ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 28, 2012

Polisi akutwa na bangi disko-Habari Leo

SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuagiza maaskari wanaokiuka maadili ya Jeshi la Polisi na kulipaka matope kuchukuliwa hatua ikiwamo kufukuzwa kazi, polisi mkoani Kilimanjaro amekamatwa akidaiwa kufanya vurugu disko huku akiwa na misokoto minne ya bangi. 

Katika tukio hilo, polisi huyo wa kituo cha Majengo mjini hapa, G842 Konstebo Deogratius, anashikiliwa na Polisi baada ya kufanya fujo katika ukumbi wa disko wa Pub Alberto. 

Akithibitisha jana kukamatwa kwa askari huyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Absalom Mwakyoma, alisema askari huyo alikutwa akifanya vurugu Jumamosi saa mbili usiku ukumbini humo. Mwakyoma alidai askari huyo alikwenda hapo kunywa pombe na kucheza muziki na wakati muziki unaendelea, mlinzi wa eneo hilo alipewa taarifa na wateja kuwa kuna mmoja wa wachezaji anawafanyia fujo. 

Alidai kuwa mlinzi huyo aliyejulikana kwa jina la Rajab Hamad alipokwenda na kumtuliza askari huyo, aling’atwa mkononi, ndipo mmiliki wa ukumbi huo, Christopher Shayo ‘Chris Burger’ alipotaka kujua kulikoni na kuambulia ngumi ya usoni kutoka kwa askari huyo. 

Kamanda aliongeza kuwa baada ya vurugu hizo, askari walifika eneo la tukio na kumkamata askari huyo ambaye alipekuliwa, na kukutwa na misokoto hiyo ya bangi mfukoni. Alisema mtuhumiwa aliwekwa mahabusu wakati upelelezi ukiendelea na hatua nyingine za kinidhamu dhidi yake zitafuata. 

Aliongeza kuwa watu wote walioshambuliwa ikiwa ni pamoja na mmiliki wa ukumbi huo na walinzi wake wawili walipewa fomu ya matibabu ya PF3 na kwenda kutibiwa hospitalini na hali zao zinaendelea vizuri. 

Matukio ya askari kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya Jeshi hilo, vimeonekana kushika kasi mkoani humo. Hili ni tukio la pili katika miezi michache ya mwaka huu baada ya lile la askari mwingine kuingia ukumbi huo akiwa na bunduki aina ya SMG na kuwafanyia watu fujo.

1 comment:

Anonymous said...

Sio huko tu hapa njombe wao ndio wababe wa baa zote