Ila sitamuachia jimbo mtu anayechekacheka
Kimsingi nilikuwa nimekufa, Mungu akaniokoa
Awaelezea kwa kina Wanakyela ugonjwa wake
Mbunge wa Kyela na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amewasili jimboni kwake jana na kutoa kauli nzito kuhusu ubunge wake.
Dk. Mwakyembe ambaye amekuwa nje ya jimbo lake kwa zaidi ya miezi saba kutokana na kuugua ugonjwa unaodaiwa kuwa umetokana na sumu na kwenda kutibiwa nchini India, alisema kama ataona vita vya ubunge ni vikubwa sana atachukua hatua ya kuachia ngazi nafasi hiyo.
Akiwa katika kijiji cha Sanu mpakani mwa Wilaya ya Rungwe na Kyela, Dk Mwakyembe alipokelewa na mamia ya wananchi, magari zaidi ya 30, pikipiki zaidi 60, huku wakiwa na mabango yaliyoandikwa “Mwakyembe endeleza mapambano dhidi ya ufisadi tupo nyuma yako”, “Mwakyembe na Mwandosya poleni sana Mungu atawajali mtapona”.
Akifafanua juu ya kauli yake hiyo, alisema hali anayoiona hivi sasa katika jimbo hilo ni watu kupigiana majungu na fitina na kwamba kama vita hivyo vikizidi ataachia ngazi.
Hata hivyo, alisema hatakubali kuachia ngazi mpaka atakapohakikisha kuwa amepatikana mtu makini wa kuliongoza jimbo hilo na sio mtu wa kuchekacheka.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa kata ya Ipinda, alisema katika kipindi cha miaka minne kilichobaki wananchi wa Kyela waachane na siasa za fitina na kutokubali kutumiwa na watu ambao sio wazaliwa wa Kyela kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
‘Kipindi tulichobaki nacho ni cha miaka minne tushikamane, tuweke pembeni siasa za fitina, tusikubali kutumiwa na watu ambao sio wana Kyela hawana uchungu na Kyela, kama ni ubunge mimi naomba niwaapie na wazazi wangu wapo hapa wazee, mimi nikiona vita vya ubunge ni vikubwa sana nitawaachia,” alisema Mwakyembe.
Akielezea kuugua kwake, alisema kimsingi alikuwa amekufa lakini Mungu amemrejesha ili aendeleze mapambano ya kupigania maslahi ya taifa bila woga wala kigugumizi kwa manufaa ya Watanzani wote.
“Naamini Mungu amenirudisha, ndugu zangu nilikuwa nimekufa, nikisema hivi watu mnasikitika, naamini kwamba Mungu hajanirudisha ili niwe mume bora kwa huyu mama (Mke wake), hata….wala hajanirudisha ili watoto wangu waendelee kuwa na baba,..hapana, nadhani Mungu anajua changamoto tulizonazo kama taifa, wilaya na anataka hizi changamoto sisi tuliopewa hizi nafasi, tuzivalie njuga bila kuogopa bila kigugumizi, “ alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema wilaya ya Kyela mara kwa mara ni kitovu cha mabadiliko ya kisiasa na mwalimu siasa nchi hii na ndiyo maana hata katika mapokezi yake wamehudhuria pia viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani.
Alisema kitendo kilichofanywa na viongozi wa vyama vya siasa ni uzalendo na tabia ambayo inapaswa kuigwa na kila mtu kwani lazima wanasiasa watambue kuwa siasa haziwezi kutugawa wananchi na Watanzania kwa ujumla.
Alisema hakubaliani na watu wanaosema chama kwanza kwani anavyofahamu utaifa kwanza chama baadaye.
“Mimi sikubalini na mtu yeyoye anayesema kitu cha kwanza ni chama chako,…hapana, mimi kitu cha kwanza kwangu siyo CCM, cha kwanza mimi ni Mtanzania, cha pili ndiyo tunaingia kwenye vyama,….mtu anayekimbilia chama kuwa cha kwanza hivi hicho chama kingetokea wapi kama siyo taifa,” alisema Dk.Mwakyembe.
Aliongeza kuwa ugonjwa unaomsumbua hajawahi kumweleza mtu yeyote lakini ni ugonjwa adimu ambao sio wa kawaida sana ambao umekuwa ukimtesa tokea mwezi wa Mei mwaka jana hadi Agosti, mwaka jana hali ipozidi kuwa mbaya.
Alisema alipokwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alielezwa na madaktari kwamba alikuwa anasumbuliwa na kisukari ambapo wakati huo hali iliendelea kuwa mbaya huku nywele zikinyofoka, kope na mifupa ikawa inapinda.
Aliongeza kuwa wakati akiendelea kuugua daktari mmoja (hakumtaja jina), alimweleza kuwa ugonjwa unaomsumbua siyo wa kisukari bali alikuwa ameathirika na sumu katika chakula (food poison) jambo ambalo lilizidi kumchanganya na kushindwa kuelewa anaumwa ugonjwa gani.
Alisema ilikuwa kila sehemu anapokaa ngozi inanyofoka na alipokwenda India, serikali ya nchi hiyo iliposikia kuna waziri anaumwa alipelekewa daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi ambaye alimhakikishia kuwa atapona baada ya wiki mbili na kuruhusiwa kurejea Tanzania.’
“Wiki mbili zilipopita daktari aliyekuwa akinitibu alipokuja kunipa dawa alikuta nimevimba mwili mzima, mwili unapasuka, nimepukutika mwili mzima, daktari akaniangalia akasema anafuta maelezo yake ya awali kwamba atapona haraka huu ugonjwa ni mgumu., baadaye walianza kunipima damu kupeleka kila hospitali pamoja na kunitoa nyama mgongoni na mfupa kwa ajili kufanya uchunguzi wa kitaalam zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa ugonjwa huo unaomsumbua umemuathiri sana kwani siku ya tatu daktari aliyekuwa anamtibu alipokwenda hospitalini alienda akiwa na uzi mwekundu mkono wa kushoto ambapo kijana mmoja wa Kihindu “akaniambia huyu daktari ameanza kuomba Mungu upone” maana hata heshima yake imeanza kushuka kwani fani yake inaweza kupotea kwa kushindwa kunitibu.
Aliongea kuwa kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo ndiyo maana hata Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alikuwa akiongea kwa hasira akishinikiza jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa ugonjwa unaomsumbua kwani alifahamu kuwa kulikuwa na dalili zote za kwamba amelishwa sumu.
“Madaktari walivyoendelea kupima wakasema huu ni ugonjwa mpya ambao bado wanasayansi hawajajua unatokana na nini, Sitta akasema basi huu ni ugonjwa wa kutengeneza, na ndiyo maana hakueleweka na vyombo vya habari vya mafisadi alipoidai polisi kufanya uchunguzi wa kina kwa sababu anasema dalili zote za sumu zinaonekana sasa chunguzeni siyo kwamba anasema kuna sumu hapana,” alisema Dk. Mwakyembe.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema kata ya Ipinda, Sadati Mwambungu, alisema Chadema itaendelea kumpigania Dk. Mwakyembe kwa sababu mambo anayoyapigania ya mafisadi ndiyo ambayo pia yanapigiwa kelele na chama hicho.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment