ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 28, 2012

Mali yasimamishwa uanachama-BBC


Jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS imesimamisha uanachama wa Mali kuafuatia hatua ya jeshi kuoindua serikali ya Rais Amadou Toumani Toure .
Viongozi wa Jumuiya hiyo walifikia uamuzi huo katika mkutano uliofanyika nchini Ivory Coast.

Sasa viongozi hao kutoka nchi sita wanachama wa ECOWAS wamepanga kusafiri hadi mjini Bamako Mali ili kukutana na baraza kuu la jeshi linalotawala nchi hiyo.
Akihutubia waandishi wa habari baada ya mkutano huo Rais wa Ivory Coast, alisema Amadou Toumani Toure bado yuko hai na yuko katika hali njema .

Kiongozi huyu wa Ivory aliongezea kuwa alizungumza na Toure saa chache kabla ya mkutano wao kuanza.
Na kwa wale waliohusika na kumwangusha madarakani rais wa Mali, ECOWAS imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kusitisha uanachama wao katika chombo hiki, kulaani mapinduzi hayo ya kijeshi na kutishia kuiwekea vikwazo nchi hiyo iwapo viongozi wapya wa kijeshi hawatarejesha utawala wa katiba.
Nae mwenyekiti mpya wa Tume ya ECOWAS, Kadre Desire Ouedraogo, ametoa wito wa kuachiliwa huru kwa wafungwa wa kisiasa na kumchagua Rais Blaise Compaore wa Burkina Faso kuwa msuluhishi wao.
"Mkutano huu unaidhinisha kuyapa uwezo majeshi ya akiba ya ECOWAS kujiandaa kwa kila tukio.
Endapo kutatokea kutoheshimu maamuzi ya CNRDR, mkutano unawaagiza wanachama wote kuweka mara moja vikwazo vya usafiri na kidiplomasia na fedha dhidi ya watawala hao wa kijeshi na marafiki zao,” Desire-Ouedraogo alitangaza "
Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara anatarajiwa kuongoza ujumbe wa viongozi sita wa nchi za Afrika Magharibi kwenda Mali kukutana na viongozi wa kijeshi.
Rais Ouattara pia amesema viongozi hao wa kijeshi wamekwisha taarifiwa kuhusu msimamo wa ECOWAS.
Rais wa Ivory Coast amesema kwa wakati huu, mazungumzo yanahitajika zaidi katika kutatua mgogoro wa kikatiba nchini Mali, lakini amesema hawatasita kutumia njia nyingine zote mbadala iwapo hii itashindikana.
Kikundi cha viongozi wa kijeshi wa kanda hiyo pia nao wamepanga kwenda Bamako kuwashauri viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, lakini pia kuweka wazi namna ECOWAS itakavyosaidia kukabiliana na mashambulio ya waasi kaskazini mwa nchi ya Mali.

No comments: