ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 14, 2012

WACHEZAJI YANGA WALIVYOMFANYIA FUJO MUAMUZI



Hii ndiyo hali halisi iliyopelekea wachezaji watano wa Yanga kufungiwa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya vurugu Uwanjani wakati wa mechi yao dhidi ya Azam FC Jumamosi, Machi 10, 2012. JE, KWA MAMBO KAMA HAYA SOKA LETU LITAENDELEA KWELI? 
Video kwa hisani ya SHAFFIH DAUDA BLOG

Wakati Shirikisho la Soka nchini (TFF) likitangaza adhabu kubwa za kuwafungia wachezaji watano wa klabu ya Yanga kutokana na vurugu katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam FC wiki iliyopita, uongozi wa klabu hiyo umeibuka na kupinga vikali adhabu hizo.

Jana, TFF kupitia kwa afisa habari wake, Boniface Wambura ilitangaza kuwa Kamati ya Ligi imewafungia wachezaji, Stephano Mwasika kwa kipindi cha mwaka mmoja pamoja na kulipa faini ya Sh. milioni 1, Jerry Tegete na Nadir Haroub 'Cannavaro' (mechi sita na faini ya Sh. 500,000 kila mmoja), Nurdin Bakari na Omega Seme (mechi tatu na faini ya Sh. 500,000 kila mmoja) kutokana na kumshambulia mwamuzi wa mechi hiyo Israel Nkongo.
Akizungumza na NIPASHE, Katibu wa Yanga, Selestine Mwesigwa alisema klabu hiyo haikubaliani na maamuzi hayo ya TFF kwa kuwa mwamuzi ndiye alikuwa chanzo cha vurugu zilizotokea kwenye mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
"Bado hatujapata taarifa za kimaandishi za kufungiwa kwa wachezaji wetu, tunasubiri barua ya TFF lakini kimsingi tangu awali tulitangaza kuwa hatujakubaliana na maamuzi na hata kufungiwa huku kwa wachezaji kama unavyosema hatuwezi kukubaliana nako," alisema Mwesigwa.
Alisema kuwa pamoja na kusubiri taarifa ya maandishi ya TFF, uongozi tayari juzi uliwasilisha rufaa yao kupinga maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo Israel Nkongo ya kuwapa kadi nyekundu wachezaji Haruna Niyonzima na Cannavaro.
Katika hatua nyingine, Wambura alithibitisha kwamba TFF imepokea rufaa ya Yanga waliyoikata kupinga kadi nyekundu kwa wachezaji wao hao.
"Ni kweli Jumapili mchana tulipokea rufaa ya Yanga na rufaa hiyo itapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu, Sheria, Katiba na Hadhi ya Wachezaji kwa maamuzi zaidi," alisema Wambura.
Alifafanua kuwa rufaa hiyo ya Yanga inataka kufutwa kwa kadi nyekundu za wachezaji wao pamoja na kubatilisha matokeo ya mchezo huo ambao Yanga walilala kwa magoli 3-1.
MWAMUZI ASAFISHWA
Wakati Yanga wakidai kwamba vurugu za mechi hiyo zilisababishwa na maamuzi ya utata ya refa, Kamati ya Ligi iliyowafungia wachezaji wa Yanga imemsafisha mwamuzi Israel Nkongo aliyecheza mchezo huo.
Wambura alisema kuwa ripoti ya kamisaa wa mchezo huo haikuonyesha sehemu ambayo mwamuzi huyo alikosea au kutoka nje ya mchezo kwa maamuzi mabaya.
"Mwamuzi ameonekana alifuata sheria zote za soka kwenye mchezo ule... hivyo kamati haijamchukulia hatua yoyote na pia kamisaa wa mchezo kwenye ripoti yake ameeleza mwamuzi alikuwa sahihi," alisema Wambura.
Aidha, alisema Kamati ya Ligi imempongeza nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na mshambuliaji wa timu hiyo Hamis Kiiza kwa kuwa mstari wa mbele kuzuia wenzao kumshambulia mwamuzi. Pia imempongeza kocha Kostadin Papic wa Yanga kwa kukemea vurugu zilizofanywa na wachezaji wake.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Sikilizeni, siku zote mchawi akizidiwa kete lazima anakuwa na hasira. Mi sishangai hapa.

Anonymous said...

Huu ni upumbavu usiostahiki kutokea katika ustaarabu wa soka daraja la kwanza. Wachezaji wanabehave kama wahuni wa barabarani. Hii ni wazi kuwa hiyo adhabu wanayochukuliwa haiwatoshi na lazima itazamwe upya kwa kutoa fundisho kwa mjingamjinga mwingine yoyote kutorejea uhuni kama huu