ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 31, 2012

Oil Com yalipishwa mil 30/- kwa uchafuzi wa bahari

Kampuni ya mafuta ya  Oil Com imelipa fidia ya Sh 30 milioni kwa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kudaiwa kusafirishaji  maji machafu yenye kemikali baharini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwanasheria wa NEMC, Manchare Suguta, wakati alipokuwa akifanya ziara ya ukaguzi katika kampuni hiyo kwa ajili ya kuangalia kama wametekeleza yale waliyotakiwa kuyafanyia kazi.
Alisema kuwa juzi waliizuia kampuni hiyo kutoa huduma kwa muda mpaka hapo watakaporekebisha tatizo hilo la kusafirisha maji ambayo yanaweza kuharibu shughuli za bahari kwa kuwa wanasafirisha maji ambayo hayatakiwi.
Suguta alisema kutokana na jambo hilo waliitaka mara moja kampuni hiyo kulishughulikia tatizo hilo na kutakiwa kulipa faini ya Sh 30 milion kutokana na uchafuzi wa mazingira.
Alisema kampuni hiyo ilivyopatiwa taarifa hizo ilishughulikia jambo hilo kwa muda mfupi na kwenda kulipa faini hiyo mara moja na kwa sasa inaendelea na kazi zake.
Hata hivyo, alisema NEMC iliwataka wazuie umwajikaji wa maji  yao kwenda baharini ili uchafuzi usiendelee.

Alisema yale maagizo waliyotakiwa kuyatekeleza wameyafanyia kazi kwa kiasi kikubwa na kwamba wanaendelee kufanyia kazi yale waliyotakiwa kwani watakuwa wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Alitoa wito kwa watanzania kuhakikisha kuwa wanalinda mazingira kwani hawapo tayari kuvumilia uchafuzi na faini zitaendelea kwa wale watakaokiuka taratibu za kisheria.
Naye, Meneja wa Ujenzi wa Kampuni hiyo, Badi Twaah, alisema kuwa juzi walikuwa wanafanya usafi mkubwa hali ambayo ilipelekea kwa maji kumwagika na kwamba hayakuwa na kemikali kama ilivyosemwa.
Alisema chemba ambayo ilijaa maji wameifanyia marekebisha na kwa sasa haisafirishi maji kuelekea baharini na wametekeleza yale waliyotakiwa kufanya na NEMC.
Wakati huo huo, Suguta alisema kuwa kwa sasa NEMC inajipanga kuichukulia hatua kali Kampuni ya Chemi and Cotex Industries LTD  kwa kitendo cha kukiuka maagizo ya NEMC.
CHANZO: NIPASHE

No comments: