ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 27, 2012

Wanasiasa wasusia kikao kwa kukosa posho

VIONGOZI wa vyama vya siasa wamejiengua katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya baada ya kubaini kuwa hakitakuwa na malipo ya posho kwa wajumbe wa kamati hiyo. 

Kikao hicho kilichoitishwa kwa ajili ya kupitia mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2012/13 katika halmashauri ya Manispaa ya Tabora, kilikumbwa na mtafaruku na matumizi ya lugha kali mara baada ya mwenyekiti wake, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Moshi Chang'a kutoa taarifa kuwa hakuna posho itakayolipwa kwa wajumbe. 

Alisema hali hiyo inatokana na fedha kwa ajili ya kulipa posho kwa wajumbe kutowasili na kwamba suala hilo liko mkoa mzima. 

Aliwashawishi wajumbe kuendelea na kikao kwa uzalendo badala ya kutanguliza maslahi binafsi. 

“Ndugu zangu nawaomba tuendelee na kikao ijapokuwa hatuna posho katika kikao hiki, kwani bado tuna deni la zaidi ya Sh milioni 14 katika kikao kilichopita hivyo si busara kuongeza deni," alisema Chang'a. 

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) wilaya ya Tabora, Kapasha wa Kapasha, alisema, “taarifa yako mwenyekiti tumeipokea na ombi lako tumelisikia lakini hatutaki kwa sababu posho ni haki ya kikao hiki.” 


Kapasha aliendelea kuwashawishi wajumbe kwa kusema, “wajumbe nawataka tususie kikao hiki hadi hapo malipo hayo yatakapokuwa tayari, tusikubali kuendelea na kikao”. 

Aliungwa mkono na viongozi wote wa vyama vya siasa waliohudhuria kikao hicho isipokuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema). Mwenyekiti wa chama cha Pona, Ali Mponda alisema hakuna haja ya kuendelea na kikao kama haki na stahili zao hazipo. 

“Mbona wabunge kama hakuna fedha wanaahirisha vikao,” alihoji Mponda. Pia Mwenyekiti wa NLD, Anatory Katabwa, aliunga mkono kwa kusema, “jamani hakuna haja ya kuendelea na kikao kama stahili za wajumbe wa kikao hazipo, kwani sidhani kama haki itakuwa imetendeka. 

Mwenyekiti wa kikao aliwataka wajumbe wanaotaka kuendelea na kikao hicho wabaki ukumbini na wale ambao hawataki kuendelea na kikao hicho watoke nje. 

Baada ya wawakilishi hao kutoka, Mwenyekiti alisema hata kama watu hao wameondoka ni vyema kikao hicho kikaendelea kwa sababu ni muhimu kwa maslahi ya maendeleo ya manispaa hiyo. 

Alisema wajumbe waliobaki wanaonesha wazi kwamba hawatawaliwi na fedha pekee na kwamba inapobidi kuwa wazalendo inatakiwa wawe hivyo. Aliwapongeza viongozi wa CCM na Chadema kukubali kuendelea na kikao. 

Katika mkutano huo wajumbe walipitisha rasimu ya bajeti ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ya Sh bilioni 22.4 kwa kipindi cha mwaka ujao. Itatekelezwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa stendi mpya na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 10 katika manispaa. Kikao kilibariki Sh milioni 117 zilizotengwa kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanawake wa Tabora manispaa.


Habari Leo

1 comment:

Anonymous said...

This is a damn shame, rushwa mpaka inafanya watu wanagoma kutekeleza majukumu yao. Mwisho watadai attendance allowance kila siku wanapokwenda ofisini