ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 7, 2012

Malima:Maisha yangu ya soka yalikuwa na mikosi

Image

NI zaidi ya muongo mmoja sasa tangu beki mahiri wa Yanga, Simba na timu ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Bakari Malima alipokamatwa na Maofisa Usalama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere akitokea Afrika Kusini alipokuwa akicheza soka ya kulipwa kwenye klabu ya Vaal Professional. 

Malima alikamatwa na Maofisa Usalama wa uwanja huo akituhumiwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na hivyo kumlazimu kulala uwanjani hapo kwa muda wa siku moja kabla ya siku inayofuata kufunguliwa kesi kwenye Mahakama ya Kisutu kujibu tuhuma hizo.
 

Baada ya kupita kipindi chote hicho Bakari Malima ameamua kuzungumza na HabariLeo kuweka wazi kisa chote hicho na mazingira yaliyosababisha kukamatwa kwake, ambapo kulihusishwa na mwanamke mmoja mfanyabiashara aliyekuwa anafahamiana naye tangu Afrika Kusini. 

Malima anasema baada ya kuichezea Vaal Professional kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu 
mwaka 1997 kuisha, alipata mapumziko mafupi kujiandaa kwa ajili ya mzunguko wa pili, hivyo aliwaomba viongozi wa timu hiyo kurudi nyumbani kwa mapumziko. 

Lakini Malima anadai wakati anacheza soka nchini Afrika Kusini walikuwa karibu na Watanzania waliokuwa wakiishi nchini humo na kutokana na hilo akajikuta anajenga mazoea na mwanamke mmoja wa Kitanzania ambaye alimfahamu kama mfanyabiashara. 

“Nilizoeana naye sana huyo mwanamke kiasi cha kunitambulisha kwa jamaa yake, ikawa siku 
moja huyo mwanamke kwenye utaratibu wa biashara zake alirudi Tanzania na kufika uwanja wa ndege ndipo maofisa usalama wakamng’ang’ania na siku iliyofuata nami nikawa narudi 
nyumbani kwa mapumziko yangu, yeye akifika kama leo, mimi kama kesho yake,” 
anasimulia Malima. 

Baada ya kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere siku inayofuata Malima alisema kuwa alikaguliwa mizigo yake kama walivyokaguliwa abiria wengine na kuruhusiwa 
kuondoka kwani hawakumkuta na kitu ambacho kingewafanya wamkamate. 

“Ile nataka kuondoka tu nikasikia jamaa ananiita kama mwandishi, nikageuka nikamwambia kama ni mwandishi tutaonana kesho, maana nimechoka sana na safari,” anasimulia Malima. 

Malima anasema kuwa hata hivyo yule jamaa alimsihi arudi kwa kumwambia kuwa yeye hakuwa mwandishi hali iliyomlazimu kusimama na kumsikiliza, ndipo huyo jamaa alipotoa kitambulisho chake kinachomtambulisha kama askari na kumtaka aende naye ofisini kwake. 

Hata hivyo, Malima anasema haikuwa rahisi kumkubalia kwani alibishana naye kwa muda kadhaa ndipo alipokubali kuongozana naye mpaka ofisini kwa huyo askari. 

“Ile naingia ofisini kwake tu wakaingia jamaa kama kumi hivi, nikaona saluti zinapigwa, kukaa kidogo akaingia askari mwingine ambaye ni bosi zaidi ya wale waliokuwepo, saluti zikapigwa zaidi,” alisema Malima. 

Malima anasema mara baada ya kupigiana saluti askari hao walianza kumhoji kwa kumwambia kuwa wao wanamfahamu kuwa ni mtu fulani ila awaambie ametokea wapi na huko alikokuwa alikuwa anajishughulisha na kitu gani. 

“Niliwaambia kuwa mimi nimetoka Afrika Kusini ambako nacheza soka ya kulipwa kwenye klabu ya Vaal Professional, kifupi niliwaambia kila kitu,” alisema Malima aliyekuwa akijulikana kwa jina la utani la Jembe Ulaya miongoni mwa mashabiki wa soka nchini kwa jinsi ya uimara wake kwenye nafasi ya ulinzi. 

“Kuna mwanamke fulani ameingia jana kutoka Afrika Kusini, anaitwa fulani unamfahamu? 
Nikawaambia kuwa namfahamu, wakaniuliza unamfahamu kivipi na kama hatuna mahusiano yoyote, nikawajibu kwa jinsi ninavyonifahamu na nikawaambia sina uhusiano naye wowote, walikuwa wakimaanisha uhusiano wa kimapenzi,” anasimulia Malima. 

Baada ya maelezo hayo, Malima anadai kuwa askari hao walimuweka chini ya ulinzi na kumuamuru avue kila kitu kwa ukaguzi zaidi. Baada ya kuwaambia hivyo Malima anadai aliwaomba askari hao wamtajie kosa lake kwani muda wote huo walikuwa bado hawajamtajia 
kosa lake. 

Ndipo askari hao wakamwambia kuwa kuna mwanamke anatokea Afrika Kusini amekamatwa na dawa za kulevya na kwamba huyo mwanamke amemtaja yeye (Malima) kuwa wanafahamiana naye. 

“Baada ya kuambiwa hivyo nikataharuki kidogo, nikahoji je amenitaja, je nina husika au la,” wakaniambia kuwa amenitaja kama mimi ninafahamu kuwa huyo mwanamke anafanya biashara halali, ila wakaniambia kuwa waliona bora waniweke chini ya ulinzi niwasaidie zaidi.” 

Malima anadai kuwa hata hivyo alimhoji huyo mwanamke kuwa kwanini amemtaja na huyo 
mwanamke akamwambia kuwa amemtaja ili amtetee kuwa anafahamu kuwa hajihusishi na biashara yoyote ile haramu. 

Malima anadai kuwa kwa maelezo ya huyo mwanamke anadai tangu wakiwa angani kuwa kuna mtu alimtaka kimapenzi lakini alimkatalia ndipo huyo mtu alipomwambia kuwa lazima atamuonesha wakifika uwanja wa ndege. 

Mara baada ya kufika uwanja wa ndege Malima anadai kuwa kwa mujibu wa maelezo ya huyo mwanamke kuwa huyo jamaa aliyemtongoza akawahi kushuka na baadaye alipokuja kushuka akajikuta yuko mikononi mwa Polisi. 

“Nilikaa uwanja wa ndege kwa muda wa siku mbili na siku ya tatu wakatupeleka pamoja na yule 
mwanamke mahakamani Kisutu,” anasema. 

Malima anadai kuwa mara baada ya kufikishwa mahakamani Kisutu ndugu zake na watu wa Yanga wakafika kuwawekea dhamana sambamba na huyo mwanamke, kwani isingekuwa vizuri kama wangemuwekea dhamana yeye pekee wakati wamekamatwa wote. 

“Watu wa Yanga walinifuata wakaniambia kuwa niwataarifu kilichotokea Vaal Professional watanielewa, nami nilifanya hivyo,” anasema. Malima anasema kwamba wakati kesi inanguruma mahakamani watu wa Yanga wakamletea fomu asajili ili washughulikie matatizo yake. 

“Wakaniambia nichague moja nisajili ili walimalize suala langu au la, kwa kuwa nilikuwa kwenye matatizo sikuhoji hata masuala ya fedha, nilisajili tu ili liishe,” anasema. “Nashukuru walinisaidia na wote tukaachiwa na msimu wa mwaka 1998 nikaanza kuchezea tena Yanga,” anasema. 

Malima anasema alidumu na Yanga mpaka mwaka 2000 na kutimkia Oman kujiunga na klabu ya Sur Sport ambapo aliichezea timu hiyo kwa muda, kwani timu hiyo ilikiuka makubaliano yao. 

Sur Sport pia alikuwa akiichezea mshambuliaji wa zamani wa Simba, Bita John Musiba ambaye alimshauri Malima arudi nyumbani. Alirudi Tanzania mwaka huo huo 2000 na kujiunga tena na Yanga lakini anadai kuwa kutokana na mizengwe ya kiongozi mmoja wa timu hiyo (jina tuna lihifadhi) alikaa nje msimu mzima bila kucheza. 

“Kiongozi huyo wa Yanga alikuwa ananipakazia kuwa wasinisajili kwa sababu mimi ni msumbufu nilikuwa nasafiri mara kwa mara, bado nilipenda kuendelea kuichezea Yanga,” anasema Malima. 

Malima anadai kuwa kwa kuwa shughuli yake ni kucheza soka alishindwa kukataa ofa aliyoletewa na viongozi wa Simba waliomtaka kujiunga na timu hiyo katikati ya msimu wa mwaka 2000. 

Alidumu na Simba kwa kipindi cha miezi mitatu na kuchukuliwa na kocha mchezaji wa zamani wa Simba, Hassan Afiff ili na kujiunga na timu aliyokuwa akiifundisha ya Itifaq ambayo aliichezea kwa misimu mitatu kuanzia 2001 mpaka 2003 ambapo mkataba wa kuichezea timu hiyo ukawa umekwisha. 

Alirejea nchini na kujiunga na timu ya Twiga Stars iliyokuwa ikimilikiwa na Idd Azan ambaye kwa sasa ni mbunge wa Kinondoni, lakini hakudumu sana alipata nafasi ya kwenda Denmark na baadaye Sweden pamoja na wachezaji Anwar Awadh na Athumani Mchuppa. 

Akiwa Sweden Malima aliibiwa pasipoti yake ya kusafiria na raia mmoja wa Somalia aliyekuwa akiishi naye chumba kimoja. Kutokana na hilo Malima alilazimika kurudi Tanzania na kujiunga tena na Twiga Stars mpaka mwaka 2006 alipoamua kustaafu rasmi kucheza soka. 

“Ukweli maisha yangu ya soka yalitawaliwa na mikosi sana lakini yote namshukuru Mungu, kwani huwezi jua alikuwa ananiepusha na nini,” alisema Malima ambaye pia aliwahi kutamba na timu ya Pan African ambayo ilimuibua na kuonekana na Yanga. 

Akizungumzia soka la sasa Malima anasema kuwa vijana wanajitahidi kulingana na wakati wenyewe uliopo lakini anadai kuwa kama wangejitahidi zaidi wangeweza kufika mbali. “Ona kwa sasa kila mchezaji karibuni ana gari ingekuwa rahisi kwao kuendesha magari yao mpaka ufukweni na kufanya mazoezi ya ziada,” anasema. 

Malima anasema alikuwa akikoshwa na soka la Athumani Juma Chama, marehemu Method Mogella, Constantine Kimanda na mjomba wake Mohamedi Bakari ‘Tall’ aliyewahi kutamba na Simba. 

ALIPO SASA 
Baada ya kuachana na soka Malima alipata kazi kwenye kampuni ya mgodi wa dhahabu ya Barrick akiwa kama mwendaji mashine, kazi aliyoifanya mpaka mwaka 2011 na kuachishwa kutokana na mgogoro kati ya Watanzania na wageni kwenye mgodi huo yeye akiwa kama 
Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi kwenye mgodi huo. 

Malima anadai kuwa kutokana na mgogoro huo wageni wakamfanyia fitina iliyomsababishia kupoteza kazi yake. Anadai mara baada ya kupoteza kazi hiyo alifanya juhudi za kuwasiliana na Rais Jakaya Kikwete, aliyemuelekeza kwa Waziri wa Nishati na Madini, Wiliam Ngeleja ili atatue tatizo lake. 

Anadai alionana na Ngeleja na kumuelezea kwa kina matatizo kwenye mgodi huo na kumuahidi kuwa angelishughulikia lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika na yeye bado anaendelea kukaa bila kazi na kupoteza haki zake za msingi kipindi anafanya kwenye kampuni hiyo. 

Kwa sasa anaishi Mbezi Makabe, akiwa na mke na watoto watatu ambao ni Ngida, Arafat na Ridhiwani.


Habari Leo

No comments: