ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 4, 2012

Mabomu ya Polisi yatanda Ubungo

  Ni operesheni kuwaondoa wamachinga
  Nao wajibu kwa kuwarushia polisi mawe
Mapambano yaliyohusisha mawe, mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kati ya askari polisi na wafanyabiashara ndogondogo, maarufu kama “Wamachinga”, yalizuka jana na kusababisha tafrani na hofu kubwa miongoni mwa wakazi, wafanyakazi, wafanyabiashara na wapita njia katika eneo la Ubungo, jijini Dar es Salaam.


Mapambano hayo yalizuka baada ya askari polisi, wakiwamo askari kanzu wakishirikiana na wale wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, kuendesha operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara hao katika maeneo hatarishi na yale yasiyoruhusiwa kufanya biashara katika maeneo mbalimbali ya Ubungo.
Maeneo hayo ni pamoja na kwenye kituo cha daladala cha Ubungo Mwisho, Ubungo Maji, Ubungo Mataa hadi darajani (Barabara ya Mandela), eneo la kituo cha kuzalisha umeme cha Songas na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hadi Riverside, Ubungo Mataa hadi darajani kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam -UDSM (Barabara ya Sam Nujoma) na Ubungo Mataa hadi Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo-UBT (Barabara ya Morogoro).
Askari hao wakiongozwa na baadhi ya maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi na walianza kuwaondoa wafanyabiashara hao katika maeneo hayo kuanzia saa 9.00 usiku wa kuamkia jana, kwa kuvunja na kuondoa meza na vibanda vinavyotumiwa na wafanyabiashara kuuza bidhaa zao.
Miongoni mwa meza zilizovunjwa na kuondolewa na askari hao katika maeneo hayo, ni pamoja na zile zinazotumiwa na wauza magazeti.
Hatua hiyo ilisababisha jana, wauzaji wa magazeti kulazimika kupanga magazeti chini, huku baadhi yao wakilalamikia hali hiyo.
ya kuondolewa katika maeneo yao ya kufanyia biashara, ilipingwa vikali na wafanyabaishara hao walioonekena kuwa na hasira na hivyo kuanza kuwarushia askari hao mawe kwa wingi na mfululizo.
Kwa jinsi mawe hayo yalivyokuwa yakirushwa kwa wingi na wafanyabiashara hao, yalionekana mithili ya kundi la ndege likiruka angani.
Mawe hayo yalianza kurushwa na wafanyabiashara hao katika eneo la Ubungo Maji kuanzia saa 1:00 asubuhi.
Katika tukio hilo, gari moja linalosadikiwa kuwa ni la polisi, lilivunjwa kioo.
Mbali na kurusha mawe, wafanyabiashara hao walifunga Barabara ya Mandela, katika eneo la Songas baada ya kuweka mawe makubwa kuzuia magari kupita.
Hali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa magari kwa takriban saa moja.
Wafanyabiashara hao walidai kuwa wameamua kufunga barabara hiyo ili kushinikiza Mbunge wao Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika, aende eneo hilo kuwatetea wasiondolewe katika maeneo yao ya kufanyia biashara.
Hali hiyo ilionekana kuwazidi nguvu askari polisi wa kawaida, askari kanzu na wale wa Halmashauri ya Manispaa waliokuwa mstari wa mbele kuendesha operesheni hiyo dhidi ya wachuuzi hao.
Hivyo, wakalazimika kuomba msaada kutoka askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
FFU walifika eneo hilo wakiwa kwenye magari manne aina ya Land Rover na gari moja la kurusha maji yenye kemikali za kuwasha mwilini.
Askari hao wakiwa wamebeba mabomu ya machozi, bunduki za risasi za moto na zile za mipira pamoja na virungu tayari kwa mapambano, walianza kufyatua mabomu ya machozi na kurusha maji ya kuwasha kuwatawanya wachuuzi hao.
Wachuuzi hao pamoja na wapita njia, walianza kukimbia hovyo katika maeneo mbalimbali, huku watu waliokuwa majumbani wakijifungia ndani ya nyumba kunusuru maisha yao.
WATU 34 MBARONI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema watu 34; wanaume na wanawake, walikamatwa na polisi. Kati yao tisa walifikishwa mahakamani jana na waliobaki watafikishwa mahakamani leo.
Mabomu na maji hayo yalirushwa kwa dakika kadhaa, hali ilirejea kuwa shwari na magari kuruhusiwaa kuendelea na safari baada ya vizuizi vilivyokuwa vimewekwa barabarani na wachuuzi hao kuondolewa na polisi.

DC RUGIMBANA: OPERESHENI YA KAWAIDA
Baada ya hali kuwa shwari, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, aliyekuwa katika eneo hilo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa operesheni hiyo ni ya kawaida na kwamba, hawataruhusu wachuuzi kuyatumia maeneo hayo kufanya biashara.
Alisema katika kutekeleza amri hiyo, maeneo hayo sasa yatawekewa ulinzi kuzuia biashara kufanyika.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, akiwa eneo la tukio, aliwataka wafanyabiashara kuondoka katika maeneo hayo na kwenda kule walikopangiwa na manispaa.
Alisema maeneo ya karibu na mitambo ya Tanesco waliyokuwa wanafanyia biashara ni ya hatari kwa vile unapita umeme mkubwa.
Kenyela alisema hivi asa ni marufuku maeneo yaliyokatazwa, kufanya biashara, si katika nyakati za mchana tu, bali usiku pia.
“Soko la saa 12 pia marufuku. Sasa we njoo usiku na vitunguu vyako hapa uone. Hatufanyi kwa nia mbaya, bali kwa faida yao (wafanyabiashara ndogondogo),” alisema Kamanda Kenyela.
 Hata hivyo, dakika chache baada ya Rugimbana na Kamanda Kenyela kueleza hayo, wachuuzi hao walijikusanya karibu na eneo la darajani na kuanza kuimba nyimbo mbalimbali za kusifu juhudi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, huku wakitoa matamshi ya kupinga kuondoka maeneo waliyoondolewa.
Kitendo hicho kiliwatia hasira FFU ambao walianza kuwatawanya kwa kuwarushia mabomu ya machozi na kupiga hewani risasi za mipira.
Wachuuzi hao waliochanganyika na vijana wanaosadikiwa kuwa ni wabwia dawa za kulevya, maarufu kama ‘mateja’, walianza kukimbia hovyo kwa mara ya pili.
Hata hivyo, juhudi hizo za kujinusuru hazikufua dafu, kwani baadhi yao walitiwa mbaroni na polisi.
Baadaye, hali ilirudi kuwa shwari, lakini askari hao waliendelea kuweka ulinzi katika maeneo hayo.
Majira ya sasa 8:20, wachuuzi hao walirejea na kuchoma taili barabarabi, lakini polisi waliingilia kati na kuwasambaratisha tena.
Akizungumza katika kikao kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, viongozi wa Tanesco na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Kenyela alisema operesheni hiyo ilifanyika kwa amani na salama bila ya mtu yeyote kujeruhiwa wala kufa.
Alisema wamejiandaa kikamilifu kupambana na mfanyabiashara yeyote atakayejaribu kufanya biashara usiku katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema operesheni hiyo ni mwanzo wa kutatua kero jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, aliwataka wafanyabishara hao kutokata tamaa, badala yake waende kuendelea na biashara katika maeneo yaliyoandaliwa na ili kujenga nidhamu nchini na kuonya kuwa hawatamvumilia yeyote atakayejaribu kufanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Sadiki alisema operesheni iliyoanza jana, ni tukio la awali katika operesheni zinazotaka kufanywa na serikali jijini Dar es Salaam.
Sadiki alisema Ubungo imekithiri uvamizi wa maeneo nyeti unaofanywa na baadhi ya watu kwa kisingizio cha wafanyabiashara au wajasiriamali ambao alisema wanasahau ujasiriamali unaweza kubadili sura ukawa na madhara.
Alisema operesheni hiyo si nguvu ya soda kama itakavyodhaniwa na baadhi ya watu, bali itakuwa ya kudumu katika maeneo yote yasiyoruhusiwa, ikiwamo kituo cha daladala cha Mwenge ili kurejesha nidhamu na usalama mkoani Dar es Salaam.
“Wapo wajasiriamali, lakini wengine ni wezi tu, ndio hao hao wanajihusisha na dawa za kulevya na bhangi,” alisema Sadiki.
Katika hatua nyingine, Sadiki aliwataka watu wote waliojenga katika maeneo ya njia za umeme kuondoka mara moja kwa hiari kwa vile maeneo waliyojenga ni nyeti, vinginevyo wataondolewa kwa nguvu.
Alisema serikali imekwishamuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco kupeleka orodha ya watu wote waliojenga katika maeneo hayo.

MKURUGENZI TANESCO: TUNAJADILIANA NAO
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, alisema wanaendelea na majadiliano na watu hao kama majirani kuhusu suala hilo.
Sadiki pia aliwataka watu wote wanaochimba mchanga na kokoto maeneo ya Pugu, katika msitu wa Kazimzumbwi, kuanzia leo, waache mara moja kuchimba kwa vile hayo ni machimbo haramu na kunaharibu mazingira.
Alisema machimbo hayo ni haramu kama biashara ya dawa za kulevya na kwamba, wanaochimba hawajapewa kibali na halmashauri na wala manispaa haipati hata senti moja.
CHANZO: NIPASHE

No comments: