ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 5, 2012

Nkya kuwajibu madaktari leo

NAIBU Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya 

NAIBU Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya amesema atatoa tamko lake leo kujibu tishio la madaktari nchini la kugoma iwapo Naibu Waziri huyo na Waziri Hadji Mponda hawatajiuzulu. 

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana Dk. Nkya, alisema yupo kijijini ambako hakuna redio wala magazeti, hivyo asingeweza kuzungumza jambo lolote kuhusu tishio hilo la mgomo mpya wa madaktari.
 

“Nitarejea Dar es Salaam kesho (leo) na kufuatilia taarifa hizo za madaktari mstari hadi mstari, ili nitoe majibu yenye usahihi. Kwa sasa sina chakusema kwa kuwa sijasikia lolote kuwahusu. 

Nipo kijijini kabisa huku, hakuna redio wala magazeti. Nitafute kesho (leo),” alisema Dk. Nkya. 
Madaktari mwishoni mwa wiki waliipa Serikali siku tatu mpaka kesho kutwa kuwaondoa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Dk. Nkya la sivyo watagoma. 

Kwa upande wa Waziri Mponda alipotafutwa na gazeti hili kutoa kauli kuhusiana na tishio hilo la madaktari, hakupatikana kufuatia simu yake ya mkononi kuzimwa. 

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Kinondoni, Emmanuel Makene alisema kitendo cha madaktari hao kuipa Serikali muda wa mwisho wa kutatua matatizo yao sio cha kiungwana kwa kuwa ilikwishayapatia ufumbuzi baadhi, na inahitaji muda zaidi wa kushughulikia mengine. 

Makene ambaye pia ni wakili wa kujitegemea alisema, kitendo cha madaktari hao kuitaka Serikali iwafukuze kazi Waziri na Naibu wake , kinaonesha udhaifu wa kimaadili katika taaluma hiyo kwa sababu mgomo wanaotaka kuufanya una madhara kwa wagonjwa na wala sio wanasiasa hao wanaowatuhumu. 

Alifafanua kuwa Dk. Mponda na Dk. Nkya ni wanasiasa ambao wanashauriwa na watendaji wakuu kwenye maeneo yao ya kazi ambao hata hivyo waliondolewa kutokana na madaktari hao kueleza kuwa ndio walikuwa tatizo na chanzo cha mgomo wa awali. 

“Sasa nashindwa kuwaelewa madaktari wetu hawa, walisema tatizo ni Katibu Mkuu (Blandina Nyoni) na Mganga Mkuu wa Serikali (Deo Mtasiwa) na wakaondolewa kwenye nafasi zao muda mfupi baada ya mvutano. 

Sasa watendaji wale hawapo wanasema na hawa wanasiasa nao waondolewe, la sivyo watagoma tena Jumatano.


Habari Leo

No comments: