ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 23, 2012

Tume yaongeza wapiga kura Arumeru

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza idadi mpya ya wapiga kura katika Jimbo la Arumeru Mashariki. Sambamba na hatua hiyo, NEC pia imebaini kwamba zaidi ya nusu ya wapiga kura waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu hawajui tarehe za kuzaliwa kwao na kusababisha kuwapo taarifa tofauti. 

Aidha, Tume hiyo pia imesema kuwa hakuna vituo bandia vya kupiga kura kama ilivyodaiwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa. 

Akitangaza jana ongezeko hilo la wapiga kura, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema hatua hiyo inatokana na waliosahaulika kuorodheshwa ili waweze kupata fursa ya kupiga kura Aprili mosi. 

Kwa hatua hiyo, wapiga kura sasa watakuwa 127,455 badala ya idadi iliyokuwapo mwanzo ya wapiga kura 127,429 kama ilivyokuwa katika Daftari katika uchaguzi wa mwaka juzi. 


Kwa maelezo ya Jaji Lubuva, marekebisho yaliyofanyika ni pamoja na kuingiza majina ya wapiga kura 54, ambao kwa sababu mbalimbali, hawakuorodheshwa katika Daftari hilo. 

Akitaja sababu hizo, Jaji Lubuva alisema ni pamoja na uwepo wa zaidi ya nusu ya wapiga kura waliojiandikisha Arumeru Mashariki wasiojua tarehe zao za kuzaliwa, jambo lililochangia mpiga kura mmoja kuandikwa zaidi ya mara moja akiwa na umri tofauti. 

“Tume imebaini uwepo wa wapiga kura 28 waliojitokeza zaidi ya mara moja katika Daftari lililotumika mwaka juzi lakini, tumerekebisha kasoro hiyo na kuchapisha Daftari lenye maboresho,” alisema Jaji Lubuva. 

“Kwa maana hiyo, kutakuwa na idadi ya wapiga kura 26 watakaoongezeka katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki, mwezi ujao,” alisema Jaji Lubuva. Akijibu swali la waandishi wa habari Dar es Salaam, Kamishna wa NEC, Jaji John Mkwawa, alisema hakuna kituo bandia na wala havitakuwepo. 

Kwa sasa vituo vya kupiga kura katika jimbo hilo ni 327. Hata hivyo alifafanua kuwa kama ikitokea dharura, kuna uwezekano wa kuhamisha kituo kutoka sehemu moja kwenda nyingine au kuongeza kituo. 

Alifafanua kuwa uhamishaji huo au uongezaji wa vituo hufanyika baada ya kutaarifu wahusika wote katika uchaguzi vikiwamo vyama vya siasa na mabadiliko hayo hayawezi kuitwa vituo bandia. 

Daftari nchi nzima Katika hatua nyingine, Jaji Lubuva alisema NEC imeanza maandalizi ya kuboresha Daftari hilo nchi nzima na kwamba ifikapo mwaka 2015, kazi hiyo itakuwa imekamilika. “Tunafanya hivyo ili kuondoa kasoro zilizojitokeza katika maeneo yote nchini. 

Ni imani yetu kuwa kazi hiyo itakamilika kabla ya siku ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema. Uchaguzi wa amani Wakati huo huo, NEC imeonya watakaosababisha uchaguzi huo mdogo kuvurugika na kusema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. 

“Uchaguzi wa amani na utulivu ndiyo demokrasia, nawasihi wapigakura na wana vyama vya siasa watakaoshiriki, kuhakikisha amani inatawala siku hiyo kwa sababu ina umuhimu mkubwa,” alisema na kuongeza kuwa vyombo vya usalama vitakuwa katika vituo vyote.

No comments: