Mambo yaliwaendea vyema mashabiki wa Simba jana baada ya mabao mawili ya John Bocco na jingine la Kipre Tchetche kuipa Azam ushindi wa 3-0 dhidi ya Coastal na kukwea hadi katika nafasi ya pili huku mahasimu wa jadi wa ‘Wekundu wa Msimbazi’, Yanga, wakiporomoshwa hadi katika nafasi ya tatu.
Mafisango aliifungia Simba bao la utangulizi katika dakika ya 25 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa ‘yosso’ Jonas Mkude na kupiga shuti kali la umbali wa mita 30 lililomshinda kipa Ntalla.
Awali, Okwi aliyegongesha mwamba mara mbili na kutoa pasi zote za mabao yaliyoipa Simba ushindi wa 2-1 katika mechi yao ya Jumapili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Kiyovu ya Rwanda, alikumbushia tena makali yake kwa kupiga shuti kali katika dakika ya 50 lililogonga mlingoti wa goli na kutoka nje.
Kagera walijibu mashambulizi katika dakika ya 57 na mshambuliaji wao Themi Felix akawasawazishia kwa kupiga shuti lililomshinda kipa Juma Kaseja kufuatia piga nikupige iliyotokea langoni mwa wenyeji.
Dakika moja kabla ya kumalizika kwa muda wa kawaida, yosso Shomari Kapombe aliangushwa na beki David Charles katika eneo la penati na refa Ronald Swai wa Arusha akaipa Simba penati iliyopigwa kiufundi na Mafisango na kuwapa bao la pili vinara hao wa kwenye msimamo wa ligi.
Katika dakika za majeruhi, Okwi aliyekuwa akiwasumbua mara kwa mara mabeki wa Kagera, aliifungia Simba bao zuri la tatu, akitumia vyema pasi safi aliyopewa na Felix Sunzu, mshambuliaji wa kimataifa kutoka Zambia aliyeifunga mabao yote ya Simba katika mechi yao ya Jumapili dhidi ya Kiyovu.
Kwa matokeo hayo, Simba wamejichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi 40, tatu zaidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga ambao hata hivyo, bado wana kiporo cha mechi moja kulinganisha na mechi 18 za ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Kagera waliendelea kubaki katika nafasi ya saba baada ya kufikisha pointi 24 kutokana na mechi 20 walizocheza.
Coastal yenye pointi 26, inaendelea kukamata nafasi ya sita baada ya kushuka dimbani mara 20.
Mabao mawili ya jana yalimfanya John Bocco aendelee kujichimbia kileleni mwa orodha ya wafungaji wanaoongoza katika ligi kuu ya Bara baada ya kufikisha mabao 13 na kufuatiwa na Kenneth Asamoah na Emmanuel Okwi wenye mabao 10 kila mmoja.
Ligi hiyo itaendelea keshokutwa ambapo Azam iliyocheza mechi 19 itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga.
Vikosi:
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Said ‘Cholo’, Amir Maftah, Kevin Yondan, Juma Nyosso, Jonas Mkude/Uhuru Selemani (dk.65), Shomari Kapombe, Patrick Mafisango, Felix Sunjzu, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi.
Kagera Sugar: Andrew Ntalla, Muganyizi Martin, David Charles, Freeman Nesta, Sunday Frank, Geoprge Kavilla, Shija Mkina/Themi Felix (dk.46), Daudi Jumanne/Juma Mpola (dk. 86), Saidi Dilunga/Mike Katende (dk. 51), Yona Ndabila na Paul Ngwai.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment