ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 3, 2012

Ufuta:Mpiga solo Cuban Marimba aliyegeukia ufundi baiskeli

Image
Dk. Joackim Ufuta akikumbushia enzi zake za upigaji gitaa la solo.
KWA wakazi wa Morogoro, eneo la Masika ni miongoni mwa maeneo muhimu na maarufu kwa watu wake kujihusisha na shughuli mbalimbali za kujipatia riziki, ni sehemu yenye maskani ya makundi mbalimbali ya watu kuanzia kituo kidogo cha daladala, taksi , ukodishaji na utengenezaji wa baiskeli, mafundi viatu na wauzaji wa magazeti. 


Katika pitapita zangu eneo hilo na kukutana na jamaa yangu mmoja akiwa kwenye maskani 
yake, na jambo la kwanza ananinong’oneza kuhusu mwanamuziki wa zamani wa Cuban Marimba, aliyemtaja kwa jina la Ufuta, mpiga solo wa bendi ya Cuban Marimba kuwa ni miongoni mwa wenye kuhangaika kujitafutia riziki eneo hilo. 

Bila ajizi niliamua kumfuata mwanamuziki huyo na kukutana naye eneo hilo akiwa kwenye harakati zake za kujitafutia riziki yake ya kila siku, safari hii si ya fani ya muziki bali ni ufundi wa kutengeneza baiskeli. 

Hivyo katika makala haya, mkongwe na gwiji la upigaji wa gitaa la solo katika bendi ya Cuban Marimba na pia TK Limpopo, Joakim Simon Ufuta ( 60), anaielezea kwa kina maisha yake ya kimuziki , changamoto mbalimbali alizokutana nazo hadi kufikia kuwa fundi wa kutengeneza 
baiskeli eneo la Masika. 

Anasema Morogoro, ni kati ya mikoa michache nchini iliyokuwa ikiwika katika muziki wa dansi, lakini bendi za Mkoa wa Morogoro ndizo zilizotikisa hapa nchini na nje ya mipaka ya Tanzania pia ushindani wa ndani ya Mkoa kwa bendi ya Cuban Marimba na Super Volcano na baadaye TK Limpopo. 

Ufuta analezea historia anasema alizaliwa eneo la Utuu Misheni lililopo mjini Mahenge Wilaya ya Ulanga miaka 60 iliyopita. Anasema masuala ya muziki aliyaanza mwaka 1966 akiwa Mahenge baada ya kuanzisha bendi yake ya Taifa Jazz iliyokuwa ikitumia vifaa visivyotumia umeme na waimbaji wanne wa bendi hiyo wakiimba bila ya kutumia vipaza sauti. 

Anasema , bendi hiyo iliyokuwa ikitumia vyombo baridi iliweza kutoa burdani kwa wakazi wa Mahenge na vitongoji vyake kuanzia mwaka 1966 hadi 1968. 

Licha ya kufanya kazi kwa kutumia vyombo vya baridi, walipata mashabiki wengi iMahenge na maeneo mengine , kitendo kilichomvutia Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mahenge , aliyemtaja kwa jina moja la Ilanga kuwaahidi kuwapatia vyombo vya muziki. 

“ Huyu mheshimiwa alikuwa ni Mbunge na mkazi wa Mahenge na kila anapofika nyumbani 
alitukuta tukitumbuiza na bendi yetu…na alituahidi kutupatia vyombo vya muziki,” anasema 
Ufuta. 

Anasema, aliwanunulia vyombo na kuwaletea ambavyo ni magitaa mawili, spika na betri 
moja kwa ajili ya kutumia magitaa na vipaza sauti na spika hizo. Pamoja na hayo anasema, akiwa kiongozi wa bendi hiyo aliweza kufanya ziara katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma na Morogoro. 

Julai mwaka 1968 alishawishiwa na kaka yake aliyemtaja kwa jina la Lucas Simoni ambaye hivi 
sasa ni marehemu aachane na bendi yake ya Taifa Jazz ili ajiunge na bendi ya Cuban Marimba. 

“ Unajua kaka yangu alikuwa ni mpenzi wa bendi ya Cuban Marimba…hivyo alinishawishi 
nivunje bendi yangu ili nijiunge na Cuban Marimba , nami nikamkubalia wazo lake hilo,” 
anasema. 

Hivyo anasema , akiwa na Cuban Marimba, pamoja na Juma Kilaza, akiwa mpiga gitaa la solo, 
kila nyimbo iliyotungwa na kuimbwa na bendi hiyo mchango wake ulikuwa mkubwa katika 
kupiga gitaa hilo. 

Ufuta anasema walipokuwa Kenya mwaka 1970 kurekodi nyimbo na Cuban Marimba , 
mtaalamu wa studio ya Kenya ya kurekodi aliamua kumpachika cheo cha ‘daktari’. 

“ Nilipewa jina hilo ni kwa ajili ya upigaji wa gitaa la solo …yule mtaalamu wa kurekodi baada ya kusikiliza upigaji wangu wa gitaa la solo, muda huo huo alinipasisha kwa kunipa cheo cha 
‘daktari’ alisema mimi ni bingwa wa kupinga sindano “ anaelezea gwiji huyo. 

Anasema moja ya mafanikio yaliyopatikana na mchango wake kutambuliwa kikamilifu ndani ya Cuban Marimba ni vibao vya ‘Zena’ , ‘Shauri Yao Hao’ pamoja na Morogoro Hoyee , ni miongioni mwa ya nyimbo alizoshiriki kikamilifu kwenye upigaji wa gitaa la solo. 

Ufuta anawakumbuka wanamuziki wenzake waliowika na bendi hiyo ni pamoja na Juma 
Sangura ambaye alikuwa ni mpiga besi gitaa , Ally Said katika safu bya upigaji wa Rythmy pamoja na Pascal Sekuru ambaye ni marehemu akipiga gitaa namba mbili la Solo. 

Katika safu ya uimbaji , anawataja waliowika wakati huo na Cuban Marimba mbali na Juma Kilaza, pia walikuwemo Macelina Taitas , na Mohamed Maneti ‘ Chiriku’ ambaye sasa ni marehemu . 

Wengine waliotamba na bendi hiyo katika upigaji tumba na manyanga ni Kashinde Kulanda , 
Said Bella. “ Tulikuwa na gari letu , hivyo kundi zima lilikuwa likitembelea mikoani na watu hawa, ” anasema Ufuta. 

Anasema mwaka 1974 kulitokea kutoelewana baina ya wanamuziki wa Cuban Marimba na mmiliki wa bendi hiyo , ambao ni familia ya marehemu Salumu Abdallah , na hivyo wanamuziki watano ,yenye mwenyewe, Kilaza, Juma Sangura, Ally Said na Maneti waliihama 
bendi hiyo. 

“ TK Limpopo ilizaliwa mwaka huo wa 1974 na kuundwa na wanamuziki hawa , na hivyo kutoa 
upinzani mkali wa kimuziki Morogoro kwa kuwa na bendi tatu , Cuban Marimba, Super Volvano na TK Limpopo, “ anasema Ufuta. 

Anasema rekodi ya kwanza ya Bendi ya TK Limpopo iliyotikisa na kuitambulisha bendi hiyo 
ni wimbo wa ‘ Maisha ya Sasa’. Hata hivyo anasema, hawakukaa sana, baada ya kutokea 
kutoelewa baina ya wanamuziki kuhusu maslahi, ambapo wa kwanza kuondoka alikuwa 
Maneti. 

Anasema , kutokana na kutoelewana huko, aliamua kurejea tena Cuban Marimba mwanzoni 
mwa mwaka 1975 na alishiriki na bendi hiyo kwenye ziara za mikoani hadi nchini Kenya mwaka 1976. 

Hata hivyo anasema ,wakiwa nchini Kenya walikosana na wenzake katika mji wa Naivasha , ambapo baadhi ya wanamuziki walirudi Morogoro na vyombo vya muziki na yeye kubakia nchini humo.

Habari Leo

No comments: