Waziri Magufuli ameutaka wakala huo kuwaandikia barua watu hao kuwataka walipe fedha hizo ndani ya wiki moja, vingimevyo watapokonywa nyumba hizo.
Aidha, Waziri Magufuli ameahidi kwamba kuanzia leo, atawasiliana na uongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi kupata wapelelezi watakaohusika na uchunguzi kuwabaini wanaopokea rushwa katika vituo vya mizani ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa idara mbalimbali za wizara hiyo, ikiwemo TBA, Wakala wa Barabara (Tanroads) na Idara ya Ujenzi, ambapo alitolea mfano kwa Mkoa wa Morogoro kwa kusema kuwa kati ya waliouziwa nyumba hizo, asilimia 54 wamelipa huku asilimia 45 wakishindwa kulipa hadi sasa.
Alisema wakala huo umeshindwa kufikia malengo ya kujenga nyumba 10,000 za watumishi wa Serikali, badala yake zimejengwa nyumba 1,043 tu hadi sasa, huku mkoani Morogoro wakijenga nyumba moja tu tena wilayani Mvomero.
“Serikali ilitaka iuze nyumba hizo ili ipate fedha za kujenga na kuuza nyumba nyingine, lakini hawa wachache wanatukwamisha, nasema agizo hili ni kwa nchi nzima, waandikiwe barua, ndani ya siku saba wawe wamelipa madeni yao, ama sivyo wapokonywe nyumba hizo, hawawezi kuishi kwa jasho la wenzao,” alisema Dk. Magufuli.
Dk. Magufuli pia alizingumzia mizani kwa kusema kuwa anashangazwa na ongezeko la makosa ya uzidishaji mizigo kwenye mizani, huku faini iliyopatikana kwa mwaka huu ikiwa ni ndogo kulinganisha na ongezeko la makosa hayo.
“Mfano, kwa mwaka huu zimepatikana Shilingi bilioni tatu tu kutokana na makosa hayo ya uzidishaji mizigo kwenye mizani, fedha hizi ni ndogo ikilinganishwa na bajeti inayotolewa kuendeshea vituo vya mizani, ambapo kwa mwaka huu pekee Serikali imetenga Shilingi bilioni nne kuhudumia vituo hivyo,” alisema Waziri Magufuli.
Kuhusu watumishi wa wizara hiyo waliolalamikia kukoseshwa fursa za kujiendeleza, alisema wizara imelenga kuajiri wataalamu waliosoma na wenye sifa ili wafanye kazi zao vizuri.
“Kama ulifeli unataka fedha za matengenezo ya barabara ndio zitumike kukusomesha wewe, no way (hakuna namna), fedha za Tanroads ni kwa ajili ya matendegenezo ya barabara, kama unataka kujiendeleza nenda Wizara ya Elimu, sisi tunataka tuwalipe vizuri sana ili mfanye kazi sana. Training (mafunzo) ya kawaida ni sawa, lakini pia mkiimarisha Tanroads mtaweza kupata hizo fursa za kujiendeleza,” alisema.
Baadhi ya watumishi wa wizara hiyo akiwemo Meneja wa kituo cha Mizani cha Kihonda, waliiomba Serikali kupitia upya sera na sheria zinazohusika na vituo vya mizani ili kurekebisha dosari kadhaa zinazoonekana kujitokeza wakati wa kutoza faini, hali inayofanya baadhi ya magari yanayozidisha uzito kwa namna mbalimbali za ujanja ujanja kuharibu barabara.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara, Dk. David Wanyancha, aliahidi kupambana na watendaji watakaobainika kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za barabara na kuongeza kuwa hivi sasa wamejipanga ziwe zinafikia halmashauri na Tanroads kwa asilimia mia moja.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga, aliahidi kuwa watahakikisha ujenzi wa nyumba 10,000 unafikiwa.
Uuzaji wa nyumba za serikali kwa watumishi wa umma kwa bei ya kutupa ni moja ya malalamiko yanayoendelea kutolewa dhidi ya Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment