ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 13, 2012

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Iddi Afungua Kikao cha Viongozi wa Serikali, Siasa na Taasisi za Kijamii Juu ya Sensa ya Watu Zanzibar

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Tanzania ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Alio Iddi akikifungua kikao cha Sensa kwa wakuu wa Mikoa, Wilaya na Maafisa Tawala wa Zanzibar hapo Jumba la Wananchi Forodhani.
Baadhi ya Wakuu wa Mikoa,Wilaya na Maafisa Tawala wa Zanzibar wakifuatilia Hotuba ya Ufunguzi wa Kikao cha Sensa ya Watu na Makazi iliyotolewa na Mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Sensa Kitaifa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Kikao hicho kilifanyika hapo katika ukumbi wa Jumba la Wananchi Forodhani Mjini Zanzibar
---
Ushirikiano wa pamoja kati ya Viongozi wa Serikali, Siasa pamoja na Taasisi za Kijamii ndio utakaowezesha ubora wa maandalizi hadi kufikia kukamilika kwa zoezi zima la Sensa ya Watu na Makazi hapa Nchini.

Akikifungua Kikao cha Wakuu wa Mikoa , Wilaya pamoja na Maafisa Tawala wa Zanzibar hapo Ukumbi wa Jumba la Wananchi Forodhani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hakuna Kiongozi asiyeelewa umuhimu wa Sensa kwa Maendeleo ya Taifa.

Balozi Seif alieleza kwamba Takwimu za Sensa wakati wote husaidia Serikali katika kufuatia utendaji wake hasa Dira ya Taifa ya Mwaka 2020 pamoja na Mpango wa kupunguza Umaskini Zanzibar { Mkuza }.

Alisema Viongozi hao wana jukumu kubwa la kuhakikisha Taratibu nzima za Maandalizi ya Sensa katika kutoa Elimu ni vyema yanawafikia kwa wakati walengwa ambao ni Wananchi.

“ Wakati muda unazidi kukaribia kinachohitajika zaidi hivi sasa ni uhamasishaji wa karibu kwa Jamii”. Alisisitiza Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi.

Balozi Seif aliwaeleza Wakuu hao wa Mikoa, Wilaya ya Maafisa Tawala wao kwamba utayarishaji wa Maeneo ya Kuhesabia Watu hapa Zanzibar umeshakamilika likiwemo pia suala la Dodoso linalokadiriwa kuchukuwa takriban dakika 50 kila Kaya kwa lile Dodoso kubwa.

Akitoa Taarifa juu ya Matayarisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 Mtakwimu Mkuu wa Serikali Nd. Mohd Hafidh alisema zoezi la Sensa hasa katika Bara la Afrika limekuwa likikabiliwa na ufahamu finyu wa umri kwa Baadhi ya Watu ndani ya Jamii.

Nd. Mohd Hafidh alisema tatizo hilo kwa kiasi Fulani limekuwa likiviza Mipango ya Kiuchumi na Maendeleo kwa Mataifa hayo ya Bara la Afrika.

Alisisitiza kwamba kadri kasi ya uhamasishaji itakavyoendelea kuwa kubwa ndivyo Changamoto zilizopo kwenye uhamasishaji huo zinaweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Nd. Mohd alieleza kuwa zoezi la Sensa halihitaji kuzuia shughuli za Wananchi lakini cha msingi ni kuhakikisha muhusika Mkuu wa Kaya anawajibika kuwa na kumbu kumbu na vielelezo vyote vya Familia anayoishi nayo.

Hata hivyo Mtakwimu Mkuu huyo wa Serikali aliwaomba Wakuu hao wa Mikoa, Wilaya na Maafisa Tawala wao kuangalia vibali vya Shughuli zote zinazokusanyisha Watu kwa usiku wa kuamkia siku ya zoezi la Sensa vinazuiliwa kwa muda.

Wakichangia Taarifa hiyo kuhusu Matayarisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 baadhi ya Wakuu hao wa Mikoa na Wilaya wameitahadharisha Serikali kuwa makini na baadhi ya Vikundi vinavyojihusisha na uhamasishaji ndani ya Jamii ambao uko nje ya Maadili ya malengo ya Taasisi zao.

Wamesema uhamasishaji huo tayari umeanza kutoa cheche za muelekeo wa shari, Vurugu na uvunjifu wa Amani katika maeneo mbali mbali hapa Zanzibar.

“ Ukwel lazima tuuseme. Wapo Vigogo waliojificha nyuma ya Vikundi hivyo wakichochea wimbi hilo lenye ishara mbaya ya kulipeleka Taifa katika Migogo isiyotambulika hatma yake”. Walitahadharisha baadhi ya washiriki wa kikao hicho.

Sensa ya Watu na Makazi inayokadiriwa kugharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 27 za Kitanzania inatarajiwa kufanyika Usiku wa Jumapili wa Tarehe 26 Mwezi wa Nane mwaka 2012.
 
Na
 Othman Khami Ame 
Ofisi Ya Makamu Wa Pili Wa Rais Zanzibar

No comments: