ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 31, 2012

Yanga, Coastal hapatoshi, Simba kwa Lyon usipime

Hamis Kiiza,Yanga
Sosthenes Nyoni, Tanga
'MSHIKE mshike...na asiye na mwana...' kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, ambapo mabingwa watetezi Yanga watakakuwa wageni wa Coastal Union, huku vinara wa ligi Simba wakiwa na kazi mbele ya African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania, timu za Simba na Yanga  watashuka dimbani wakiwa na malengo tofauti kila mmoja, Yanga wenyewe wanajua kupoteza mchezo huo ni kupoteza ndoto yao ya kutetea ubingwa wao huku Simba wakitaka ushindi wajiimarishe kileleni kabla ya kuelekea Algeria kuivaa ES Setif.

Yanga hivi sasa inashikilia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43, hivyo ushindi dhidi ya Coastal utasaidia kupunguza pengo kati yake na kinara Simba inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 47, pia kuiondoa Azam FC katika nafasi ya pili ambayo ina pointi 44 kabla ya mechi yake ya kesho dhidi ya Ruvu JKT.

Ukweli ni kwamba uzito wa mechi kati ya Yanga na Coastal Union unazidishwa na taswira tofauti za timu zote mbili hivi sasa pamoja na uwepo wa kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio'. 

Mabingwa hao wa mwaka 1988, Coastal Union waliojikusanyia pointi 29 baada ya kuzinduka na kushinda mechi sita mfululizo za raundi ya pili wenyewe wanatarajiwa kuendeleza rekodi hiyo kwa kusaka pointi tatu zitakazoipandisha juu kutoka katika nafasi ya sita iliyojiweka mpaka sasa. 

Kocha wa Coastal,  Kihwelo 'Julio' ameapa kuwadharirisha wapinzani wake kwenye mchezo huo akitarajiwa kuwatumia nyota kama Benard Mwalala, Edwin Mukenya kufikia malengo yake ingawa pia yupo Aziz Gilla anayecheza hapo kwa mkopo akitokea Simba.

Naye kocha wa Yanga, Kostadin Papic bila shaka ataingiza timu uwanjani akiwa katika hali ya kujiamini baada ya nyota wake waliokuwa kifungoni kufunguliwa kwa muda hivyo itakuwa ni hiyari yake kuwatumia au la.

Silaha za Papic zinazoweza kuonekana leo baada ya kunasuliwa kwa muda kutoka katika kifungo cha Kamati ya Ligi kutokana na utovu wa nidhamu ni mabeki, Nadir Haroub na mwenzake Stephano Mwasika, pamoja na viungo Omega Seme, Nurdin Bakari na mshambuliaji Jerryson Tegete.

Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Rashid Msangi wa Dodoma ambaye atasaidiwa na Rashid Lwena (Ruvuma) na Issa Malimali (Ruvuma).

Vita nyingine itakuwa jijini Dar es Salaam, wakati vinara wa ligi Simba wakiwa kwenye kiwango bora zaidi watakapowakabili ndugu zao African Lyon.

Kocha Milovan Cirkovic amewasisitizia wachezaji wake kutofanya uzembe utakaotoa nafasi kwa wapinzani wao ili kujiweka vizuri kabla ya kuivaa ES Setif wiki ijayo.

Simba itashuka dimbani bila ya kiungo wake Patrick Mafisango aliyesimamishwa na uongozi kutokana na utovu wa nidhamu.

Hata hivyo, Cirkovic licha ya kuwa na akiba ya kutosha ya wachezaji mahiri pia atakuwa na furaha baada ya kurejea kwa beki aliyekuwa majeruhi Juma Jabu.

Kesho matajiri wa Chamazi, Azam watakuwa wenyeji wa Ruvu JKT timu iliyopoteza makali yake katika siku za hivi karibuni.


Mwananchi

No comments: