Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya, wazee na wananchi wa wilaya hiyo wamewasha moto upya katika sakata la ugonjwa unaomsumbua Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, baada ya kuazimia kuunda kamati itakayokwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili kuishinikiza serikali kutoa tamko juu ya suala hilo.
Diwani wa Kata ya Bujonde, Lameck Mwambafula, akizungumza katika mkutano huo alisema ipo haja kwa Rais Kikwete kumfukuza kazi Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai (DCI), Kamishina Robert Manumba, kutokana na taarifa yake ambayo anadai kuupotosha umma na kutaka kuficha ukweli uliopo katika suala zima la kinachomsumbua Dk. Mwakyembe.
Kamati hiyo inatarajiwa kuundwa kuanzia wiki ijayo na inakusudia kuonana na Rais Kikwete kwa lengo la kuondoa utata wa taarifa zinazotolewa na watendaji wakuu wa Jeshi la Polisi na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu chanzo cha ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe ambazo zinawachanganya Watanzania.
Azimio hilo limefikiwa juzi kwa pamoja katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Siasa, mjini Kyela, chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Gabriel Kipija.
Mkutano huo uliitishwa kwa lengo la kujadili hatima ya Mbunge wa Kyela ili kuishinikiza serikali kueleza uwazi juu ya ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe hasa baada ya kutokea mkanganyiko miongoni mwa watendaji wa serikali juu ya chanzo cha ugonjwa wake.
Kipija akizungumza baada ya washiriki wa mkutano huo kutoa hoja mbalimbali, alisema pendekezo la kuunda kamati hiyo itakayowashirikisha watu mbalimbali wa Wilaya hiyo, litazingatiwa haraka bila kujali itikadi za kisiasa.
“Hapa tunachotaka ni kuunda tume madhubuti itakayoweza kumfikishia taarifa Rais Kikwete juu ya kilio cha wananchi wa Kyela katika suala la utata wa ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe,”alisema Kipija.
Kipija akisoma tamko hilo, alisema wananchi wa Kyela wanampongeza sana Rais Kikwete kwa uamuzi wake wa kuamuru Dk. Mwakyembe apelekwe haraka kwenye matibabu nchini India ambako kuna madaktari waliobobea katika fani ya maradhi ya binadamu.
Alisema hata hivyo, wananachi wa Kyela wanashtushwa kwa mkanganyiko wa viongozi ngazi za juu serikalini kutoa taarifa zinazokinzana na kusababisha kuzua maswali mengi juu ya afya ya Dk. Mwakyembe ukichukulia taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, aliyetamka wazi kuwa alilishwa sumu.
“Je ukweli ni upi? Wananchi wa Kyela tunataka kujua utata huu unatokana na nini? Na kinafichwa kitu gani kwa faida ya nani? Wananchi Kyela tunaiomba serikali kupitia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, atoe tamko juu ya kiini cha ugonjwa huo na hali halisi ya ugonjwa wa Dk. Mwakyembe,” alisema Kipija.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment