ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 30, 2012

Askofu aitisha kikao kujadili uchimbaji dhababu kanisani


Sakata la kuchimba dhahabu ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Usharika la Brandt wilayani hapa, limeanza kufanyiwa kazi na uongozi wa kanisa hilo ambapo Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele, ameitisha  kikao cha wazee wa kanisa leo kujadili suala hilo na kulitolea tamko.
Mchungaji wa kanisa hilo Usharika wa Brandt, Emanuel Lunda,  aliiambia NIPASHE kuwa, alisema Askofu Mengele ameamua kukutana na wazee wa kanisa hilo kujadili kilichotokea.
Zoezi hilo la kuchimbua dhahabu ndani ya kanisa hilo Usharika wa Brandt lilisistiswa Jumatano iliyopita baada ya kutokea vurugu za wananchi na kuhatarisha amani hali iliyopelekea polisi kuingilia kati. Kusitishwa kwa zoezi hilo kuliamuliwa na Askofu Mengele ambapo shughuli hiyo itaweza kuendelea ama kutokuendelea baada ya mkutano wa leo.
Mchungaji Lunda awali aliielezea NIPASHE kuwa uchimbaji wa  madini hayo  uliokuwa ukifanywa ndani ya kanisa hilo karibu na madhabahu ulilenga kutafuta dhahabu ambazo inadaiwa zilichimbiwa chini na wamisionari wa Ujerumani waliolijenga kanisa miaka ya 1908.

Alisema kabla ya vurugu hizo kutokea na kutolewa amri ya kusitishwa kwa zoezi hilo, tayari walikuwa wamechimba urefu wa zaidi ya futi 10 lakini hakuna dhahabu iliyokuwa imepatikana.
Mchungaji Lunda alisema pia fedha hizo ambazo zingetokana na kuuza dhahabu hiyo, zingetumika kujenga kanisa jipya la kisasa, nyumba ya mchungaji na ya Mwinjilisiti wa mtaa wa kanisa hilo pamoja na kuweka huduma ya umeme.
Alisema tetesi za kuwepo dhahabu ndani ya kanisa hilo  kwa muda mrefu zilikuwa zikienezwa na baadhi ya wakazi wa kjijiji cha Ihahi ambapo Mkuu wa Jimbo la Chimala, Laulent Ng’umbi naye, alidokezwa suala hilo ambaye naye aliwaeleza viongozi wa Dayosisi ya Kusini na hivyo kuamuriwa kufanyike utafiti wa madini hayo kwa kuchimba ndani ya kanisa.
Alisema mwanzoni mwa Aprili, 2012,  uongozi wa Dayosisi, Jimbo na Usharika baada ya majadiliano ya suala hilo, waliitwa wataalamu wa madini ambao walipima ndani ya kanisa kwa kutumia vifaa maalum vya madini mara tatu kwa nyakati tofauti na kugundua kuwa kulikuwa na madini ndani ya kanisa hilo.
Alisema mara ya tatu wataalam hao walipofika katika kanisa hilo kwa ajili ya kupima madini hayo waliambatana na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kusini,  Mwamisole;  Mkuu wa Jimbo la Chimala, Laulenti Ng’umbi’ Mchungaji wa Jimbo la Chunya, Mchungaji Mbilinyi na Mkuu wa Jimbo la Mtwara-Lindi, Mchungaji Mbedule ambapo baadaye iliamuriwa kuwa ufanyike utafiti kwa kuchimba.
CHANZO: NIPASHE

No comments: