ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 31, 2012

SMZ kujenga gereza la kisasa Unguja

KATIKA kuhakikisha inapunguza msongamano kwa wafungwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kujenga gereza jipya la kisasa lenye uwezo wa kuchukua wafungwa wengi kwa wakati mmoja na kuondosha msongamano uliopo sasa. 

Hatua hizo zinakwenda sambamba na mikakati ya kuimarisha dhana ya utawala bora na haki za binaadamu ambayo inasisitiza suala la kuimarisha mazingira bora ya wafungwa magerezani. 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Sheria na Katiba, Abubakar Khamis Bakari wakati akijibu swali aliloulizwa na mwakilishi wa Jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub (CCM) aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya kuondoa msongamano wa wafungwa katika magereza yake. 

Abubakar alifafanua na kusema kwamba tayari Serikali imeanza kazi ya kutafuta kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa gereza hilo huko Hanyegwa Mchana, wilaya ya kati mkoa wa kusini Unguja.
 

Alisema gereza hilo litakapomalizika ujenzi wake litakuwa na nafasi kubwa ya kuchukuwa watuhumiwa na wafungwa wengi kwa wakati mmoja na kuondoa tatizo la msongamano lililopo katika magereza ya Unguja na Pemba. 

“Nakubaliana na mheshimiwa kuhusu suala la kuwepo kwa msongamano wa wafungwa na mahabusu katika magereza yetu ya Unguja na Pemba...mipango ya kujenga gereza jipya kwa sasa imekamilika na tunatarajia kupata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi,” alisema Abubakar. 

Hivi karibuni, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu alifanya ziara katika Magereza mbali mbali ya Unguja na kukagua sehemu ya kiwanja cha gereza jipya huko Hanyengwa Mchana wilaya ya kati Unguja. 

Makungu alisema kumalizika kwa ujenzi wa gereza hilo jipya litaondosha moja kwa moja msongamano wa wafungwa na mahabusu lililopo sasa huku akitaka kuwepo kwa kuharakisha kusikilizwa kwa kesi za watuhumiwa mbalimbali.


Habari Leo

No comments: