ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 17, 2012

Nani anasema penzi bila fedha ni uhusiano butu?-2

 KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya, niliuliza: Je, unayo imani kwamba tatizo la fedha linaweza kuharibu muungano wako wa kimahaba na mwenzio? Inawezekana lakini siyo kihivyo!
Kwa migogoro yote ya fedha uliyonayo leo, haitofautiani na ile ambayo itakufika siku za usoni au mbeleni. Maumivu ni ya wawili, ni vizuri kuvumiliana, kushikamana ili kuvuka vizingiti.

Kitu muhimu cha kufanya ni kushirikiana, kuepuka kugeukana na kucheza mchezo wa lawama. Huyu amuone mwenzake ndiyo chanzo cha tatizo. Zingatio ni kwamba mapenzi yakishamiri,  kwa kiasi fulani hupunguza mawazo yanayosababishwa na ukata.
Hali imekuwa mbaya, ni sawa ila zingatia kuwa vyovyote mnavyojikuta mpo kwenye mazingira tata kiuchumi, mnapaswa kushirikiana mpaka pale yatakaponyooka. Hii inajumlisha kupanga bajeti ya vitu na kujibana kuliko mwanzo, pia kujitahidi kutafuta bidhaa za gharama nafuu, yote hiyo ni ili mfurahie maisha licha ya ukata unaowakabili.
Kushirikiana katika kutafuta vitu vyenye sura ya kimahaba, kutoka ‘out’ kwenye maeneo ambayo hayagharimu fedha nyingi, ni muhimu mno katika kuweka hai uhusiano wako, pale unapobeba tafsiri ya “mambo magumu.”
Ni aibu kizuizi cha fedha kusababisha mtengane. Ni muhumi mambo ya fedha yakapata kujadiliwa pamoja. Ila mtikisiko huo hauruhusiwi kuwafanya muwe wazembe kujenga penzi endelevu. Ikitokea ni dhambi kubwa! Hamna fedha, lakini yapo mambo ambayo mkiyafanya mtafurahi, ingawa hayatagusa mfuko wa yeyote kati yenu.
Mfano, kukaa nyumbani na kuangalia muvi nzuri itawagharimu kiasi gani? Fikiria kwamba wewe na yeye mmeketi vizuri kitini sebuleni, mnazungumza mambo yenye kuleta mwanga wa kimaisha, huku matukio ya filamu yakiteka hisia zenu.
Maisha yametofautiana, inawezekana ‘cha kuonea’ hakipo nyumbani, lakini hiyo siyo ishu! Kila mtu anahitaji kupewa elimu ya mapenzi, iwe mjini au kijijini. Kwa maana hiyo, anaweza kuketi faragha na mwenzi wake na kusimuliana hadithi za kimapenzi.
Yapo mazingira mazuri yenye hewa safi, fukwe mbalimbali, bustani na kadhalika. Yote hayo ni maeneo ambayo unapaswa kuyatumia na mwenzi wako kuhakikisha furaha haipotei. Lingine ambalo linaweza kufanyika bila kuwagharimu kutoboka mifuko ni kupika chakula kizuri cha usiku ambacho kitakupendeza wewe na mwenzi wako.
Furaha kidogo huyeyusha maudhi na msongo wa mawazo! Kula ‘msosi’ mtamu, kuchombezana kwa hadithi za hapa na pale ni kitu maalum sana. Inawezekana pia, kutoka ‘out’ na kwenda kujumuika pamoja kiwanja tulivu, kupata ‘dinner’ pamoja, huku mkiburudishwa na muziki laini.
Kuna mambo mengi ya kufanya, ila pointi ya msingi ni kuwa makini na uhusiano wako na kuhakikisha huyumbishwi na matatizo ya kifedha. Hustahili kuchachawa, kuna wakati wa kupigana kwa ajili ya fedha lakini pia kipo kipindi cha kudumisha penzi.
Hisia zako kwenye fedha na mapenzi ni muhimu lakini si busara kuchanganya moja kwa lingine. Katika kukamilisha furaha yako ya kimapenzi wakati mambo ya kifedha yanapokwenda segemnege, hapa chini kuna pointi za kuzingatia.
Mlikuwa na hisia gani wakati mlipojikuta mnaangukia kwenye sayari ya kimapenzi kwa mara ya kwanza? Ukipata jibu, basi nakukumbusha kuheshimu mlipotoka! Mlipendana na kila mmoja akili yake ilielekea kwenye mapenzi, hivyo ndivyo mnavyotakiwa kuwa siku zote. Iwe kwenye shida na raha!
 * Kumbuka jinsi mlivyokuwa mnasaidiana kipindi kile mambo yanakwenda murua. Ni muda sasa kushirikiana wakati wa harakati za kutafuta ‘ankara’, pale uchumi unapokuwa mgumu.
* Zingatia kuwa inahitaji wawili wanaopendana ili kuyafanya maisha yawe safi, pia kupitia kwao, sukari inaweza kugeuka shubiri. Mkiishi kama timu moja ni ufunguo wa kufanikiwa kwenye njia zote.
* Siku zote fungueni masikio na msikilizane hata kama huwa hamkubaliani. Kupuuza kitu alichosema mwenzako, kulaumiana au kufunga mjadala wakati mwenzako anachangia ni kosa.
Aidha, kutaka matatizo yako uyajadili wewe mwenyewe, ilhali naye angependa apewe fursa ya kutoa mchango wake, haiwezi kukusaidia matatizo yatoweke, badala yake, inawezekana hali ikawa mbaya zaidi.
* Zingatia yote hayo, pia muwe na utaratibu kwamba mnapokutana kila mmoja anaweka mezani mpango wake wa kukabiliana na mtikisiko wa kiuchumi, na kuheshimiana.
Watu wanasema penzi bila fedha ni uhusiano butu? Yaani hauna makali! Upande mmoja naamini kwa sababu nimeona na ninaendelea kushuhudia lakini maandishi haya yakizingatiwa, thamani ya penzi itabaki kusimama katika kipimo chake.

www.globalpublishers.info

No comments: