comments: