ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 3, 2012

Zitto, Makamba wapingwa vikali

  Wasema urais si ngoma ya vijana
  Wataka umri wa miaka 40 uendelee
Wabunge vijana, January Makamba (CCM-Bumbuli) na Zitto Kabwe (Chadema-Kigoma Kaskazini)
Wazo lililoibuliwa na wabunge vijana, January Makamba (CCM-Bumbuli) na Zitto Kabwe (Chadema-Kigoma Kaskazini), kutaka umri wa kugombea urais upunguzwe kutoka miaka 40 hadi 35, limepingwa vikali na wasomi nchini, ambao wamesema hawakubaliani na umri wa miaka 35 kwa sababu ni mdogo katika kufanya maamuzi makubwa. 

“Sikubaliani na umri wa mgombea kuwa miaka 35, anatakiwa kukaa na kuelewa jinsi mfumo unavyofanya kazi…wengine unawakuta wanaanza kwa jazba, lakini baada ya muda anajirekebisha baada ya kuelewa jinsi mfumo unavyofanya kazi,” alisema Profesa Manoris Meshack, Makamu Mkuu wa kwanza wa Chuo Kikuu cha St. John mjini Dodoma. 


Alisema umri wa miaka 40 ni umri mwafaka kwa mtu kuwa rais kwa kuwa atakuwa amekaa kwenye mfumo kwa miongo miwili tangu alipotoka shuleni na hivyo kufahamu jinsi mfumo utenda kazi. 
Mwenyekiti Udomasa
Mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), Paul Loisoria, alitaka kuwepo kwa mjadala ambao utazungumzia umri unaofaa kwa mtu kugombea nafasi hiyo. 
Alisema mtu mwenye umri wa miaka 40 watu wanamtarajia ni mtu wa makamo ambaye anaelekea kutulia kimawazo. 
“Hata hivyo, tunahitaji kuweka ukomo wa umri wa mtu kugombea urais kama ni miaka 80 basi tutakavyoamua,” alisema. 
Mhadhiri RUCo
Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCo), Rwezaura Kaijage, alisema nafasi hiyo haistahili kupewa kijana kwa sababu urais ni taasisi nyeti na muhimu kwa taifa ambayo maamuzi yake hayapaswi kufanyika kiujana.
 “Lazima tutizame umri na nafasi ya urais katika sura mbili, kwanza ni asili ya ujana wenyewe katika rika la watu wenye miaka 35 ambao kihistoria bado wanaathiriwa na ujana kiasi cha kuwafanya watoe maamuzi yao kiujana. Pili, ni suala la kushuka kwa umri wa mwanadamu wa kuishi, ndiyo maana huo umri tunaukataa hata kama umri wa kuishi umepungua,” alisema Kaijage.



Kuhusu pendekezo la kurekebisha umri wa kupiga kura kutoka miaka 18 hadi miaka 16, Kaijage, ammbaye ni wakili wa Mahakama Kuu alisema kijana mwenye umri wa miaka 16 hana maamuzi yaliyokomaa kama mtu mwenye umri wa miaka 18.



ASKOFU MDEGELLA
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenberg Mdegella, alisema kuwa mawazo ya wanasiasa hao vijana, January Makamba na Zitto Kabwe kuhusu ndoto ya kupunguza umri wa kugombea urais ni uchemfu wa mawazo kwa kuwa huko ni kuchanganya tamaa ya madaraka na taasisi ya urais.



“Umri wa mgombea urais hauwezi kushuka hapo ulipo kwa sababu tatu ambazo ni hizi, kwanza lazima awe na karama ya uongozi ya kuzaliwa nayo, pili lazima apate mafunzo (elimu ambayo si ya kubabaisha) na tatu uzoefu wa taaluma ya uongozi na utawala. Sasa kwa huo umri wa miaka 35 atakuwa amejifunza nini zaidi ya mambo ya ujana wake…Wasitake cheap popularity (umaarufu) na waache kuchanganya tamaa ya madaraka na taasisi ya urais,” alionya Askofu Dk. Mdegella.



MHITIMU TEKU
 Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku) cha mkoani Mbeya, Kazamoyo Jidawaya, alisema kwa sasa asilimia 60 ya Watanzania ni vijana, hivyo anaunga mkono suala la kupunguza umri wa mtu anayestahili kugombea urais ili kutoa fursa kwa watu wanaoyajua vizuri matatizo yanayowakabili vijana.
Alisema kuwa kwa sasa vijana wanakabiliwa na matatizo ya kukosekana kwa ajira na mengine mengi, hivyo mtu anayestahili kuwangoza napaswa kuwa yule anayeguswa na matatizo hayo.
MWANAFUNZI OUT
Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) tawi la Mbeya, Eddo Makata, alisema kuwa anaunga mkono wazo hilo kwa vile anaamini kuwa mtu liyefikia umri wa miaka 35 anafaa kuongoza taifa hasa kwa nchi za Afrika ambazo zinakabiliwa na changamoto nyingi.
Alisema ikiwa nchi za Kenya na Burundi ambazo ni miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaruhusu mtu mwenye umri wa miaka 35 kugombea nafasi ya rais, haoni sababu kwa Tanzania kutoruhusu.
Dk. MWAKAJUMILO
Dk. Stephen Mwakajumilo alisema kuwa hakubaliani na wazo hilo kwa sababu anaamini kuwa kwa sasa taifa linazo changamoto nyingi ambazo zinahitaji mtu mzima, tena mwenye busara zaidi ili kukabiliana nazo.
“Nadhani umri wa kuanzia miaka 40 kwenda juu ndio unaostahili zaidi kwa mtu anayefaa kuliongoza taifa hili, hii ni kwa sababu kuna changamoto nyingi zinazolikabili taifa, hivyo suala la kupunguza umri hadi miaka 35 mimi sikubaliani nalo,” alisema Dk. Mwakajumilo.
Alisema Tanzania isiwaige marais vijana wa nchi jirani kama Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya kongo (DRC) na Pierre Nkurunzinza wa Burundi kwa kuwa wao walichukua madaraka katika mazingira tofauti ambayo hayawezi kufananishwa na changamoto zinazoikabili Tanzania hivi sasa. 
PROFESA BAREGU
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa toka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino (SAUT) kilichoko Mwanza, Profesa Mwesiga Baregu, amesema suala hilo ni muhimu, lakini si kipaumbele kwa vijana kwa kuwa kulenga urais moja kwa moja kunaleta picha kwamba urais ni kitu kikubwa katika kuunda serikali.
Profesa Baregu alisema kilicho muhimu katika uongozi wa nchi ni kuwa na serikali yenye tija inayozingatia uongozi bora na endelevu na kwamba hilo ndilo linalotakiwa kuangaliwa kwenye mjadala wa mambo ya kuingizwa kwenye katiba mpya.
“Urais bila ya kugusa sera au bila ya kuelewa huyu anayeutaka urais ana sera gani za kutuendeleza, ana mawazo gani ya kutuendeleza na bila ya kujua atatuelekeza wapi, haina maana. Mimi nawaasa vijana wasome kitabu cha Mwalimu Nyerere cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania,” alisema.
Kuhusu kupunguza miaka ya umri wa kupiga, Profesa Baregu alisema bado umri wa miaka 18 ni sahihi kwa kuwa mtu mwenye umri huo mbali na kupiga kura pia ana haki kisheria ya kupigiwa kura, na kwamba si busara kumpigia kura mtoto wa umri huo kuwa kiongozi kwa kuwa bado hajaufikia utu uzima.
DK. BENSON BANA
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kwamba maoni waliyoyatoa wabunge hao ni haki yao ya msingi, lakini akasema kwamba la muhimu kuangalia hapa ni sababu zilizofanya umri wa miaka 40 kuwa sifa ya kugombea urais kwenye katiba tuliyonayo.
Dk. Bana alisema mazingira yaliyoangaliwa kwa wakati huo ni umri aliokuwa nao mwalimu Nyerere wakati anaanza kuongoza nchi kwamba alikuwa na umri wa miaka 39 na bahati nzuri aliongoza nchi bila ya kutuangusha.
“Kwa hiyo kwa kweli utaona kwamba umri wa miaka 40 bado ni muhimu kwa kuwa ni wa mtu aliyekomaa, tofauti na kijana na ujana una mambo mengi. Cha msingi cha kujadili katika suala hili ni vigezo vya kuwa rais na viingizwe kwenye katiba yetu, awe ni mtu mwenye wajibu, aliye na mke na si kapera, analipa kodi na vitu vingine,” alisema.
Alisema ni vizuri umri wa miaka 18 ukabakia, kwa kuwa ni umri ambapo kijana anakuwa yuko tayari kuchukua majukumu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na kulipa kodi tofauti na mtoto wa miaka 16.
PROFESA MAKUNDI
Profesa mstaafu katika Chuo Kikuu cha California nchini Marekani, Willy Makundi, alisema nafasi ya kuongoza nchi si kazi lelemama, inahitaji mtu ambaye amekomaa kiakili na mwenye busara za kutosha katika kuamua mambo makubwa ambayo yanatoa hatma ya nchi.
“Ni nadra sana kukuta kijana wa umri huo anaweza kuamua mambo kwa busara ya hali ya juu na mwenye busara ya kutosha, wengi hata mambo ya familia yanawashinda na bado wako kwenye mambo ya ujana, hivyo hatuwezi kuwa na rasi wa umri huo mana tutaingiza pabaya...hii ni kauli ya kijinga,” alisema Profesa Makundi ambaye kwa sasa anaishi mjini Moshi.
Alisema urais unahitaji uzoefu, busara ya kutosha kwani ni meli kubwa inayohitaji muongozaji makini na asiye na papara kama za vijana, kwani ngazi hiyo ndio kubwa na ndiye Amiri Mkuu Jeshi, na anayeamua hatma ya maisha ya wananchi.
Imeandikwa na Godfrey Mushi, Iringa; Sharon Sauwa, Dodoma; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Salome Kitomari, Kilimanjaro na Raphael Kibiriti, Dar.

CHANZO: NIPASHE

No comments: