ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 30, 2012

Mwili wa aliyezikwa hai wafukuliwa


Mwili wa mkazi wa kitongoji cha Itezi Magharibi katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Nyerere Kombwee, aliyezikwa na wananchi wenzake akiwa hai baada ya kutuhumiwa kuwa mchawi umefukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Diwani wa kata ya Itezi, Frank Maemba, alisema viongozi wa kata hiyo kwa kushirikiana na polisi wamefanikiwa kuufukua mwili wa mtu huyo na kuupeleka katika Hospitali ya Rufaa Mbeya ili kusubiri taratibu za kuuzika upya ziweze kufanyika.
Maemba alisema uongozi pamoja na wanafamilia wamekubaliana kuwa mtu huyo atazikwa katika kaburi hilo alilofukiwa akiwa hai ambalo awali lilikuwa limechibwa kwa ajili ya kumzika mtoto wa kaka yake Leonard Kombwee.
Alisema kwa upande wa mtoto Leonard ambaye alifariki katika mazingira ya kutatanisha akihusishwa kulogwa na Nyerere Kombwee ambaye naye ni marehemu, atazikwa katika kaburi jingine ambalo limechibwa katika makaburi ya ukoo.

Diwani huyo alisema hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi.
Juzi wananchi wanaodaiwa kuwa na hasira kali wa kitongoji cha Itezi Magharibi walimzika akiwa hai mkazi mwenzao, Nyerere Kombwee, wakimtuhumu kuwa ni mchawi. Wananchi hao walichukua uamuzi huo wakimhusisha na kifo cha mtoto mdogo wake Leonard Kombwee ambacho kimetokea katika mazingira yenye utata Aprili 27 mwaka huu.

No comments: